Enrique apata ajali ya baiskeli, kufanyiwa upasuaji
Muktasari:
- Tukio hilo lilitokea Ijumaa iliyopita wakati kocha huyo Mhispaniola, Enrique alipokuwa kwenye mazoezi yake ya kuendesha baiskeli. Baada ya kufikichwa hospitali, vipimo vilionyesha bosi huyo wa Parc des Princes alikuwa na ufa kwenye mfupa wake wa bega.
PARIS, UFARANSA: KOCHA wa Paris Saint-Germain, Luis Enrique alilazimika kuwahishwa hospitalini baada ya kupata ajali ya baiskeli na kuumua mfupa wa mabega.
Tukio hilo lilitokea Ijumaa iliyopita wakati kocha huyo Mhispaniola, Enrique alipokuwa kwenye mazoezi yake ya kuendesha baiskeli. Baada ya kufikichwa hospitali, vipimo vilionyesha bosi huyo wa Parc des Princes alikuwa na ufa kwenye mfupa wake wa bega.
Hata hivyo, Enrique anashukuru kwamba hakupata madhara makubwa sana kutokana na ajali hiyo, licha ya kwamba atahitaji kufanyiwa upasuaji ili kurekebisha eneo hilo lililopata madhara.
PSG ilitangaza ajali hiyo ya Enrique kwenye chaneli zake za mitandao ya kijamii, ambapo taarifa hiyo ilisomeka hivi: "Kufuatia ajali ya baiskeli iliyotokea Ijumaa, kocha mkuu wa Paris Saint-Germain, Luis Enrique alihitaji kupatiwa huduma ya dharura na atafanyiwa upasuaji wa kurekebisha ufa uliojitokeza kwenye mfupa wake wa bega.
"Klabu inampa sapoti muda wote na inamtakia apone haraka. Taarifa nyingine zitawajia."
Taarifa hiyo iliwavuta mashabiki wa soka kutoka duniani kote na kuweka komenti zao kwenye mitandao ya kijamii wakijaribu kumtakia heri kocha huyo wa zamani wa Barcelona.
Shabiki wa kwanza aliandika kwenye X: "Nakutakia upone haraka, kila la heri."
Mwingine alisema: "Pona haraka."
Na kuna shabiki alisema: "Jamani. Upone haraka."
Shabiki mwingine aliandika: "Namtakia kila la heri."
Bado haijawekwa wazi kilichosababisha ajali hiyo kama Enrique aligongwa na gari akiwa na baiskeli yake ay alianguka tu mwenyewe. Enrique amekuwa na kawaida ya kushiriki kwenye mbio za baiskeli kila anapojisikia kufanya hivyo.
Machi 2023, alishiriki kwenye mbio za siku za nane za kilomita 700 za kuendeesha baiskeli huko Afrika Kusini. Enrique aliweka historia msimu uliopita wakati alipoipa PSG mataji matatu ndani ya msimu mmoja, ikiwamo taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.