FILBERT BAYI: Miaka 51 rekodi yake bado inaishi
Muktasari:
- Bayi aliweka rekodi katika michezo ya Jumuiya ya Madola 1974 iliyofanyika Christchurch, New Zealand, Jumamosi, Februari 2, 1974. Alitumia dakika 3:32.16 na ni moja ya rekodi chache Jumuiya ya Madola zilizodumu muda mrefu. Rekodi mbili nyingine ziliwekwa na Waingereza, George Bailey katika mbio za maili mbili za kuruka viunzi na kukimbia kwenye vidimbwi vya maji (steeple chase) na ile ya Ian Thomson katika mbio za nyika (marathoni).
KWA sasa ni miaka 51 tangu mwanariadha nyota wa kimataifa wa Tanzania, Filbert Bayi alipoipatia rekodi ya kwanza na ya pekee ya dunia katika riadha. Nimeona nizungumzie habari za Bayi na alivyoweka hii rekodi kwa vile Watanzania wengi hawaelewi hasa ilikuwaje kutokana na habari zake kusikika kwa nadra na wala hakuna tuzo za kitaifa alizopewa au jengo, barabara ama daraja lililopewa jina lake hapa nchini.
Bayi aliweka rekodi katika michezo ya Jumuiya ya Madola 1974 iliyofanyika Christchurch, New Zealand, Jumamosi, Februari 2, 1974. Alitumia dakika 3:32.16 na ni moja ya rekodi chache Jumuiya ya Madola zilizodumu muda mrefu. Rekodi mbili nyingine ziliwekwa na Waingereza, George Bailey katika mbio za maili mbili za kuruka viunzi na kukimbia kwenye vidimbwi vya maji (steeple chase) na ile ya Ian Thomson katika mbio za nyika (marathoni).
Tangu Bayi alipoweka ile rekodi ya dunia hakuna Mtanzania aliyefanya vizuri katika riadha kama Bayi na nina shaka iwapo atatokea katika miaka ya karibuni kwa kuzingatia matayarisho yasiyoridhisha ya wanariadha katika mashindano ya kimataifa. Wakati Bayi alipoweka rekodi ile wengi zaidi ya nusu ya Watanzania wanaoishi hivi sasa walikuwa hawajazaliwa.
Kwa hivyo, naona ni vyema nielezee kilichotokea siku ile kule Christchurch.
Siku ile kamwe siwezi kuisahau. Nilifika ofisi ya Daily News na Sunday News iliyokuwa katika Barabara ya Maktaba, Dar es Salaam kujua matokeo ya mbio zile za mita 1,500 za mashindano ya Jumuiya ya Madola mapema asubuhi - muda mrefu kidogo kabla ya kuanza mbio saa 2 usiku kule Christchurch. Pale ofisini wengi tulitarajia kuwa Bayi atafanya vizuri, ila angeweza kuambulia medali ya shaba, lakini sio ya dhahabu. Hii ilitokana na kushindana na wakimbiaji mahiri zaidi ya sita wa nchi za Jumuiya ya Madola na wote walipewa nafasi kubwa ya kunyakua medali ya dhahabu.
Kati ya wote Bayi ndiye aliyekuwa na uzoefu mdogo wa mashindano makubwa kama ya Jumuiya ya Madola.
Baada ya kusubiri kwa nusu saa ofisini asubuhi tulimsikia kijana aliyekuwa na dhamana wa mtambo wa kupokea habari (tele printer), Kinyunyu, akipiga kelele kama mwendawazimu.
Alikuja chumba cha habari na kikaratasi kilichokuwa na sentensi moja tu ya maneno yaliyoandikwa “Bayi wa Tanzania ameshinda medali ya dhahabu ya mbio za mita 1,500 kwa kuweka rekodi mpya ya dunia.”
Nikiwa mhariri wa michezo akanikabidhi ile karatasi. Nilipoisoma taarifa ile sikuamini na nilimwambia Kinyunyu sio vizuri kufanya mzaha katika mambo ya kazi. Nilidhani yeye ndiye aliyechapa ile taarifa.
Alinimbia: “Kwa jina la Yesu Kristo sikufanya hivyo, bali hio ni taarifa ya Reuters (shirika la habari la Uingereza).”
Baada ya kuwadokeza wenzangu katika meza ya duara ya wahariri na wasanifu wa gazeti nilikwenda kwenye mtambo (wa tele printer) na kuona habari za Bayi zikimiminika na maelezo ya ushindi wake. Baada ya dakika chache yalikuja maelezo kwamba rekodi hiyo ilikuwa ya dakika 3: 32.16 na Bayi alifuatiwa na John Walker wa New Zealand, Ben Jipcho wa Kenya na Rod Dixon wa New Zealand
Nilimpigia simu aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, hayati Daudi Mwakawago kumpa taarifa ile kwa vile hakuwa nayo kutokana na Daily News kuwa ndio taasisi pekee wakati ule nchini iliyokuwa na tele printer.
Hakutaka kuamini na kuniuliza kama ni kweli au ndio utani niliokuwa nao.
Nilipomueleza siwezi kumtania kwa hilo alisema neno moja tu “nakuja.” Baada ya dakika zisizozidi 10 waziri alifika chumba cha habari akiwa anahema na kutoka jasho kama vile na yeye alikimbia mbio kama Bayi.
Kumbuka siku zile hapakuwepo na msongamano wa magari Dar es Salaam kwani ilikuwa inachukua kati ya dakika 10 hadi 15 kutoka Msasani kufika katikati ya jiji.
Waziri ambaye alitukuta tumejaa furaha kupongezana alimkumbatia mwandishi mmoja baada ya mwingine na akachukua zile karatasi za habari za Reuters na kwenda Msasani kumpa taarifa rasmi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Tulitaka kuwa na toleo maalumu (la gazetu) mchana ule, lakini wachapaji wetu - Printpak walikuwa wamefungua mashine kuzisafisha. Badala yake tuliamua kuongeza nakala za uchapishaji kwa 5,000 (wakati tulikuwa tunachapa nakala 35,000).
Siku ile magari yalijaaa nje ya ofisi ya Daily News kuanzia saa 2 usiku kusubiri gazeti ambalo nakala zake za kwanza zilichapishwa saa tatu usiku.
Habari za Bayi kuweka rekodi ya dunia zilichukua muda mfupi tu kuzagaa kila pembe ya Dar es Salaam na kelele za honi za magari na ving’ora vya magari ya kubeba wagonjwa zilisikika kila pembe ya jiji kutangaza habari za Bayi.
Miaka kama 12 hivi iliyopita nilimpigia simu Bayi kumweleza nilivyofurahi kumsikia mmoja wa wapinzani wake wakubwa katika mbio za masafa ya kati, Sebastian Coe wa Uingereza akikieleza kituo televisheni cha Sky katika kipindi cha matayarisho ya michezo ya Olimpiki iliyofanyika Uingereza wakati ule kwamba hawezi kumsahau Bayi maishani mwake.
Alimuelezea Bayi ambaye aliongoza mbio hizo mara baada ya kuanza na kubaki hivyo hadi mwisho kama mkimbiaji wa aina yake, aliyejiamini na aliyejua alichokuwa anafanya tangu mwanzo wa mbio hadi mwisho na zuri zaidi ni kwamba alikuwa mcheshi, hana maringo au majivuno. Nilikuja kufurahi zaidi kumuona Coe akimkaribisha Bayi jijini Monaco pale jina lake lilipoingizwa katika ukumbi wa wanariadha maarufu duniani.
John Walker wa New Zealand aliyekuwa wa pili Bayi alipovunja rekodi ya dunia kule Christchurch katika kitabu anachoelezea maisha yake, anasema: “Watachomoza wanariadha watakaokimbia kwa kasi zaidi na kuweka rekodi mpya, lakini hakuna kama Bayi katika mita 1,500 na maili moja. Mtanzania huyu alikuwa hatari na lazima nikiri ninamheshimu.”
Wakimbiaji maarufu wa zama zile wa masafa ya kati kama Brendan Foster wa Uingereza, Dick Quax wa New Zealand, Kipchoge Keino na Henry Rono wa Kenya wameeleza mengi juu ya ustadi na umahiri wa Bayi.
Rono ambaye katika kipindi cha siku 81 ka mwaka 1978 aliweka historia ya rekodi nne za dunia katika masafa ya kati anasema kama alipokimbia angekuwa na Bayi, basi alikuwa hana uhakika kama angepata mafanikio.
Kaka yangu hayati Elly Mboto aliyetangaza habari zile katika Redio Tanzania kila baada ya dakika chache alipata kigugumizi cha kutangaza kutokana na furaha kubwa aliyokuwa nayo.
Nchi nzima ilikuwa katika furaha na mpaka leo Watanzania wanasubiri kama atatokea mwanariadha mwingine atakayefanya makubwa kama Filbert Bayi.
Ninachosubiri ni kuona kama Bayi atapewa moja ya tuzo za utumishi uliotukuka katika taifa au jengo moja kubwa kupewa jina lake ili kutambua mchango wake katika michezo.