Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hanifa: Soka lilinipa kitanda, ndoa

Muktasari:

  • Hanifa ambaye aliwahi kuzichezea timu mbalimbali za Ligi Kuu ya wanawake kama Tanzanite Queens, Amani Queens, Evar Green, Sayari, Panama, Uzuri Queens anasema alama aliyoiambulia kwenye soka, tofauti na vitu anavyomiliki kwa kununua na pesa nje na mpira wa miguu.

KIPA wa zamani wa timu ya taifa ya wanawake ‘Twiga Stars’ Hanifa Iddy, katika mahojiano yake na Mwanaspoti anaelezea utofauti wa soka la sasa linavyolipa, akitofautisha na kipindi chao ambacho walicheza kwa kiwango cha juu, ila hawakunufaika.

Hanifa ambaye aliwahi kuzichezea timu mbalimbali za Ligi Kuu ya wanawake kama Tanzanite Queens, Amani Queens, Evar Green, Sayari, Panama, Uzuri Queens anasema alama aliyoiambulia kwenye soka, tofauti na vitu anavyomiliki kwa kununua na pesa nje na mpira wa miguu.

“Kila safari ya mtu inasimuliwa zake za kufurahisha na kuumiza ndiyo ubinadamu, pamoja na kuambulia vitu kiduchu katika soka, lakini nimepata familia,” anasema.


 KUTENDWA NA NDOA

Kabla ya kuoana mwaka 2016 na mume wake anayemtaja kwa jina la Mustafa Mabruck anasema alisoma naye Shule ya Sekondari ya Makongo na alimsaidia kumjenga kuwa golikipa bora.

“Baada ya kuhitimu kidato cha nne kila mtu aliendelea na maisha yake ya kazi na mahusiano na wala hatukuwahi kuwasiliana, mwaka 2016 kipindi hicho alikuwa anaichezea Ndanda FC ya Mtwara, mzunguko wa kwanza timu hiyo ilikuja kucheza na Simba Uwanja wa Benjamin Mkapa, nilienda kuangalia mechi hiyo, baada ya kumalizika kwa mechi tukaonana na kubadilishana namba,” anasema Hanifa.

“Kipindi hicho nilitoka kupigwa matukio na baba mtoto wangu wa kwanza, basi nikawa najikuta nawasiliana naye mara kwa mara, tukaanza kusimulia maumivu yetu.

“Alipanga tuonane ana kwa ana, ikawa hivyo naye alikuwa ametoka kuachwa na mama mtoto wake, katika kupeana pole tukajikuta tunajenga hisia za upendo, tukaanza mahusiano katikati ya mwaka 2016 tukaona na sasa tuna miaka 10 kwenye ndoa yetu na tumejaaliwa kupata mtoto mmoja.”

Anasema mume wake kwa sasa ni kocha wa makipa wa timu ya Mashujaa Queens, wana mpango wa kuanzisha kituo cha watoto chini ya umri wa miaka 10 na wameanza mchakato wa kutafuta wadhamini.

“Kusema ukweli ukimpata mwenza sahihi maisha ya ndoa ni mazuri na kazi inakuwa rahisi, mimi na mume wangu tumesoma kozi ya ukocha pamoja kuanzia ngazi ya awali hadi Diploma D ya CAF na yeye ndiye aliyelipa ada na alikuwa ananielekeza kwa ziada zaidi baada ya mafunzo ya wakufunzi.”

Anasema kwa sasa anaendelea kusomea udaktari wa michezo chini ya Chama cha Madaktari wa Tiba kwa Wanamichezo Tanzania (TASMA)

“Hata katika kozi hiyo mume wangu ndiye aliyelipa na ukumbuke tunataka kuanzisha kituo, hivyo lazima tuwe na uelewa wa vitu vingi na bado tuna mpango wa kuendelea zaidi kusomea kozi ya ukocha,” anasema.


UOGA WANAWAKE

Anasema wanasoka wengi wa kike wana uoga wa kuanzisha familia kwa kuhofia ajira, lakini anasisitiza wanapaswa kuandaa maisha ya baadaye baada ya uwanjani.

“Siwezi kuficha baada ya kuzaa mtoto wangu wa kwanza nilikaa nje kwa muda mrefu, maana nilihakikisha naacha salama mazingira ya mwanangu, hata mwanangu wa pili nilikaa miaka minne bila kucheza, hilo wengi wao linawatisha kuona watapoteza kazi zao, lakini kama wanawake lazima wajue thamani yao na umuhimu wa kuwa na familia, hilo ni jambo halizuiliki ikiwezekana viongozi na makocha wawe wanawaelimisha wachezaji, kama wanasoka wa kiume wanavyokuwa na familia zao, iwe hivyo kwa mwanamke,” anasema.

“Watu ambao nimecheza nao hata uvaaji wangu ulikuwa tofauti, nilivaa asili ya mwanamke, soka kwangu ni kazi haiwezi kubadilisha uhalisia wangu, ndiyo maana wengi wao wanaojichukulia maisha yao kama ya wanaume inakuwa ngumu kwao kufanya maamuzi ya kuzaa.”

Anasema mwanamke anayejitambua haiwezi kuwa ngumu kwake kuitunza familia na kufanya kazi.

“Kila kitu kinahitaji utayari na Mungu ametupa kitu cha kipekee wanawake, ndiyo maana unaweza ukawa na familia na ukafanya kazi na kila kitu kikaenda, ila kubwa zaidi nimepata mwanaume mwenye sapoti kubwa ambayo inatupa nguvu ya kufanya vitu vya maendeleo kwa pamoja.”


SOKA LIMEMPA NINI

Licha ya kipaji alichokuwa nacho anaelezea kumbukumbu pekee aliyonayo kucheza ligi Bara ni kununua kitanda kwa pesa za usajili kuichezea Panama ya Iringa. “Nilisajiliwa kwa Shilingi 300,000 nikanunua kitanda, ambacho nikikiangalia nakumbuka jasho la uwanjani, ilikuwa mwaka 2019 kipindi hicho ilikuwa Daraja la Kwanza nikapanda nayo hadi 2020 iliposhuka, ilipofika 2021 nilipata mimba ya mtoto wangu wa pili nikatulia nyumbani kwa miaka minne, kisha nikarejea kazini,” anasema Hanifa.

“Soka la kipindi hicho lilikuwa halilipi kama ambavyo ipo kwa wadogo zetu wa sasa hivi, mfano tukiwa kambini timu ya taifa (Twiga Stars) tulikuwa tunapewa Sh.10000 kwa siku, tofauti na sasa.” 

Ukiachana na Tanzanite Queens, anasema angalau alivyokuwa amekwenda kucheza Kenya katika timu ya Kiminini Girls alipewa pesa ndefu ya usajili kwa kipindi hicho ilikuwa Sh3,000.  “Siwezi kukumbuka sawasawa ilikuwa sawa na Shilingi ngapi ya Tanzania.”


ALIITWAJE KASEJA?

Anasema wakati anaichezea timu ya Tanzanite Queens, ambayo ilikuwa inaweka kambi yake Kawe, katika uwanja ambao walikuwa wanafanyia mazoezi na wakati mwingine kuchezea mechi za kirafiki alikuwa anakutana na kipa wa zamani Simba, Yanga na Taifa Stars, Juma Kaseja.

“Wengi wanajiuliza kwa nini A.K.A yangu ilikuwa Kaseja ilitokana na kipaji nilichokuwa nacho wengi wakawa wananiita hivyo, Kaseja ni mtu ambaye napiga naye stori kila mara kitu kikubwa nilichojifunza kutoka kwake ni upambanaji bila kukata tamaa,” anasema.