Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Jinamizi la Nii Lamptey liwaepuke Serengeti Boys

PUM 01


WAKATI Watanzania wote tukijiandaa kuwatazama na kuwashangilia vijana wetu wa Serengeti Boys kwenye fainali ya leo ya AFCON U-17 dhidi ya mabingwa watetezi Senegal, ningependa kwenda hatua moja zaidi mbele...maisha yao baada ya fainali hii.


Nilibahatika kufuatilia kwa ukaribu sana fainali za Kombe la Dunia kwa vijana chini ya miaka 20 mwaka 2005. Kwa hapa nchini zilioneshwa na kituo cha DTV ambacho baadaye channel yake ilinunuliwa na Azam TV na sasa ndiyo ZBC2.


Wakati ule DTV ilikuwa na maudhui mawili makubwa, mashindano haya ya vijana na tamthilia moja iliyoitwa La Mujer de Lorenzo...nilikuwa sikosi.

Fainali iliwakutanisha Nigeria na Argentina na muda kama huu kuelekea mchezo huo, majina mawili yalitawala; John Obi Mikel wa Nigeria na Lionel Messi wa Argentina.

PUMZI Pict

Hata hivyo, jina la Mikel Obi ndilo lilikuwa mbele kwa takwimu bora za kiufundi, kwenye mbio za kuwania mchezaji bora wa mashindano.

Ni bahati mbaya kwake Nigeria ilipoteza 2-1 fainali ile huku mabao ya Argentina yote yakifungwa na Messi...akamzidi na kuwa mchezaji bora.


Mikel alitabiriwa makubwa sana na kweli akaja kuwa mchezaji mkubwa akizigombanisha timu kubwa za England, Chelsea na Manchester United...na baadaye kutamba na Chelsea kwa zaidi ya miaka 10.

Lakini kabla ya Kombe la Dunia la chini ya miaka 20, dalili za Mikel kuja kufanikiwa zilianza kujionyesha kwenye Kombe la Dunia chini ya miaka 17 nchini Finland.

SERE 01

Hata kwa vijana wetu wanaocheza fainali leo, dalili zimeanza kuonyesha kwenye mashindano haya.

Nyota kama Issa Mussa Chole aliyetwaa tuzo mbili za mchezaji bora wa mechi; hatua ya makundi dhidi ya Msumbiji na  nusu fainali dhidi ya Misri, pamoja na Chande Alwatan aliyetwaa tuzo ya mchezaji bora wa robo fainali dhidi ya Algeria, wameanza kuvutia klabu kubwa.

Mambo yakiwaendea vizuri, vijana hawa na wenzao wanaweza kupita njia ya Mikel na kuja kuwa nyota wakubwa baadaye.

Lakini hata hivyo, kwa kila Mikel mmoja, ambaye alienda mbali na kushinda EPL na Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na Chelsea na AFCON akiwa na Nigeria, kuna kina Nii Lamptey kibao ambao walitabiriwa makubwa lakini hawakufika.

Ni huyu Nii Lamptey ndiye ninayetaka kuzungumzia leo kuelekea fainali ya kihistoria kwa vijana wetu.

SERE 02

Jina lake halisi ni Nii Odartey Lamptey, alizaliwa Desemba 10, 1974 nchini Ghana na kama walivyo nyota hawa tunaowaangalia leo, yeye aliangaliwa namna hii kwenye mashindano kama haya ngazi ya dunia mwaka 1991.

Nii Lamptey anatajwa kama nyota wa Afrika aliyejaaliwa kipaji kikubwa zaidi ambaye hakufikia matarajio kwa alichokionyesha katika ngazi kama hizi.

Aliiongoza Ghana kushinda Kombe la Dunia la chini ya miaka 17 mwaka 1991 akiwa na kina Sammy Kuffour, aliyekuja kung'aa na Bayern Munich kwa miaka zaidi ya 10 mfululizo.

Mashindano ya mwaka 1991 yalishirikisha nyota wa baadaye kama Alessandro Del Piero wa Italia na Juan Sebastian Veron wa Argentina, lakini hakuna aliyemsogelea Nii Lamptey kwa kipaji hata kidogo.

SERE 03

Mfalme wa mpira, Pele wa Brazil, alimtaja  Lamptey kama mrithi wake halisi kutokana na uwezo wake na alisema hajawahi kuona mchezaji mwenye uwezo kama wake baada ya yeye mwenyewe.

Lamptey alilianza balaa lake kwenye mashindano ya FIFA ya chini ya miaka 16 yaliyofanyika Scotland 1989, akiwa na miaka 14 tu, Pele akiwa jukwaani, kisha akaja kutamba kwenye U-17 ya 1991 ambayo Ghana ilibeba. AFCON U-20 1993 Ghana ikafika fainali na akashinda medali ya shaba ya Olimpiki Barcelona 1992 na fainali ya Kombe la Dunia U-20 mwaka 1993.

Akiwa na miaka 18, tayari Nii Lamptey alikuwa nyota mkubwa anayetarajiwa kuibeba dunia mabegani mwake, lakini kwa bahati mbaya huo ndiyo ukawa mwisho wa umaarufu wake na alikuwa maarufu kuanzia alipokuwa na umri wa miaka 14 hadi 18...baada ya hapo akapotea.

SERENGETI Pict

KWA NINI

Hili ndilo somo ninalotaka liwafikiwe watoto wetu wanaocheza fainali leo, na wasimamizi wao. Nii Lamptey hakufeli kwa sababu ya uwezo mdogo bali kukwama kwa kipaji chake kutokana na usimamizi mbaya.

Kung'aa kwake kukampitisha njia mbaya na kuangukia kwa mawakala matapeli, waliowaza matumbo yao badala ya maendeleo ya kipaji cha mtoto.

Mwaka 1990 akiwa na miaka 15, alichukuliwa kimagendo kwa hati ya bandia ya kusafiria kwenda Ubelgiji.

Hapo ndipo safari yake ya uharibifu ilipoanza na akiwa na miaka 16 akaanza kucheza ligi kuu Ubelgiji na akawa tegemeo kwa timu yake na matika msimu wake wa kwanza tu, akafunga mabao 7 kwenye mechi 14...hatari

Hakuachwa atulie sehemu moja ili aendelee kukua kidogo kidogo. Mawakala walikuwa wakilala wakiamka wanamtafutia timu mpya ili wapate pesa. Akapelekwa PSV ya Uholanzi na kabla hajakaa sawa akauzwa England kwenye klabu ya Aston Villa na baadaye Coventry City. Kuanzia 1990 akiwa na miaka 15 hadi 1994 akiwa na miaka 18, akawa tayari amecheza klabu nne.

Katika kipindi ambacho alitakiwa aachwe akue ili apate maendeleo ya kiufundi, akawa anatumika kama mtu mzima...akadumaa. Badala ya kwenda mbele, Nii Lamptey akarudi nyuma na kushindwa kufikia matarajio.

Vijana wetu wanaocheza leo, wengi wao wana umri ule ule wa Nii Lamptey wa 1991 alipoishika Dunia kwenye Kombe la Dunia la U-17. Huu ndiyo umri ambao mawakala huwawinda watoto hawa ili wawapitishe njia ya Nii Lamptey, wao wapate pesa bila kujali maendeleo yao.