CYCLE BALL: Mchezo wa mpira unaotumia baiskeli
Muktasari:
- Mchezo wa Cycle Ball, au unaweza kuuita radball kwa Kijerumani, ni mchezo wa kipekee unaowataka wachezaji kutumia baiskeli kucheza soka badala ya miguu yao.
MUNICH, UJERUMANI: PENGINE umezoea kuona mpira wa miguu ukichezwa kwa kutumia miguu, lakini vipi kuhusu hii ya mchezo wa mpira ambao wachezaji hawaupigi kwa miguu bali baiskeli pekee?
Mchezo wa Cycle Ball, au unaweza kuuita radball kwa Kijerumani, ni mchezo wa kipekee unaowataka wachezaji kutumia baiskeli kucheza soka badala ya miguu yao.
Ingawa haujulikani sana duniani, Cycle Ball ni mchezo maarufu sana barani Ulaya hususani nchi kama Ujerumani, Uswisi na Austria ambazo zina hadi ligi. Leo tumekusogezea ufahamu kwa undani zaidi kila kinachouhusu.
HISTORIA
Cycle Ball ilianzishwa mwanzoni mwa karne ya 20 na mchezaji wa Ujerumani, Nicolai ‘Nikolaus’ Dufner, mwaka 1893. Awali, ilikuwa ni burudani ya kawaida kama sehemu ya kujifurahisha na ulichezwa zaidi ndani.
Kisha ulipata umaarufu kwa haraka kutokana na kuingizwa kwenye mashindano rasmi ya kimataifa mwaka 1929, ambapo kwa mara ya kwanza mataifa yalichuana huko Ulaya.
Upekee wa mchezo huu kiasi cha kuvutia watu wengi ni kitendo cha wachezaji kutopiga mpira kwa miguu na badala yake kutumia baiskeli.
SHERIA, KANUNI
Cycle Ball ina kanuni maalumu ambazo zinahakikisha mchezo unaendelea kwa usawa na usalama:
Kila timu ina wachezaji wawili tu ambao wanaweza kufanyiwa mabadiliko na wachezaji wengine waliopo benchini.
Wachezaji hutumia baiskeli maalumu ambazo hazina breki na huwa zina gia moja tu ili kuwasaidia kudhibiti mpira.
Ni marufuku wachezaji kugusa mpira kwa miguu au mikono badala yake wanatakiwa kutumia baiskeli tu, hasa sehemu ya mbele.
Goli huwa ni la kawaida kama la katika mpira wa miguu na huhesabiwa pale mpira unapopitia mstari wa goli la mpinzani.
Kawaida mechi huwa na vipindi viwili, lakini ni tofauti na vile vya mpira wa miguu wa kawaida. Hapa kwa mechi za wakubwa huwa kuna kipindi cha kwanza cha dakika 10 na kipindi cha pili cha dakika 10, kwa upande wa watoto huwa kuna vipindi viwili pia lakini huwa ni dakika saba kila kipindi.
UWANJA
Cycle Ball huchezwa kwenye uwanja wenye sakafu mara nyingi huwa ni mbao na hauchezwi nje, badala yake huchezwa kwenye viwanja vya ndani kama ilivyo kikapu au Futsal.
Mbali ya sakafu ya mbao, pia kuna viwanja vimewekwa sakafu laini ya plastiki ili mchezaji hata akidondoka asiumie.
Kwa mashindano ya kimataifa, urefu wa kiwanja kinachochezewa hutakiwa kuwa na kati ya mita 14 hadi 16 na upana mita saba hadi tisa.
Kama mpira wa miguu, uwanja wake huwa na mstari wa eneo la goli, katikati na sehemu nyingine.
ZAWADI
Katika mashindano ya Cycle Ball, kama ilivyo katika mashindano mengine ya michezo ya kimataifa kama Olimpiki, washindi hupokea medali za dhahabu, fedha, au shaba kulingana na nafasi wanazomaliza.
Wachezaji bora hupokea vyeo vya mabingwa wa taifa au kimataifa.
Vilevile huwa kuna zawadi za kifedha katika mashindano makubwa ambapo washindi hupata zaidi ya Euro 200,000.
NCHI ZINAZOSUMBUA
Ujerumani, Uswisi na Austria ndio nchi zinazocheza zaidi mchezo huu kwa kuwa na ligi ya ndani na nchi hizo ndio zinaongoza duniani kwa sasa zikiwa na idadi kubwa ya mastaa ambao ni mabingwa wa mchezo huu.
Shirikisho la Union Cycliste Internationale (UCI) ndio linasimamia mashindano haya duniani likiwa linafanya kazi kama FIFA.
Mashindano ya kimataifa yanaitwa UCI Cycle Ball ambayo huandaliwa na UCI na kushirikisha nchi wanachama wa mchezo huu.
WACHEZAJI NYOTA
Mjerumani Peter Porschke ni miongoni mwa wachezaji mashuhuri na bora wa mchezo huu kwa sasa, pia Dominik Planzer anayetokea Uswisi ni miongoni mwa wanaosumbua ni kama vile Cristiano Ronaldo na Lionel Messi walipokuwa katika ubora wao.