Jaruph: Soka la ufukweni yeyote anaitumikia Stars
NJIA inayotumika kuwaita wachezaji wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, ndivyo ilivyo pia katika soka la ufukweni. Mchezaji yeyote ana haki ya kuitumikia nchi, endapo atakuwa na nafasi ya kufanya hivyo.
Katika mahojiano na Mwanaspoti, kocha wa timu ya taifa ya soka la ufukweni, Jaruph Juma anasema wengi wao wanadhani timu hiyo ina wachezaji maalumu wa kucheza, jambo ambalo si sahihi.
Anasema jambo la msingi ni kujua timu hiyo inachukua wachezaji kama ilivyo kwa Taifa Stars.
“Timu ya taifa ya soka la ufukweni, hata akiitwa Mbwana Samatta, kama anakuwa na nafasi ya kucheza, anatakiwa kuja, kwani ni mchezo ambao upo chini ya Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF). Sheria zinazotumika ni zile zile 17 za mpira wa miguu,” anasema kocha huyo na kuongeza:
“Ndiyo maana wamepita wachezaji mbalimbali wa Ligi Kuu kuichezea, mfano Juma Kaseja, Shaban Kado, Deogratius Munishi ‘Dida’, Benjamin Asukile na Samson Mbangula, ingawa kati ya hao, wengine wana majukumu mapya baada ya kustaafu uwanjani.”
Tofauti na mpira wa miguu, soka la ufukweni linachezwa kwa vipindi vitatu, kila kipindi kikiwa na dakika 12. Wachezaji wa ndani ni wanne na kipa anakuwa wa tano kwa kila timu.
“Kuhusu mchezaji akifanya makosa, atapewa kadi za kuonywa za njano na nyekundu kama kawaida. Penalti zinapigwa, lakini tofauti nyingine ni uwanja wa kuchezea, ambao una urefu wa sentimita 37 hadi 38, upana wa sentimita 27 hadi 28 na unatakiwa uwe na mchanga usiopungua sentimita 30 kwenda chini. Magoli kipimo cha upana ni mita 5.5, urefu mita 2.2, anasema kocha huyo na kuongeza:
“Kuhusu nafasi za kucheza, wanaweza kuwepo washambuliaji wawili na mabeki wawili, au wakawa mabeki wote wanaoshambulia na kuzuia. Jumla ya kikosi kinatakiwa kiwe na wachezaji 12, angalau makipa wawe wawili kwa kila timu. Hivyo, watano wakiwa ndani, saba nje. Hesabu zinafanywa muda wowote, hazina kikomo, kama vile unavyokuwa mchezo wa kikapu.
“Jambo lingine, lazima mshindi apatikane. Hakuna matokeo ya sare. Zinapomalizika zile dakika za vipindi vitatu, zinaongezwa dakika tatu. Zikishindikana, zinapigwa penalti na kila kipa anaruhusiwa kudaka moja moja.
“Kunapokuwa na michuano ya kimataifa, unatakiwa kusajili watu ambao wanakuwepo kwenye timu. Hivyo, hata daktari anaweza kucheza, hata mwandishi anaweza kucheza, ilimradi awe anajua na yuko kwenye timu. Pia vipindi vya mapumziko tunapewa dakika tatu kwa vipindi viwili, hivyo mapumziko ni jumla ya dakika sita.”
CHANGAMOTO
Anasema kukosekana kwa wadhamini kumesababisha ligi ya soka la ufukweni kutochezwa katika misimu ya 2024/25 na 2025/26, isipokuwa kunapokuwa na michuano ya kimataifa ama mashindano mbalimbali, wachezaji wanaocheza Ligi Kuu huitwa.
“Misimu mitatu nyuma ilikuwa inachezwa ligi ya ufukweni. Timu 16 zipo, wachezaji wapo, ila shida ni udhamini, jambo linalokuwa gumu kufikia ndoto za kushiriki Kombe la Dunia,” anasema na kuongeza:
“Tunachotamani kingine kifanyiwe kazi ni timu ya taifa angalau iwe inakaa pamoja kwa muda mrefu kambini. Ikishindikana, basi tuwe tunakaa mara kwa mara kambini kwa ajili ya kufanya maandalizi, maana ili kupata nafasi ya kucheza Kombe la Dunia, lazima ushinde mechi sita za kimataifa. Ukiacha hilo, tuwe tunacheza mechi za kirafiki za kimataifa na mashindano mbalimbali ya kimataifa nje ya yale ya Afcon.”
Jambo lingine, anaiomba serikali iwashike mkono wanapokuwa na michuano ya kimataifa.
“Tunaomba, kama walivyofikiwa wenzetu katika Ligi Kuu, basi na sisi tuungwe mkono. Kwanza, soka hili likipata udhamini linatanua ajira kwa vijana, kwani ni mchezo ulio na raha yake,” anasema.
JE, SOKA LA UFUKWENI LINALIPA?
Anasema wakati ligi inachezwa, ilikuwa ngumu, angalau timu ya taifa kunakuwa na posho.
“Kwa levo zangu limenipa. Baada ya kusajiliwa Ligi Kuu ya ufukweni ya Morocco katika timu ya AIN-DIAB, hakuna mshahara, ila kuna posho ninazolipwa kila mechi,” anasema na kuongeza:
“Nalipiwa nyumba, chakula, nikiumwa natibiwa. Ligi hiyo inachezwa miezi minne. Nilisajiliwa 2024, unaongeza mkataba kila mwaka. 2026 natarajia kujiunga na timu Novemba. Pia wanalipa tiketi ya ndege ya kwenda na kurudi.”
NIDHAMU YA JUU
Anasema kile kinachofanywa na wachezaji, akitolea mfano wa mazoezi, nidhamu na kujiepusha na starehe katika soka la ufukweni, kinafanyika mara mbili kutokana na mchezo huo kuchezwa kwa nguvu.
“Bila utimamu wa mwili, ni ngumu kuhimili kucheza, kwani tunacheza mchangani, hivyo misuli inatumia nguvu. Lazima kupumzika sana, kula chakula sahihi ili kujenga mwili na kurejesha nguvu,” anasema kocha huyo, aliyewahi kupitia Yanga B na Simba B, kisha akaenda chuo kikuu alikosomea shahada ya uhandisi wa umeme. Anasema yeye ni mchezaji na kocha, jambo ambalo halizuii chochote katika soka hilo.
“Majukumu yangu ni kutoa maelekezo sahihi ya maandalizi mazoezini. Nikiwa uwanjani, nakuwa nahodha. Nikitoka nje, wakati wa mapumziko, nakuwa kocha. Hivyo, kazi siyo ngumu,’ anasema Jaruph.
Kabla ya kujikita moja kwa moja katika soka la ufukweni, anasema aliwahi kuichezea African Lyon kwa misimu miwili.
“Ndiyo maana nasema soka la ufukweni, ambalo ndani ya uwanja tunacheza bila viatu, mchezaji wa Ligi Kuu anacheza timu ya taifa.”
NJE NA SOKA
Nje ya mchezo wa soka, Jaruph ni fundi anayeweza kujenga nyumba.
“Mbali na kazi niliyosomea, nafanya kazi nyingi za ujenzi wa nyumba kwa ujumla, kama kuweka marumaru, kupaka rangi, ujenzi wa kawaida na kuchora ramani za nyumba. Kuna kazi nilijifunzia nikifanya kazi, kisha nikaenda kusomea,” anasema na kuongeza:
“Mimi ni kijana, nafanya kazi mbalimbali kadri niwezavyo ili kuwa huru kiuchumi. Ndiyo maana nilitoka kwenye kupanga, sasa ninaishi kwangu.”