Maana ya nyota 10 jezi za Nigeria
Muktasari:
- Tofauti na nyota nyingi zinazowekwa kwenye jezi za timu za taifa ambazo mara nyingi huwakilisha mafanikio ya Kombe la Dunia, kwa Nigeria zina maana tofauti.
HUENDA umeitazama iimu ya taifa ya Nigeria, Super Falcon na kuvutiwa na nyota 10 zilizopambwa kwenye jezi yao. Unajua ina maana gani?
Tofauti na nyota nyingi zinazowekwa kwenye jezi za timu za taifa ambazo mara nyingi huwakilisha mafanikio ya Kombe la Dunia, kwa Nigeria zina maana tofauti.
Kila nyota moja inawakilisha ubingwa mmoja wa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) ambao Nigeria imeutwaa, ikiwa nayo 10 kati ya matoleo 13, tangu mashindano hayo yaanze kutumia mfumo wa fainali wenye hatua ya makundi mwaka 1998.
Mataifa yaliyovunja utawala wao ni Equatorial Guinea mwaka 2008 na 2012 na Afrika Kusini mwaka 2022.
Ni jezi zinazoelezea hadithi ya kizazi kilichopambana kuandika historia kuanzia nyota kama Mercy Akide, Perpetua Nkwocha, Asisat Oshoala, Esther Okoronkwo na mastaa wengine walioandika historia kwenye taifa hilo.
Jezi hizo zilianza kutumika kwenye mechi wa kirafiki dhidi ya Tanzania wa kujipima nguvu kabla ya WAFCON 2026 na Super Falcons ilishinda kwa mabao 2-1.
Hizi hapa katika mashindano hayo tangu mwaka 1998.
1 - GHANA 1998
Mashindano ambayo yalikuwa ya kwanza kucheza kwa mfumo kamili wa makundi na hatua za mtoano.
Chini ya Kocha Ismaila Mabo, Nigeria ilianza kwa nguvu kubwa baada ya kuifunga Morocco mabao 8-0, kisha Misri 6-0 na DR Congo 4-0 hatua ya makundi.
Ilionekana mapema kuwa moja ya timu itakayoandika historia kwenye fainali hizo baada ya kufunga mabao 18 na kutoruhusu bao hata moja hatua ya makundi.
Katika nusu fainali waliifunga Cameroon 6-0 kabla ya kukutana na wenyeji Ghana kwenye fainali mjini Accra na kushinda 2-0 mabao ya Mercy Akide na Patience Avre.
2. AFRIKA KUSINI 2000
Kama kawaida ilianza kampeni za makundi ikimaliza kileleni baada ya kuzichapa wenyeji Afrika Kusini, Zimbabwe na Reunion ikatinga nusu fainali ilipoiondoa Cameroon.
Katika fainali dhidi ya wenyeji Afrika Kusini, ilishinda mabao 2-0 na kutwaa ubingwa wa pili mfululizo.
3. NIGERIA 2002
Super Falcons iliendelea kuthibitisha ubabe wake baada ya kushinda mechi zote za hatua ya makundi kabla ya kuingia hatua ya mtoano.
Baada ya kuifunga Cameroon nusu fainali, ilikutana na Ghana fainali na kushinda 2-0, likiwa taji la tatu mfululizo.
4. AFRIKA KUSINI 2004
Nigeria iliendelea kutawala tena mwaka 2004 baada ya kufanya vizuri katika hatua ya makundi na kufika tena fainali.
Katika fainali hiyo, ilikutana na Cameroon na kuonyesha ubora mkubwa kwa kushinda mabao 5-0, ikitwaa la nne mfululizo, huku Perpetua Nkwocha akimaliza mfungaji bora.
5. NIGERIA 2006
Ikiwa nyumbani tena mwaka 2006, Nigeria iliendelea na rekodi yake ya kutisha na fainali ilikutana tena na Ghana.
Bao moja lilitosha kuipa Nigeria ushindi wa 1-0 na kutwaa ubingwa wa tano mfululizo. Katika kipindi hicho, Super Falcons ilikuwa haijapoteza ubingwa wowote tangu kuanzishwa kwa mfumo wa fainali za WAFCON mwaka 1998.
6. AFRIKA KUSINI 2010
Mwaka 2008 Nigeria ilishindwa kufurukuta mbele ya wenyeji Equatorial Guinea ambao walivunja utawala wao kwa kubeba taji hilo baada ya kuichapa Afrika Kusini kwa mabao 2-1.
Katika fainali hizo Nigeria iliondolewa nusu fainali na Equatorial Guinea kwa bao 1-0, hata kwenye makundi ilimaliza nafasi ya pili.
Nigeria ilirejea kwa nguvu mwaka 2010 na kufika fainali na kukutana na Equatorial Guinea na iliichapa mabao 4-2 na kurejesha taji, ikithibitisha ubabe wake.
7. NAMIBIA 2014
Mwaka 2012, haikufanya vizuri na iliishia nusu fainali kwa kuondolewa na Afrika Kusini kwa bao 1-0, lililofungwa na nahodha Janine van Wyk, dakika ya 23.
Huo ulikuwa ushindi wa kwanza wa Banyana Banyana dhidi ya Nigeria katika historia ya michuano hiyo.
Baada ya kuikosa fainali nyingine tena Nigeria ilirejea na matumaini makubwa mwaka 2014 na iliifunga Afrika Kusini katika nusu fainali kabla ya kukutana na Cameroon kwenye fainali na ilishinda 2-0, huku Asisat Oshoala akiibuka kuwa mmoja wa mastaa wakubwa baada ya kutwaa tuzo ya mfungaji bora na mchezaji bora wa mashindano.
8. CAMEROON 2016
Nigeria ikakutana na Cameroon kwenye fainali na kuitandika bao 1-0 na kutwaa taji lingine la WAFCON.
Ushindi huo uliinyima fursa Cameroon ya kusherehekea ubingwa mbele ya mashabiki wao.
9. GHANA 2018
Baada ya sare ya 0-0 dhidi ya Afrika Kusini katika fainali, bingwa aliamuliwa kwa mikwaju ya penalti.
Nigeria ilishinda penalti 4-3, huku kipa Tochukwu Oluehi akiwa shujaa kwa kuokoa penati mbili.
10. MOROCCO 2024 (ILICHEZWA 2025)
Nigeria iliingia mashindano hayo ikiwa na dhamira ya kurejesha taji baada ya Afrika Kusini kushinda mwaka 2022.
Katika fainali dhidi ya wenyeji Morocco mjini Rabat, Nigeria ilikuwa nyuma kwa mabao 2-0 kipindi cha kwanza.
Lakini kipindi cha pili kilikuwa cha tofauti kabisa baada ya kufanya mabadiliko ya wachezaji wawili, ikimwingiza Esther Okoronkwo aliyekuja kuwarejesha mchezoni baada ya kufunga penati.
Baadae Folashade Ijamilusi akasawazisha, kabla ya Jennifer Echegini kufunga bao la ushindi na kuipa Nigeria ushindi wa 3-2.
Nigeria ndiyo timu ya kwanza ya wanawake Afrika kufikisha mataji 10.
Hivyo nyota hizo sio mapambo kwenye jezi kama baadhi wanavyofikiria, bali ni kumbukumbu ya vizazi vya wachezaji waliopigania heshima ya Nigeria.
Zinawakilisha majina makubwa kama Mercy Akide, Perpetua Nkwocha, Asisat Oshoala, Desire Oparanozie, Onome Ebi na Rasheedat Ajibade ambao wamejenga historia hiyo.