KUNA wachezaji wanaofika Ligi Kuu kwa sababu ya kipaji, wengine kwa juhudi zao lakini kwa winga wa Azam FC, Zidane Sereri safari ya kufika alipo leo ina sura ya mtu aliyeshikwa mkono wakati ambao ndoto yake ilikuwa bado haijawa na uhakika.
Zidane, aliyezaliwa Novemba 19, 2005, anakumbuka jinsi maisha yake yalivyobadilika baada ya Mohamed Aden ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Soka Dodoma na mjumbe wa Kamati ya TFF, kumtafuta akiwa nyumbani na kuamua kumsaidia katika safari yake ya soka.
Kilichofuata hakikuwa tu kwenda kufanya majaribio Dodoma, bali kukaa nyumbani kwa Aden kwa takribani miaka miwili na nusu, akilelewa kama mtoto wa familia na kupewa mazingira yaliyomruhusu kuutazama mpira kama kazi yake badala ya kuhangaika na mahitaji ya msingi ya maisha.
Akizungumza na Mwanaspoti, Zidane anasema hadi leo bado anakumbuka siku ambayo simu ya Aden ilibadilisha mwelekeo wa maisha yake.
“Nilikuwa nyumbani, nikapigiwa simu kwamba nahitajika katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya. Nilipoenda nikakutana na Mwenyekiti wa Chama cha Soka cha Wilaya, Msekela ndipo nikazungumza na Mohamed Aden,” anasema Zidane.
Anasema Aden alimweleza kuwa alikuwa amemsikia na kumfuatilia, licha ya kwamba wao wawili hawakuwa wamewahi kufahamiana.
“Aliniambia, ‘kijana nimekusikia na nimekufuatilia. Najua hunijui na hatufahamiani, lakini nataka kukusaidia kwenye misingi ya mpira. Nimeshawahi kusaidia watu wengi na naamini na wewe utafika mbali.’ Akanipa namba yangu na kuniambia muda wowote angenitafuta,” anasema.
Baada ya hapo, Zidane anasema alikaa takribani wiki mbili bila kusikia chochote, kabla ya simu nyingine kutoka kwa Aden, safari hii ikiwa na maagizo ya kuanza safari ya Dodoma.
“Alinipigia simu usiku na kuniambia, ‘Kesho naomba upande gari uje.’ Sikujua ni timu gani. Mara ya kwanza aliniambia huenda nikaja JKT Tanzania au Dodoma Jiji kwa sababu kipindi hicho timu zote zilikuwa Dodoma,” anasema.
Kesho yake Zidane hakutaka kupoteza muda. Aliamka mapema na kuanza safari ya Dodoma, ambako alifanya majaribio na hatimaye kusajiliwa katika kikosi cha vijana cha Dodoma Jiji
“Nilifika Dodoma asubuhi mapema, nikafanya majaribio na Alhamdulillah, yalikwenda vizuri. Walinipokea vizuri na nikasajiliwa Dodoma Jiji Under-20,” anasema.
Lakini hapo ndipo ukurasa mwingine muhimu wa maisha yake ulipoanza. Aden hakumwacha Zidane ajitegemee baada ya kumfikisha Dodoma, badala yake alimchukua na kumpeleka nyumbani kwake.
Zidane anasema alikaa katika familia hiyo kwa takribani miaka miwili na nusu, akipata chakula, malazi na usafiri wa kwenda mazoezini bila kulazimika kuanza kuhangaika na mambo ambayo yang eweza kuondoa akili yake kwenye mpira.
Nilikaa kwake kama miaka miwili na nusu. Kila kitu, kuanzia chakula hadi usafiri wa kwenda mazoezini, alikuwa anahakikisha kinapatikana. Namshukuru Mungu alikuwa na moyo wa kipekee,” anasema.
“Yeye, mke wake na watoto wake wote walinipokea kama mwana wao. Kwangu ilikuwa kitu kikubwa sana kwa sababu nilipata muda mwingi wa kufanya mazoezi na nilikuwa huru kichwani,” anaongeza.
Kwa Zidane, msaada huo haukuwa wa kawaida. Anasema mchezaji anayepambana kufika mb ali anahitaji kwanza kuwa na utulivu wa akili, chakula na sehemu salama ya kulala kabla ya kufikiria mambo mengine.
“Sikuwa na stresi ya kuanza kufikiria nitakula nini au nitapata wapi nauli ya kwenda mazoezini. Kwa mchezaji, vitu vya msingi ni kula na kulala vizuri, halafu akili yako iwe kwenye mpira,” anasema.
Ndiyo maana Zidane anasema alijiona akiwa na deni la kulipa si kwa fedha, bali kwa mafanikio.
“Malipo yangu kwake yalikuwa ni kufanya vizuri na kutimiza malengo yangu. Ningefeli, ningemwangusha kwa kiasi kikubwa. Pia ningemvunja moyo na huenda akapoteza moyo wa kusaidia vijana wengine,” anasema. Sasa anapoangalia alipo, Zidane anaamini mafanikio yake ni sehemu ya ushahidi kwamba Aden hakukosea zaidi ya hapo, amebeba somo ambalo anataka kulirudisha kwa kizazi kingine.
“Mpaka leo najivunia sana. Anaweza kusema. Kumbe nilimshika Zidane mkono na akafika sehemu fulani. Na mimi sasa napata nguvu ya kuwashika mkono vijana wengine wafike sehemu,” anasema.
Lakini kabla kijana hajafika Azam FC au Ligi Kuu, Zidane anasema kuna mambo matatu ya msingi ambayo ni nidhamu, jitihada na uvumilivu.
“Cha kwanza ni nidhamu. Unaweza kuwa na kipaji kikubwa, ukawa unapiga mpira vizuri, lakini ukikosa nidhamu unaweza kujifelisha mwenyewe,” anasema.
“Cha pili ni jitihada. Kipaji pekee hakitoshi. Mpira wa sasa unabadilika na jitihada imekuwa muhimu sana. Kuna wakati kipaji kinaweza kwenda nyuma, lakini jitihada ndiyo inaenda mbele,” anaongeza.
Na kwa jambo la tatu, Zidane anasema vijana wengi hukosea kwa kutaka matok eo ya haraka bila kupitia safari ya ma umivu.
Ha iwezekani ucheze Ligi Kuu leo halafu ndani ya mwaka mmoja uta ke uwe um efika kila kitu. Lazima uwe na uvumilivu mkubwa,” anaongeza.
Zidane mwenye kasi na anayependa kushambulia akitokea pembeni kuelekea kwenye boksi, anasema aina yake ya uchezaji haikujengwa kwa kulazimishwa na mtu, bali imetokana na kiu yake ya kujisukuma mwenyewe.
“Staili yangu naanza nayo mwenyewe. Ni kitu ambacho kiko ndani yangu. Mimi ni mchezaji mwenye kasi, napenda kushambulia na kuingia kwenye maeneo ya hatari kutafuta boksi,” anasema.
Anasema hata mazoezini hapendi kusubiri kocha amsukume ndipo afanye kazi, kwa sababu amejifunza kwamba kwanza mchezaji mwenyewe lazima awe na njaa ya mafanikio.