Genilson Santos ‘Jaja’ + Andrey Coutinho = Okwi
Muktasari:
Itabidi wasubiri sana hadi hapo mchezaji mwenye umri zaidi ya miaka ishirini na tisa, Genilson Santos ‘Jaja’ raia wa Brazil, nchi iliyojaza vipaji vya wanasoka azoee mazingira ya Tanzania, aanze kufunga mabao muhimu.
HAKUNA shaka kwamba mashabiki wa Yanga msimu huu itawabidi wasubiri sana kama wanataka kupata mafanikio, itabidi wasubiri zaidi kwani malengo na mipango ya kocha, Marcio Maximo, si kuipa timu ubingwa msimu huu.
Tena hata huko kwenye Kombe la Shirikisho hana mpango nako sana zaidi ya kushiriki kama kawaida yake.
Itabidi wasubiri sana hadi hapo mchezaji mwenye umri zaidi ya miaka ishirini na tisa, Genilson Santos ‘Jaja’ raia wa Brazil, nchi iliyojaza vipaji vya wanasoka azoee mazingira ya Tanzania, aanze kufunga mabao muhimu.
Kwa hesabu za haraka haraka, ni baada ya michezo kama 20 hivi ndipo labda Jaja anaweza kuwa amezoeleka na wachezaji wa timu pinzani sasa watakuwa wameshaanza kumdharau kwamba si lolote, hapo ndipo tutakapoyaona mabao yake.
Nasema itabidi wasubiri sana kwani kwa sasa Jaja ni mzito, hivyo hana budi kuendelea kupunguza uzito ili aendane na kasi ya kina Mrisho Ngassa na Simon Msuva, lakini ataendelea kucheza tu hata kama mashabiki wanalalamika.
Itawabidi Yanga waendelee kusubiri kwamba huo ulaini laini wake utakwisha na ataanza kutembea na mipira kwa kasi huku akimpunguza mchezaji mpinzani mmoja mmoja na kufunga.
Itabidi wasubiri sana hadi pale kocha Marcio Maximo atakapobadili mfumo wake wa kumtegemea mshambuliaji mmoja badala ya kuwa na washambuliaji wawili au watatu, mbinu zake za wachezaji kupiga pasi nyingi tu katikati ya uwanja huku viungo wakiwa hawakabi, watasubiri sana hadi pale Maximo atakapoondoa fikra potofu ya kuwapanga kila mchezo Wabrazili Jaja na Andrey Coutinho wakati uwezo wao ni wa kawaida sana.
Haihitaji kutumia msimu mzima kubaini kama Wabrazili hao wataifaa Yanga ama la.
Nakumbuka mwandishi mwenzangu, Egbert Mkoko, miezi michache iliyopita aliandika ‘Yanga na ulimbukeni wa Wabrazili’.
Ndani ya makala hayo alishangaa ni vipi Wabrazili waje kucheza ligi Bongo na akawa akielezea ujio wa kocha Maximo kwamba haukuwa na tija kwa soka letu, alisema anawapa mwaka mmoja watu wa Yanga na baada ya hapo lazima Wabrazili watafukuzwa.
Ikiwa hata huo mwaka haujafika, amekuja Frank Sanga na amejitoa kabisa kumkubali Jaja. Kote huko tunafika mbali, hawa wachezaji si wa viwango vya kuchezea Yanga, huwezi kumleta mchezaji kutoka Ulaya, Asia au Amerika Kusini kuja nchini akiwa na viwango vya akina Jaja, hiyo ni sawa na kulitukana soka la Tanzania. Ni dhihaka dhidi ya Ligi Kuu yetu, si sahihi.
Hivi kulikuwa na ulazima gani kwa Maximo kumwekea vioo vyeusi Emmanuel Okwi kwa viwango vya akina Jaja?
Kulikuwa na sababu gani ya Yanga kuwanunua Jaja na Coutinho kwa Dola 35,000 na sasa ikiwalipa Dola 5,100 kila mwezi wakati Okwi alitakiwa kumaliziwa Dola 50,000 na mshahara wake ukiwa pungufu ya jumla ya akina Coutinho.
Jumamosi iliyopita katika mechi ya Simba na Yanga, nilitumia zaidi ya dakika tisa na nusu baada ya kipindi cha kwanza kuanza kubaini kiungo mshambuliaji, Coutinho hakuwa anautendea mpira haki. Hakutoa pasi nzuri au kunyang’anya. Lakini ndani ya dakika tano tu, tayari Okwi alishajaribu, alishatengeneza nafasi kadhaa za wenzake kupita.
Okwi si wa kiwango kizuri sana ukilinganisha na alivyokuwa zamani, lakini bado kila alipoupata mpira ilikuwa hatari langoni kwa Yanga.
Kwa hakika uwepo wa Jaja na Coutinho ulikuwa ni unafuu sana kwa wachezaji wa Simba na hasa mabeki. Kila mpira uliofika miguuni mwa Okwi, ulikuwa ukitulia na kutendewa haki huku Okwi akiwa anakabana na mabeki wazoefu.
Jaja yeye alikuwa akikabana na mabeki chipukizi. Hata kipa wa Simba, Manyika Peter, ni chipukizi aliyekuwa anajaribu mechi za Ligi Kuu, hakukuwa na mashambulizi ya maana yaliyomfikia kipa huyo na si sahihi kwa kijana huyo kupimwa ndani ya mchezo huo mmoja tu.
Pamoja na hisia tofauti za wengi, binafsi naamini mechi hii ilikuwa moja ya michezo inayozikutanisha Simba na Yanga iliyokosa mipango, wala hakukuwa na kasi ya uchezaji. Utulivu ulikuwa ziro kuanzia kwa mabeki hadi wafungaji, mchezo haukuwa na mashambulizi ya uhakika huku wataalamu Maximo na Patrick Phiri wakiwaacha benchi baadhi ya wachezaji mahiri.
Kwa Maximo, hii Yanga ambayo haina Okwi na Frank Domayo ndio iliyoitoa jasho Al Ahly ya Misri kwa mara ya kwanza na kutolewa kwa njia ya mikwaju ya penati, hii ndio Yanga iliyokuwa ikiwafunga watu mabao matano, sita hadi saba. Sasa hata bao moja kupatikana tabu.
Kwa Phiri, Simba hii inastahili pongezi, ni tofauti na alivyoikuta.