Hawa hapa wajumbe wanaoitaka Yanga
Muktasari:
- Baada ya kuwangalia Yanga Makaga na Rodgers Gumbo kwenye toleo lililopita leo tunahamia kwa Alexander Ngai na Injinia Mustapha Himba ambao nao wanawania kati ya nafasi tano za wajumbe wanaotakiwa kutokana na kupigiwa kura.
TUNAENDELEA kuwaangalia wagombea wa uchaguzi mkuu wa Yanga tukisalia palepale kwenye kundi la waaoutaka ujumbe wa kamati ya utendaji wa klabu hiyo ambao wameshapita kwenye mchujo wa mwisho kuwania nafasi hizo.
Baada ya kuwangalia Yanga Makaga na Rodgers Gumbo kwenye toleo lililopita leo tunahamia kwa Alexander Ngai na Injinia Mustapha Himba ambao nao wanawania kati ya nafasi tano za wajumbe wanaotakiwa kutokana na kupigiwa kura.
Tuanze na Ngai ambaye jamaa baada ya kuwa madarakani kwa miaka minne ya kwanza, kwenye muhula wa rais injinia Hersi Said anataka kurudi tena kwa njia ileile kupitia kura za wanachama kutetea nafasi yake.
Ngai ambaye ni mfanyabiashara kijana, kwenye uchaguzi wa mwaka 2022 alikuwa mmoja wa wagombea waliojizolea kura nyingi akikubalika na makundi ya wanachama na mashabiki wa klabu hiyo akishinda kirahisi.
Kabla ya kuingia kwenye uongozi safari ya Ngai ilianzia kuwa kama mwanachama wa kawaida aliyekuwa anasafiri maeneo mengi ambayo timu hiyo inakwenda kabla ya baaadhi ya mashabiki na wanachama wenzake kumkalia kooni na kumwambia agombee kisha kupata.
Eneo ambalo Ngai lilimpa heshima kubwa mbele ya wanachama na mashabiki wa timu hiyo ni kwenye lile sakata la mechi dhidi ya Simba, akiwa mmoja wa viongozi aliyesimama imara kusimama na watu wa klabu hiyo mpaka timu hiyo ikashinda vita ya mechi hiyo kubwa.
Ukiondoa Hersi na makamu wake Arafat Haji, Ngai ni mmoja wa viongozi vijana ambao wana ushawishi mkubwa kwa makundi makubwa ya vijana kutokana na kuwa nao karibu katika kuwasikiliza na kupeana akili ya maisha hatua ambayo imempa uhakika mkubwa wa kukubalika.
Sio vijana peke yake, Ngai amekuwa akiwa karibu hata na wazee wa klabu hiyo wamekuwa sehemu ya maisha yake katika kuipigania klabu hiyo.
Akizungumza katika kurudi kwake,Ngai amesema: "Baada ya kuwa sehemu ya uongozi kwenye muhula wa kwanza, sasa nimeona kwamba bado tuna nafasi ya kuisaidia klabu yetu kuwa na mafanikio zaidi, tumeshinda mataji mengi ya ndani lakini sasa ni wakati wa kushirikiana na maono ya uongozi wa juu kwenda kuweka alama kubwa zaidi Afrika,”amesema Ngai.
KUHUSU HIMBA
Mgombea mwingine ambaye anautaka ujumbe ni injinia Mustapha Himba, akirudi tena kutafuta kura za kutosha kumwezesha kuwa mjumbe wa kamati ya utendaji.
Himba alikuwa mmoja wa wagombea walioutaka ujumbe kwenye uchaguzi wa mwaka 2022 lakini bahati mbaya kwake kura hazikutosha akikwamia hapo.
Hata hivyo, hakukosa vyote akakutana na uteuzi wa kuwa mjumbe wa kamati ya mashindano ya timu hiyo msimu uliopita ambayo mwenyekiti wake alikuwa Gumbo.
Himba alikuwa mjumbe muhimu muhimu kwenye kamati ya mashindano ya Yanga akionekana kuwa mbele kwenye mechi nyingi za timu hiyo.
Himba hakuwa Yanga pekee lakini pia taifa linamtambua baada ya kuwa kwenye sekretarieti ya maandalizi ya Fainali za Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani CHAN zilizofanyoka nchini mwaka jana,Tanzania ikiwa mwenyeji pamoja na Kenya na Uganda.
Kitaaluma Himba ni injinia wa miradi mikubwa ya ujenzi na miundombinu, akibobea kwenye usimamizi wa muda, gharama,ubora na rasilimali.
Kwenye uchaguzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) uliopita ambao Rais Wallace Karia alishinda, Himba alikuwa mmoja wa wagombea nafasi hiyo ya juu, akikwamia kwenye kukosa uthibitisho wa wanachama wa mkutano mkuu.
Himba anarudi tena kujiuliza mbele ya wanachama wa Yanga akitafuta kuingia kwa mara ya kwanza kwenye kamati ya utendaji kutoa mchango wake katika kuipasha Zaidi timu hiyo badaa ya kuwa sehemu ya mafanikio ya mataji ya misimu mine iliyopita.
Himba akizungumzia dira yake amesema:”Wanachama wenzangu wananifahamu, mimi sio mtu wa maneno zaidi ya vitendo, kuna kazi kubwa imefanywa na viongizi wanaomaliza kipindi hiki, mengi yamefanya mazuri lakini siwezi kuwa na sera zangu lakini nitashirikiana na viongozi wa juu ambao naona wote wawili watarudi ili tuzidi kuipa mafanikio zaidi klabu yetu,tuna rais na makamu wake ambao wana nishati kubwa ya kuzidi kuweka alama ya kiungozi” amesema Himba.