Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sitaki tena Urais – Sehemu ya 21

RAIS 21 Pict

ILIKOISHIA

Ilikuwa saa tatu asubuhi, Rais Shanga akiwa ofisini kwake ikulu alipojulishwa kuwa mkuu wa jeshi la polisi amefika ikulu akiomba kukutana naye.

Rais Shanga alitoa ruhusa mkuu huyo aingie ofisini kwake. Mkuu wajeshi la polisi alipoingia ofisini humo alisalimiana na rais na kumueleza kuwa kulikuwa na tatizo lililotokea kwa upande wa polisi.

“Tatizo gani?” Shanga akamuuliza. Mkuu wa Jeshi la Polisi alifungua mkoba wake na kutoa fomu tatu za kundi la freemaso zilizokuwa na majina ya Rais Shanga. Kanal Mbasha na aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani.

SASA ENDELEA


“JANA usiku tulianza kuwakamata hawa watu. Tumewaweka ndani viongozi saba wa kundi lao. Kiongozi wao mkuu bado anatafutwa. Sasa tulikuta hizi fomu za wanachama wao. Fomu moja ina jina lako na picha yako, fomu nyingine ina jina na picha ya Niwako aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani na fomu nyingine ina jina na picha ya Kanali Mbasha aliyeongoza uasi na kuuawa na maafisa usalama.” Mkuu wa jeshi alimwambia Rais Shanga na kumuonesha zile fomu.

Ingawa kulikuwa na kifaa cha kuingiza hewa ya baridi ofisini kwa rais, Shanga alihisi mwili wake ukimfumka moto na mara moja uso wake ukajaa tembe za jasho.

Alizitupia macho fomu hizo na kufahamu kuwa zilikuwa fomu sahihi za wahusika. Fomu iliyokuwa na jina na picha yake aliijaza yeye mwenyewe wakati anajiunga na kundi hilo ingawa ingawa sahihi aliyoweka ilikuwa tofauti.

Uso wake uliokuwa mtulivu sasa ulianza kutaharuki.

“Hawa ni watu wa ajabu sana. Wanajaribu kutengeza fomu bandia na kuweka picha za watu wasiohusika ili kudanganya wanachama wao!” Rais Shanga akasema kwa hasira.

“Kiongozi wao mmoja alipoulizwa alisema Kanali Mbasha na Niwako ni wanachama wao. Lakini alipoulizwa kuhusu wewe hakujibu ila alisema uulizwe mwenyewe”

“Niulizwe nini? Hawa watu bure kabisa!. Wanataka kuchafua majina ya watu!”

“Mheshimiwa rais tutawafungulia kesi nyingine ya kugushi jina lako katika fomu zao”

Shanga aliona kama viongozi hao watafikishwa mahakamani na kufunguliwa kesi hiyo, yatazuka makubwa. Wanaweza kueleza kila kitu.

“Hapana, msiwafikishe mahakamani. Hizi fomu ziache hapa. Suala lao litashughulikiwa na ikulu. Kwa hiyo ninaagiza wawekwe kizuizini hadi hapo nitakapoeleza vinginevyo”

“Sawa mheshimiwa. Je kuhusu ile kesi ya mwanzo ya kuvunja amri ya serikali ya kuwapiga marufuku?”

“Nimesema wawekwe kizuizini. Suala lao litashughulikiwa na ikulu”

“Nimekuelewa mheshimiwa?”

                                    ***************

Zilikuwa zimepita siku tatu tangu Osaka na wenzake wawekwe kizuizini kwa amri ya Rais Shanga. Dhamiri ya Rais Shanga ilikuwa kuwatia adabu viongozi hao ili wasithubutu tena kuijaribu serikali yake na pia wasitishe kabisa shughuli za chama chao nchini humo.

Siku ile ya tatu Shanga alipokea barua binafsi iliyowasilishwa kwa anuani ya ikulu. Afisa wake aliyekuwa akishughulikia nyaraka zinazokwenda kwa rais alitakiwa aifungue bila kuisoma na kisha aipeleke kwa rais.

Shanga alipopelekewa barua hiyo hakujua ilikuwa inatoka kwa nani ingawa ilionesha kuwa ilitoka Afrika Kusini.

Akaisoma. Maelezo ya mwanzo tu yalianza kumshitua. Ilikuwa inatoka kwa kiongozi wa Freemaso wa Afrika aliyekuwa anaishi Cape Town nchini Afrika Kusini.

Barua ilihusu kukamatwa na kuwekwa kizuizini kwa viongozi saba wa kundi hilo. Kiongozi huyo alimtaka Rais Shanga kuwaachia mara moja viongozi hao na bila masharti yoyote kwa kile alichodai kuwa hawakuvunja sheria yoyote ya nchi.

Shanga alipomaliza kuisoma barua hiyo aliikunja na kuitia kwenye mfuko wa koti lake kisha akawaza kwa sekunde kadhaa.

Alijiambia kwamba utawala wake sasa ulikuwa umeanza kuingiliwa na mamluki kutoka nje. Kitendo kile cha kuandikiwa barua na kiongozi wa taasisi ya kiraia na kutakiwa kuwaachia watu ambao aliamini walivunja sheria nchini mwake, kilimkera.

“Sitawaachia” akajiambia “Mimi ndiye rais wa nchi hii. Hakuna mtu yeyote anayeweza kunifundisha nifanye nini!”

Kwa sababu ya kutaharuki Shanga alitoka ofisini kabla ya muda wake na kutaka afikishwe nyumbani kwake.

Dukuduku la roho lilimfanya amuoneshe mke wake ile barua.

“Amenitumia kiongozi wa Freemaso wa Afrika”


“Anataka nini?” Mke wake alimuuliza wakati anaipokea.

“Anataka niwaachie wale viongozi wa kundi lao tuliowakamata”

Mke wa rais aliisoma ile barua.

“Ana mamlaka gani ya kuingilia mambo ya nchi yetu?” akauliza mara tu alipomaliza kuisoma.

“Isitoshe wale ni wahalifu wa sheria, wamevunja amri ya serikali na pia wanajihusisha na vitendo vya kihaini”

“Halafu bado anataka waachiwe!”

“Na sitawaachia!”

“Mimi najua wewe ndiye mwenye mamlaka na maamuzi yote, si mtu mwingine”

“Na maamuzi yangu ndiyo hayo. Watakaa kizuizini mpaka hapo nitakapoamua vingineyo. Na kuna kiongozi wao mkuu wa hapa nchini hakukamatwa. Nitamuagiza mkuu wa jeshi la polisi kuhakikisha mtu huyo anakamatwa na kuunganishwa na wenzake”


 *********************

Ilikuwa saa sita mchana wakati mkuu wa jeshi la polisi na mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai walipomaliza mazungumzo yao.

Mkurugenzi wa upelelezi alirudi ofisini kwake na kumuita Shamla. Kachero Shamla alipofika mkurugenzi huyo alimuuliza.

“Umeshamkamata kiongozi mkuu wa Freemaso?”

Kachero Shamla hakutegemea kuulizwa swali kama hilo na hivyo hakuwa amejiandaa kutoa jibu maridhawa. Mara tu baada ya viongozi saba wa Freemaso kukamatwa na kuwekwa kizuizini, Shamla hakushughulika tena kumtafuta kiongozi wao mkuu akisubiri amri kutoka ngazi za juu.

“Kwa kweli hajakamatwa kwa sababu…..”

“Shamla unataka kutoa sababu gani wakati jukumu la kumkamata ni lako wewe?” Mkurugenzi alimkatiza Shamla.

“Ni kweli afande. Siku ile tulimkosa. Tuliwakamata wale wengine tu. Nilikuwa nasubiri….”

“Ulikuwa unasubiri nini?. Mbona unanipa hadithi za sungura na paka wakati nilshakupa jukumu la kuwakamata viongozi wote wa Freemaso!”

Shamla alinywea na kunyamaza. Si cheo tu cha bosi wake kilichomtisha bali umri wake pia. Alikuwa amemzidi kwa zaidi ya miaka kumi. Shamla alizingatia kwamba heshima kilikuwa kitu muhimu kwenye kazi za jeshi na kiubinaadamu.

“Sasa sikiliza, mkuu wa jeshi la polisi amepewa agizo na rais hii asubuhi ahakikishe kuwa kiongozi huyo anakamatwa. Hivyo ninakupa tena jukumu hilo. Ninataka umtafute na kumkamata kiongozi huyo haraka iwezekanavyo”

“Sawa afande”

                                      **********************

Polisi wa Kamisa walikuwa wameacha kuweka ulinzi katika jumba la Freemaso siku mbili tu baada ya kuwakamata viongozi wa kundi hilo. Walimuacha mlinzi wa jumba hilo aendelee na kazi yake.

Katika kuanza upelelezi wao wa kumtafuta na kumkamata kiongozi mkuu wa kundi hilo Shamla na kachero mwenzake walifika tena katika jumba hilo.

Walimkuta mlinzi wa jumba hilo huku jumba lenyewe likiwa kimya.

“Wako wapi wahusika ?” Shamla alimuuliza mlinzi huyo.

“Wahusika hawapo” Mlinzi alimjibu akionesha kuwa na wasiwasi.

“Najua kwamba baadhi ya viongozi tuliwakamata hivi karibuni, nina maanisha wahusika wengine”

“Hawapo”

“Una maana hakuna anayefika katika jumba hili?”

“Bado sijaona mtu”

“Yaani unakuja kulinda jumba tupu na kuondoka?”

“Ndiyo jukumu langu”

“Si kweli. Wewe umefundishwa jinsi ya kuzungumza na polisi?”

“Hapana sijafundishwa. Ninachosema ni kitu cha kweli”

“Kuna kiongozi mkuu wa kundi hili tunamtaka. Tuambie mahali alipo”

“Kwa kweli siwezi kujua”

Shamla alimtazama yule mlinzi kisha alimwambia.

“Tunataka kuingia ndani”

“Wenyewe wameniambia nisiruhusu mtu kuingia”

“Wenyewe kina nani, wakati umeniambia hakuna mtu yeyote aliyefika hapa”

Mlinzi huyo alihamanika na kutaka kusema neon kwa pupa lakini alisita ghafla na kubaki kumtazama Shamla. Bila shaka  Bila shaka aliona alichotaka kusema hakikuwa na maana.

“Tupishe” Shamla alimwambia mlinzi huyo ambaye aliwapisha kwenye geti. Shamla na kachero mwenzake wakaingia ndani. Macho ya makachero wote wawili yalielekea kwenye gari moja iliyokuwa kwenye banda la magari. Ilikuwa gari mpya aina ya benz ya rangi nyeusi.

“Gari lile ni la nani?” Shamla akamuulizamlinzi huyo.

“Ni la wenyewe”

“Wamo ndani?”

“Ni mtu mmoja tu aliyeko ndani”

“Ni nani?”

“Nimeambiwa nisimtaje”

Shamla alihamaki na kumkwida ukosi mlinzi huyo.

“Usituletee upuuzi hapa!. Tuambie nani yuko ndani?”

“Ni Master!” Mlinzi alijibu kwa sauti ya kigugumizi huku koo lake likiwa limekaba pamoja na ukosi wa shati lake.

Shamla akamuachia na kumwambia kachero mwenzake.

“Twende ndani tukamkamate”

Wakatembea kwa hatua za haraka kuelekea kwenye lango la jumba hilo.

“Huyo mtu ndiye tuliyekuwa tunamtaka. Yule mlinzi alikuwa anajaribu kutubabaisha” Shamla alisema wakati wanaingia katika jumba hilo.

Kwa vile jumba hilo walishaliingia na kulipekua walikuwa wakizijua sehemu zake zote.

“Twende moja kwa moja kwenye ofisi yake” Shamla aliendelea kumwambia kachero mwenzake.

Walipanda ngazi hadi ghorofa ya pili ilipokuwa ofisi ya Master.

Kabla ya kuifikia ofisi ya Master kulikuwa na sebule na hapo ndipo walipomkuta Master ameketi akiangalia tv iliyounganishwa na kamera iliyokuwa inamulika geti.

Tv hiyo ilikuwa ikimuonesha mlinzi aliyekuwa kando ya geti akisikitika peke yake. Pengine ni wa sababu ya wale makachero kumzidi nguvu na kuingia ndani.