Ronaldo aenda Arsenal? Fikiri, halafu fikiri tena

SHABIKI mnazi wa Arsenal, Piers Morgan anashikilia bango kuitaka Arsenal imsajili supastaa wa Ureno, Cristiano Ronaldo kwamba aende kuongeza nguvu wakati huu wakiwa kwenye msimu wao bora kabisa.
Cristiano Ronaldo aende Arsenal? Tafadhali, hebu fikiria, halafu fikiria tena.
Si kitu cha kushangaza kwenye soka la siku hizi, lakini ushauri wa kumtaka Mikel Arteta amchukue Ronaldo kwa sababu tu anapatikana bure kutoka Manchester United ni jambo linalohitaji kufikiriwa kwa kina. Arsenal isiingie mkenge huu kwa sababu Piers Morgan amekuwa akipiga kelele za kumtaka swahiba wake Ronaldo atue Emirates. Kishabiki utamuunga mkono Morgan.
Lakini, kwenye uhalisia, je, Arsenal inamhitaji Ronaldo? Hakuna ubishi, Ronaldo ni mwanasoka mahiri, mmoja kati ya magwiji kabisa. Lakini, kwa sasa ni tofauti kabisa na kila Arsenal inachokihitaji. Wakati akiwa Old Trafford, alitaka kuonyesha yeye ni mkubwa kuliko klabu. Je, hatafanya hivyo akiwa Emirates? Ameifanyia timu yenye mataji 20 ya Ligi Kuu England, matatu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Hataonyesha dharau mbele ya Arsenal yenye mataji 13 ya Ligi Kuu England na taji sifuri la Ligi ya Mabingwa Ulaya? Fikiri halafu fikiria tena.
Sawa unaweza kusema kwenye vyumba vya kubadilishia nguo kwa sasa Arsenal inamhitaji mtu aliyeshiba uzoefu kama yeye. Lakini, ni wazi hilo haliendani na mtazamo wa Kocha Arteta. Arsenal na kocha wametumia misimu miwili iliyopita, kuwaondoa wachezaji wanaojifanya wakubwa kwenye timu ili kutuliza hali ya mambo kwenye vyumba vya kubadilishia.
Imemwondoa Mesut Ozil. Imemwondoa Pierre-Emerick Aubameyang na imewaondoa wengine kibao waliokuwa wakijiona kuwa ni wakubwa kama vile Willian, David Luiz na wengineo. Na ukiutazama msimamo wa Ligi Kuu England kwa sasa, unaweza kuona hilo limeleta matundo mazuri. Hii haikuwa na maana kwamba Arteta hawezi kuwaongoza wachezaji wakubwa, kama ambavyo Aubameyang alivyosema alipoondoka kwenye timu hiyo mwaka jana, bali kuondoa wanaojiona wakubwa kuzidi timu.
Kwa sasa Arsenal imebaki na kundi la wachezaji wanaoaminiana. Kila mmoja anamwamini mwenzake na kila mmoja anapambana kwa ajili ya mwenzake. Hicho ndicho kinachohitajika kwenye timu ya aina yoyote ile. Kupambana pamoja.
“Hatuwaruhusu wanajiona wakubwa,” alisema Mohamed Elneny wakati alipoulizwa kile kinachoifanya kikosi cha Arsenal kwa sasa kuwa na mshikamano mkubwa chini ya Kocha Arteta. “Hivyo ndivyo tulivyo vyumbani kwa sasa. Kila mtu anampenda mwenzake, anapambana kwa ajili ya mwingine. Hilo ndilo linalofanya kikosi chetu kuwa imara, kwa sababu hatutaki wanaojiona wakubwa kwenye timu yetu.”
Maneno hayo yanasadifu kile kinachoendelea Arsenal kwa sasa. Mchakato huo ulifanyika kwa zaidi ya miaka miwili na sasa kila kitu kinakwenda sawa, Arsenal ipo kileleni kwenye msimamo wa ligi, tena kwa tofauti ya pointi tano.
Kuhusu Ronaldo, Morgan alisema hivi: “Gabriel Jesus anahitaji pacha wake pale mbele. Arsenal inahitaji mnyama kwenye boksi, mchezaji wa kiwango cha dunia aliyejaa uzoefu, ambaye alishinda kila kitu, atatusaidia kufika tunapopataka.
“Naweza kumfikiria mtu fulani Cristiano Ronaldo! Ningeweza kumsajili kwa miezi sita. Hii ya kusema Ronaldo sasa hachezi mpira, hapana, ni kichekesho.”
Ukweli ni kwamba hakuna anayesema Ronaldo hawezi kucheza mpira, hafai. La, anaweza na ukitazama idadi yake ya mabao aliyofunga Man United msimu uliopita, bado anaweza kufanya jambo kama timu itajengwa kumzunguka yeye na kuhakikisha anapewa mipira muda wote. Lakini, hilo si Arsenal wanalolitaka kwa sasa.
Arsenal inahitaji teamwork, inakaba pamoja, inashambulia pamoja. Je, Ronaldo ataweza? Kwenye umri wake kuna namba 37. Na je, hatataka mshahara utakaoanza kuvuga vyumba vya kubadilishia hapo Emirates? Arteta aliwaondoa wote wenye mishahara mikubwa na sasa mchezaji wake anayemlipa pesa nyingi kwa wiki ni Thomas Partey, Pauni 250,000 kwa wiki.
Je, Ronaldo aliyezoea kulipwa mkwanja unaoanzia Pauni 400,000 kwa wiki kwenda juu - atakubali kushuka?
Ipo sehemu inayomfaa Ronaldo kwa kipindi hiki anachoondoka Manchester United, lakini kwa bahati mbaya sana sehemu hiyo si Arsenal. Atakwenda kuwavuruga wajute. Hata Arsenal hawapo pia kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, michuano ambayo Ronaldo anataka kucheza.