Baiskeli ya mashindano ya bei ghali zaidi
Muktasari:
- Je uliwahi kufikiria kwamba kuna baiskeli inayoweza kuuzwa kiasi hicho? Huo ndio ukweli, na hii ni miongoni mwa baiskeli zinazotumika katika mashindano mbalimbali makubwa duniani.
NEW YORK, MAREKANI: KAMA kuna mambo ya kushangaza, basi huja pale unapoambiwa jambo ambalo wala hukufikiria kwamba lingeweza kuwa vile ambavyo hujafikiria. Na hivyo ndivyo ilivyo pia katika baiskeli za magurudumu mawili, ambapo ile inayouzwa bei ya juu zaidi duniani inagonga Dola 1 milioni. Hapa unazungumzia takriban Sh2.5 bilioni.
Je uliwahi kufikiria kwamba kuna baiskeli inayoweza kuuzwa kiasi hicho? Huo ndio ukweli, na hii ni miongoni mwa baiskeli zinazotumika katika mashindano mbalimbali makubwa duniani.
Katika mazingira ya Kibongo Sh2.5 bilioni zinaweza kumiliki eneo kubwa sana la ardhi, na ni wazi kwamba mtu akiwa nazo anaweza kuwahamisha watu hususan katika mitaa ya pembezoni mwa miji au hata katikati.
Hii ni baiskeli moja tu duniani iliyopo ‘show room’ aina ya 24K Gold Extreme Mountain Bike kutoka The House of Solid Gold ambayo imebaki kuwa ghali kutokana na namna ilivyoundwa ikiwa na mifumo bora ya kumwezesha mtumiaji kuiendesha kwa kasi atakayo iwe katika milima au tambarare. Pia ina nakshi za madini ya dhahabu, shaba na almasi.
Lakini kama unamiliki baiskeli kwa ajili ya usafiri, mashindano au hata matumizi ya mazoezi ya kawaida uliinunua bei gani? Kwa hapa nchini baiskeli inayouzwa bei ya juu haizidi Sh500,000 na hii inatumika kwa ajili ya mashindano na mazoezi. Makala hii inakuletea baiskeli za kifahari na ghali zaidi duniani zikiwa ni zile zilizoundwa kwa utendaji na mifumo ya kisasa ya anasa yenye ubora wa kipekee kwa mtumiaji. Twende pamoja
14. Pinarello Dogma
Hii ni aina ya baiskeli ya kisasa, na zipo nyingi zinazotumia jina hilo ila chukua hili ‘Pinarello Dogma F Disc Campagnolo Super Record WRL’. Achana na urefu wa jina lake, lakini baiskeli hii ya kisasa imetengenezwa kwa ustadi nchini Italia kwa ajili ya mashindano ya kiwango cha juu, na inajulikana kwa kutawala mashindano ya Tour de France. Bei ya kawaida katika masoko ya Ulaya na Afrika ni Dola 16,000 (takriban Sh39.4 milioni).
Sifa kuu za baiskeli hii ni muundo na wepesi wake, ikiwa imetengenezwa kwa teknolojia ya TorayCa T1100 1K Dream Carbon yenye uimara hata inapopita katika vilima vyema mawe madogo madogo. Unapoiendesha ina uwezo wa kukabiliana na upepo mkali kumwezesha mtumiaji kutochoka haraka. Pia ina mfumo wa gia wa kielektroniki usiotumia waya kuunganishwa na magurudumu.
13. Bianchi Oltre
Aina ya baiskeli imekuja na tole jina linaloitwa Bianchi Oltre RC Tour de France Limited Edition Dura-Ace Di2 9200, ambayo inauzwa Dola 17,500 takriban Sh43.1 milioni. Baiskeli hii ya mashindano kutoka Italia ni toleo maalumu lililoundwa kwa heshima ya Tour de France - mashindano makubwa kabisa ya mbio za baiskeli duniani na yenye ushawishi na udhamini mkubwa. Ina muundo mzuri ikiwa na teknolojia ya juu ya kupunguza upinzani wa hewa na mfumo wa gia wa kielektroniki na pia ni nyepesi, imara na ina ufanisi wenye spidi kubwa.
Sababu ya bei kubwa ni kwamba aina hii ya basikeli ni adimu (zimetengenezwa 176 pekee duniani), zikiwa na vifaa vya ubora wa juu na pia uhusiano wake na tukio la kihistoria la michezo ya Tour de France 2025. Kuhusu Bianchi, hii ni kampuni ya baiskeli iliyoanzishwa 1885 nchini Italia. Bianchi ni moja ya chapa kongwe na mashuhuri zaidi duniani kwa ubunifu wa baiskeli za mashindano.
12. Audi Sport Racing Bike
Baiskeli hii ya mashindano inauzwa Dola 18,620 (sawa na takriban Sh45.8 milioni), na ni matokeo ya ushirikiano kati ya Audi na CarbonSports za Ujerumani. Ina fremu yenye uzito wa gramu 790, matairi mepesi ya Meilenstein na mfumo wa gia wa kiwango cha juu unaotengenezwa na kampuni maarufu ya utengenezaji baiskeli ya Shimano ya Japani.
Hata kiti chake kimetengenezwa kwa ngozi halisi ya Nappa (ngozi laini ya hali ya juu inayotengenezwa kutokana ngozi ya kondoo, ng’ombe au mbuzi yenye mwonekano wa kifahari) inayotumika kwenye Audi R8. Baiskeli hizo ziko 50 tu na ziliuzwa kupitia maduka maalumu ya Audi na wauzaji wa baiskeli za kifahari.
11. BMC Lamborghini Impec
Hii ni baiskeli ya kipekee iliyotengenezwa kuadhimisha miaka 50 ya kampuni ya magari ya kifahari duniani ya Lamborghini. Baiskeli hiyo iliyotengenezewa Uswisi inauzwa Dola 32,000 (takriban Sh78.7 milioni), imeundwa kwa mfumo wa breki wa Campagnolo Super Record Skeleton (unaotengenezwa na kampuni ya Campagnolo ambayo ni mojawapo ya wazalishaji maarufu wa vipuri vya baiskeli duniani hasa za mashindano. Inatumia gia za kielektroniki, fremu ya kifahari sawa na ile inayotumika kwe-nye magari ya Lamborghini. Zipo za rangi ya njano na nyeusi kipekee na zilitemgenezwa 50 tu.
10. Gucci ‘Guccissima’ Cruiser Bike
Ni baiskeli ya kifahari inayouzwa Dola 35,000 (takriban Sh85.9 milioni) na ni aina ya cruiser iliyotengenezwa kwa mikono nchini Italia na kupambwa kwa ngozi halisi iliyo na nembo ya Gucci Guccissima. Ilianza kwa kuuzwa katika maduka machache ya Gucci na sasa hupatikana tu katika minada ya kifahari.
9. Litespeed Blade
Litespeed Blade inauzwa Dola 40,788 (takriban Sh100.3 milioni) na ni miongoni mwa baiskeli chache zilizoundwa Marekani kwa madini aina ya titanium. Inajulikana kwa kasi, uimara na muundo wa kifahari. Titanium ni ghali zaidi kuliko alumini au kaboni, na ndiyo sababu bei yake ni ya juu.
8 Montante Luxury Gold Collection
Usafiri huu unauzwa Dola 46,000 (takriban Sh113.1 milioni) kutoka Italia na ni mahususi kwa ajili ya wanawake ukiwa umepambwa kwa nakshi za dhahabu na madini mengine, huku pia ikiwa na ngozi ya chatu kwenye kiti na fremu ya juu. Ni mfano mwingine wa baiskeli ya kifahari unaotambulika duniani.
7. Chrome Hearts X Cervelo
Baiskeli hii ya milimani ni matokeo ya ushirikiano kati ya kampuni za Chrome Hearts (Marekani) na Cervelo ya Canada. Ina thamani ya Dola 60,000 (zaidi ya Sh147.6 milioni). Usafiri huu upo wa rangi nyeusi na nyekundu na umepambwa kwa madini ya thamani. Hizi zipo baiskeli 10 pekee.
6. Trek Madone 7: Diamond Bike
Kama una Dola 75,000 (zaidi kidogo tu ya Sh184.5 milioni) unaweza kuumiliki usafiri huu wa mashindano uliorembwa kwa madini ya almasi. Mojawapo wa baiskeli hizo iliwahi kupigwa mnada katika hafla ya Lance Armstrong Foundation Gala. Ni moja ya baiskeli za kwanza za aero zenye kasi ya juu zaidi duniani.
5. Aurumania Gold Bike Crystal Edition
Baiskeli hii kutoka Skandinavia imepakwa dhahabu ya karati 24 na kupambwa kwa madini ya kifahari yanayopatikana katika milima ya Himalaya. Kwa sasa sokoni inapatikana kwa Dola 114,000 (zaidi ya Sh280.4 milioni). Watengenezaji walitumia mikono na si mashine.
4. Kaws: Trek Madone
Unaweza kuipata kwa Dola 160,000 (takriban Sh393.5 milioni) na ukaitumia kwa mambo mbalimbali ikiwamo mashindano ya baiskeli. Trek Madone imeundwa kwa ushirikiano kati ya msanii maarufu KAWS, kampuni ya Trek na mpanda baiskeli maarufu Lance Armstrong. Fremu yake ina mchoro wa mzuri na ina nakshi za madini kibao katika sehemu mbalimbali. Mara ya mwisho iliuzwa katika mnada wa Sotheby’s kuchangia taasisi ya Lance Armstrong Foundation.
3. Trek Yoshitomo Nara
Baiskeli hii inapatikana kwa Dola 200,000 (takriban Sh491.9 milioni), ambapo imeundwa na msanii wa Kijapani Yoshitomo Nara ikiwa na michoro ya kipekee yenye mtindo wa katuni.
2. Trek Butterfly Madone
Usafiri wa kifahari unaouzwa Dola 500,000 (takriban Sh1.23 bilioni). Baiskeli hii ni matokeo ya kazi ya msanii Damien Hirst ikiwa imepambwa kwa mabawa ya vipepeo. Mara ya mwisho iliuzwa katika mnada wa Sotheby’s kwa ajili ya kuchangia taasisi ya Livestrong Foundation.
1. 24K Gold Extreme Mountain Bike
Hii ndiyo baiskeli ghali zaidi duniani ikiwa inauzwa kwa Dola 1 milioni (Sh2.5 bilioni). Usafiri huu umeundwa na kampuni ya The House of Solid Gold ya Beverly Hills, Marekani. Imefunikwa kwa dhahabu ya karati 24, kiti cha ngozi ya mamba, na nembo yenye vito vya thamani. Zipo basikeli 13 tu duniani kwa sasa.
Kwa ujumla thamani ya baiskeli hizo zote inatokana na madini yaliyotumika kuzitengeneza, uimara wa vyuma uliolainishwa kitaalamu ili kuzifanya ziwe nyepesi na ubora wa chapa. Pia zimetengenezwa chache sokoni. Vilevile nyingi kati ya hizo zina bima ya ajali na kupotea (yaani iwapo zitaibiwa), kuwezesha mhusika kupata fidia nono kutoka mashirika makubwa ya bima duniani.