Prime
Hiki Kikosi cha Kwanza hakuna mchezaji wa Arsenal ametia mguu
Muktasari:
- Lakini, Liverpool ina wachezaji wanne kwenye kikosi hicho, lakini mastaa watatu kati ya hao, wote mikataba yao itafika ukomo mwishoni mwa msimu huu.
LONDON, ENGLAND: NDIYO hivyo. Hakuna mchezaji yeyote wa Arsenal kwenye kikosi cha kwanza cha Ligi Kuu England cha msimu huu, licha ya miamba hiyo kushika namba mbili kwenye msimamo na ina rekodi tamu kabisa kwenye safu ya ulinzi.
Lakini, Liverpool ina wachezaji wanne kwenye kikosi hicho, lakini mastaa watatu kati ya hao, wote mikataba yao itafika ukomo mwishoni mwa msimu huu.
Hii ni kwa mujibu wa takwimu za ubora za WhoScored zilizokusanywa hadi sasa ilipofikia ligi hiyo na ilichagua wachezaji walau walioanzishwa kwenye mechi 20 za Ligi Kuu England. Kikosi chenyewe ni hiki hapa.
KIPA: Mark Flekken (Brentford)
Brentford imekuwa na msimu mzuri kwenye Ligi Kuu England, lakini timu hiyo imekabiliana na mashuti mengi sana ya wapinzani yaliyolenga kwenye goli lao. Ni Southampton pekee ndiyo waliokabiliana na mashuti mengi kuwazidi Brentford, kutokana na hilo kipa Flekken alikuwa na kazi ya ziada na ndiyo maana ana sevu nyingi sana. Kipa mwingine aliyefanya vizuri msimu huu ni Matz Sels, lakini kwenye takwimu za WhoScored, aliyechomoza ni Flekken wa Brentford.
BEKI WA KULIA: Trent Alexander-Arnold (Liverpool)
Achana na mabao yake mawili aliyofunga na asisti sita zinazomfanya kuhusika kwenye mabao sita katika kikosi cha Liverpool msimu huu, beki wa kulia Trent amekuwa na kiwango bora sana kwenye ligi, hasa linapokuja suala la kukokota mpira na kuvuka wapinzani kwenye eneo hilo. Beki huyo Mwingereza amepiga mashuti matano pia msimu huu na hakika atakuwa mchezaji atakayekumbukwa kwenye Ligi Kuu England atakapojiunga na Real Madrid.
BEKI WA KATI: Virgil van Dijk (Liverpool)
Beki wa kati bora wa msimu? Mdachi huyo amefaulu vipimo vya kuangaliwa ubora wake kwa macho tu, lakini takwimu pia zinambeba na kumfanya awe kwenye orodha ya mabeki mahiri kabisa kwenye Ligi Kuu England msimu huu. Liverpool ipo kwenye nafasi nzuri ya kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu na kwenye hilo, Van Dijk ameripotiwa ni mchezaji muhimu zaidi kwa miamba hiyo ya Anfield pengine kuliko mabao ya Mohamed Salah.
BEKI WA KATI: James Tarkowski (Everton)
Everton imeruhusu mabao machache kuliko Manchester City msimu huu na sababu kubwa ya jambo hilo ni uwepo wa beki wa kati, James Tarkowski, ambaye amenasa mipira uvuguni kwenye miguu ya wachezaji wa timu pinzani mara nyingi kuliko mabeki wengine wote wa kati kwenye ligi, pia anaongoza kwa kuzuia mashuti, kuokoa na kunasa mipira njiani. Ni mtu ambaye amekuwa bize sana uwanjani na hilo ndilo linaloifanya Everton kuwa mahali salama kwenye ligi.
BEKI WA KUSHOTO: Antonee Robinson (Fulham)
Asisti 10 kwenye Ligi Kuu England ni kitu kilichowafanya wengi waanze kumtolea macho, lakini amekuwa akiongoza pia kwa kunyang'anya mipira kwenye miguu ya wapinzani kwa kulala yombo, akilifanya hilo kwa ubora mkubwa kuliko beki mwingine yoyote wa kushoto msimu huu. Ni suala la muda tu kabla ya kupata dili la kujiunga na klabu kubwa ya Ulaya, lakini kwenye hilo la klabu kubwa bila shaka haiwezi kuwa Liverpool na upande wa kushoto haina shida.
KIUNGO WA KATI: Bruno Fernandes (Man United)
Amekuwa akitumika kwenye kiungo ya kati kwa siku za karibuni na kocha Ruben Amorim baada ya kuja na mtindo wake wa 3-4-3, ambao umeondoa kabisa majukumu ya Namba 10. Kiungo, Bruno Fernandes amefunga mabao manane na kuasisti tisa kwenye Ligi Kuu England msimu huu na hakika jambo hilo limeifanya Manchester United kuhitaji huduma yake zaidi ili kutokuwa kwenye hali mbaya zaidi ya inayowakabili kwa sasa. Man United ni Fernandes FC.
KIUNGO WA KATI: Ryan Gravenberch (Liverpool)
Amekuwa mchezaji muhimu sana katika mchakamchaka wa Liverpool kwenye kufukuzia ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu, akicheza kwenye kiungo sambamba na Alexis Mac Allister. Kwenye kikosi hiki, Ryan amewapiku Youri Tielemans na Declan Rice, ambao pia wamekuwa na takwimu nzuri kwa mujibu wa WhoScored. Lakini, nafasi iliyopo Liverpool na kile Ryan, ambacho amekuwa akikifanya ndani ya uwanja msimu huu kimempa namba kwenye kikosi hiki.
WINGA WA KULIA: Mo Salah (Liverpool)
Je, Mohamed Salah ni winga bora kabisa kwenye Ligi Kuu England msimu huu? Takwimu zake linaweka hilo bayana kabisa. Na msimu huu amefunga mabao 27 na kuasisti 17 na bila ya shaka atakuwa kwenye orodha ya wachezaji watakaofukuzia tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu England, huku akiwamo pia kwenye vita ya kusaka Kiatu cha Dhahabu na mchezeshaji bora wa mwaka. Kwenye kikosi hiki, Mo Salah atashambulia kutoka kulia kama kawaida.
KIUNGO MSHAMBULIAJI: Cole Palmer (Chelsea)
Hajafunga wala kuasisti tangu kati ya Januari, lakini Cole Palmer bado amehusika kwenye mabao 20 msimu huu. Amepata nafasi kwenye kikosi hiki cha WhoScored, kwa sababu amekuwa akipiga sana mashuti na kutengeneza nafasi nyingi za mashambulizi kwa timu yake ya Chelsea licha ya kwamba amekuwa hafungi au kuasisti. Kilichokosekana kwa Palmer ni mabao na asisti na ndiyo maana kocha Enzo Maresca anapambana arudi kwenye ubora wake uwanjani.
WINGA WA KUSHOTO: Matheus Cunha (Wolves)
Fowadi huyo anayehusishwa na Arsenal, Mbrazili Cunha na yule wa Bournemouth, Antoine Semenyo wamekuwa kwenye viwango bora sana kwa timu zao msimu huu na wote wamekuwa na takwimu sawa huko kwenye WhoScored. Lakini, mchango wa mabao 17 aliyotoa kwa timu yake ya Wolves, ambayo haipo pazuri kwenye msimamo wa ligi, hilo halimharibii Cunha na kumfanya kuwa mmoja wa wachezaji bora msimu huu na ndiyo maana Arsenal na Liverpool zinamtaka.
STRAIKA: Alexander Isak (Newcastle United)
Newcastle United haiwezi kuthubutu kumuuza straika wake ambaye ana mabao 20 kwenye ligi. Kiwango chake bora kabisa kwenye ligi hiyo, kimemfanya Alexander Isak kuwa kwenye rada za klabu nyingi zinazohitaji saini yake, ikiwamo Arsenal, ambayo itakwenda kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi ikiwa na kazi moja tu ya kusaka straika wa mabao ili kwenda kuwapa nguvu ya kushindania na kubeba ubingwa msimu ujao.