Sitaki tena Urais – Sehemu ya 19
ILIKOISHIA
Taarifa hiyo ilimchukiza Rais Shanga akampigia simu waziri mkuu na kumuita ofisini kwake.
Dakika chache baadaye, waziri mkuu alipowasili ofisini kwake Shanga alimuulizia kuhusu agizo lake la kupiga marufuku shughuli za freemaso.
“Unakumbuka nilikuagiza nini?” Shanga alimuuliza.
“Nilitekeleza agizo lako mheshimiwa Nimehakikisha kuwa usajili wa kundi hilo umefutwa na niliwapelekea barua kuwajulisha kuwa usajili wao umefutwa na shughuli zao haziruhusiwi nchini mwetu”
SASA ENDELEA
“Umehakikisha kuwa kweli wamesimamisha shughuli zao?”
“Ndiyo.”
“Nimepata taarifa kuwa kundi hilo bado linaendelea na shughuli zao kama kawaida.”
“Kama ni hivyo, watakuwa wanafanya kosa la kukiuka agizo la serikali.”
“Hawa watu wanaonesha ukaidi. Sasa ninakuagiza kuhakikisha kwamba viongozi wote wa kundi hilo wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa kukiuka agizo la serikali na kuendesha shughuli zao huku wakijua kuwa wamepigwa marufuku. Umenielewa?”
“Nimekuelewa, mheshimiwa.”
“Sasa nenda ukafanye kazi hiyo.”
Waziri mkuu aliporudi ofisini kwake, naye alimwita waziri mpya wa mambo ya ndani kwa simu.
Waziri huyo alifika ofisini kwa waziri mkuu dakika chache tu baadaye.
“Siku ile nilikuagiza ufute usajili wa Freemasons na niliwaandikia barua ya kupiga marufuku shughuli zao. Je, umefuatilia na kuhakikisha wametii agizo la serikali?” Waziri mkuu akamuuliza waziri wa mambo ya ndani.
“Kwa kweli sikufuatilia, mheshimiwa. Labda nianze sasa kuwatuma vijana wangu wafanye uchunguzi.”
“Nimepata taarifa kutoka kwa mheshimiwa rais kuwa bado watu hao wanaendelea na shughuli zao kama kawaida, wakati tulikwishawapiga marufuku. Sasa ninakutaka uanzishe operesheni maalumu ya kuwakamata viongozi wao ili wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.”
“Ni vizuri kwanza tuwe na ushahidi kuwa wanaendelea na shughuli zao kabla ya kuwakamata.”
“Mheshimiwa rais anazo taarifa kuwa wanaendelea na shughuli zao na ameagiza wakamatwe.”
“Ili sisi tuweze kupata ushahidi kuwa wamekiuka agizo la serikali na tuweze kuwafikisha mahakamani, ni vyema tufuatilie nyendo zao kwanza kabla ya kuwakamata.”
“Utahitaji muda gani?”
“Ninachofahamu ni kuwa wanakuwa na mikutano yao siku za Jumamosi na Jumanne usiku. Jumanne ni leo. Nitatuma vijana wangu wawafuatilie. Endapo watakutwa wamekusanyika, watakamatwa.”
“Sawa. Fanya hivyo, halafu unifahamishe umefikia wapi ili niweze kumpatia taarifa mheshimiwa rais.”
“Sawa, mheshimiwa.”
Waziri wa mambo ya ndani alipotoka ofisini kwa waziri mkuu, alirudi ofisini kwake na kuwapigia simu mkuu wa jeshi la polisi na mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai nchini humo.
Maofisa hao walipofika ofisini kwake, waziri huyo aliwaeleza kuhusu agizo lililotolewa na rais.
“Wale hukutana kila Jumamosi na Jumanne. Mnaweza kuwatuma makachero wawili wajanja kwenda kufanya uchunguzi?”
“Tunaweza kuwatuma,” mkurugenzi wa upelelezi alimjibu.
“Haitatakiwa watambulike, na inatakiwa waingie ndani kabisa ya jumba lao na wajumuike nao kama wenzao. Tunataka tupate ushahidi wa kuwafikisha mahakamani,” waziri wa mambo ya ndani aliendelea kuwaeleza.
Katika kikao hicho, uliandaliwa mpango kabambe wa kuwapenyeza makachero wawili ndani ya jumba la watu hao lililokuwa katika eneo la Osariver.
Makachero hao, ambao walitakiwa kuvaa suti nyeusi, walitakiwa kujumuika na watu hao kama wanachama. Kwa vile mkusanyiko wa watu hao ulihusisha watu wengi, ilitarajiwa makachero hao wasingeweza kutambulika kirahisi.
Maofisa hao walikubaliana kuwa endapo makachero waliotumwa wangetambulika, wajitambulishe kuwa ni makachero na kisha wawapigie simu polisi wenzao watakaokuwa wakiwasubiri nje ya jumba hilo.
Mpango huo ulitaka kuwepo na magari mawili ya polisi pamoja na polisi wa kutosha wenye silaha na mabomu ya kutoa machozi.
Polisi hao, watakapopigiwa simu na makachero watakaokuwa ndani, wataharakisha kuingia ndani na kuwaweka chini ya ulinzi viongozi wa kundi hilo.
Baada ya waziri wa mambo ya ndani pamoja na maofisa hao wa vyeo vya juu vya polisi kuandaa mpango huo, walikubaliana kutumiana taarifa za matokeo ya zoezi hilo wakati huo wa usiku.
Mkuu wa jeshi la polisi na mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai waliporudi makao ya polisi, walianza kushughulikia zoezi hilo.
Polisi kumi na askari saba wa upelelezi walishirikishwa katika operesheni hiyo. Katika askari hao saba wa upelelezi, wawili waliandaliwa kuingia ndani ya jumba hilo wakijifanya kuwa wanachama.
Kuanzia saa kumi na moja jioni, askari wa upelelezi walianza kuzunguka karibu na jumba la Freemasons. Ilipofika saa moja, walianza kuona magari yakiingia katika geti la jumba hilo.
Magari hayo yaliingia kwa wingi, kama vile yanaingia katika klabu ya usiku, hali ambayo iliwapa ishara makachero hao kuwa watu hao walikuwa wakiendelea na shughuli zao kama ilivyodaiwa.
Mnamo saa moja na nusu, makachero hao walirudisha majibu kwa mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai.
“Tumegundua kuwa kuna harakati zinazoendelea. Watu hao watakuwa na mkutano bila shaka,” mmoja wa makachero hao alimwambia mkurugenzi wa upelelezi.
“Ni harakati gani mlizozigundua?”
“Kuanzia saa moja usiku, kulikuwa na magari mengi yaliyokuwa yanaingia katika jumba lao.”
“Hicho ndicho kitu tulichokuwa tunataka kujua. Sasa tutaendelea na mpango wetu kama tulivyopanga.”
Makachero wawili waliokuwa wameandaliwa kuingia katika jumba hilo waliitwa ofisini kwa mkurugenzi wa upelelezi, ambako kulifanyika kikao cha nusu saa. Mbali na makachero hao, pia alikuwepo mkuu wa kikosi cha polisi kilichopangwa kushiriki katika operesheni hiyo.
Mkuu huyo wa kikosi alipangiwa kwenda kusubiri karibu na jumba la Freemasons hadi atakapopigiwa simu na makachero watakaokuwa wameingia ndani ya jumba hilo. Kadhalika, makachero watakaokuwa ndani walitakiwa kumpigia simu mkuu wa kikosi hicho na kumfahamisha hatua za kuchukua.
“Kama hakutakuwa na mawasiliano yoyote kati yenu na wapelelezi watakaokuwa ndani, utasogeza magari kwenye geti la jumba hilo na mtawakamata viongozi wa kundi hilo,” mkurugenzi wa upelelezi alimwambia mkuu wa kikosi.
“Ni baada ya muda gani tutatakiwa tusogee kwenye geti la jumba hilo?” mkuu wa kikosi akamuuliza.
“Ni kuanzia saa tatu. Na ni endapo hakutakuwa na mawasiliano na wenzenu watakaokuwa ndani. Inawezekana wakawa wamebanwa.”
Mkurugenzi wa upelelezi akawatazama makachero wawili, Deo na Herman, waliokuwa wamepangiwa kuingia ndani ya jumba hilo.
“Nyinyi kazi yenu itakuwa kushuhudia kile kitakachokuwa kinafanyika mle ndani. Mtakuwa mashahidi wetu muhimu, lakini endapo mtagunduliwa, mtajitambulisha na kuwapigia simu wenzenu watakaokuwa nje,” mkurugenzi huyo aliwaambia makachero hao na kuongeza:
“Endapo kama watu hao hawatawaruhusu kupiga simu, hamtakuwa na sababu ya kuwa na wasiwasi, kwani wenzenu watakaokuwa nje wakiona kimya wataingia ndani.”
Ilikuwa saa mbili usiku wakati kachero Deo na mwenzake Herman walipokuwa ndani ya gari lenye namba za kiraia, wakikaribia geti la jumba la Freemasons.
Herman aliyekuwa kwenye usukani alitazama saa yake ya mkononi na kumwambia Deo:
“Ni saa mbili na dakika moja sasa.”
“Kama ni mkutano, watakuwa wameshaanza.”
“Lakini naamini hatujachelewa sana.”
Waliona gari lililokuwa likifunguliwa geti na kuingia ndani. Kabla ya geti hilo kufungwa, Herman naye aliliingiza gari hilo. Alitupa macho ndani ya ua wa jumba hilo na kugundua kuwa magari yalikuwa yanaegeshwa upande wa kushoto.
Gari lililokuwa limewatangulia lilikuwa limesimama. Herman alilipeleka gari na kuliegesha kando ya gari hilo.
Makachero hao hawakujua kuwa kila gari lililokuwa linaingia katika geti la jumba hilo lilikuwa linanaswa na kamera na kutazamwa katika chumba maalumu. Herman alizima gari, wakafungua milango na kushuka.
Mtu aliyeshuka kutoka kwenye gari lililowatangulia alikuwa akiingia kwenye lango la jumba hilo. Herman na Deo walimfuata kwa hatua za haraka.
Walifuatana na mtu huyo hadi katika ukumbi wa chini wa jumba hilo. Walikuta watu wengi waliokuwa wameketi kwenye viti. Makachero hao, wakijifanya kama wenyeji, walikwenda kuketi kwenye viti na kusubiri kuona kilichokuwa kinaendelea.
Hakukuwa na watu wowote walioonesha kuwajali, pengine kwa sababu haikuwa kawaida kwa mtu asiyehusika kujiingiza katika jumba hilo.
Osaka alifika baadaye na kuongoza kile kilichoonekana kuwa ni ibada. Kilichowashangaza makachero hao ni kivuli cha mtu aliyeketi kilichotokea katika kioo kilichokuwa mbele.
Walikuwa wakijiuliza, mtu yule alikuwa wapi na kwa nini hakujitokeza mwenyewe?
Mara tu baada ya kumaliza ibada zao, sauti nzito iliyotoka kwenye kioo ilimlaani Rais Shanga na kueleza kuwa wataendelea kupambana na utawala wake bila kujali vitisho vya serikali yake.
“Sisi ndiyo tuliomuweka kwa makubaliano maalumu ambayo ameyageuka,” sauti iliendelea kueleza na kuongeza:
“Paka hashindwi na utumbo wake!”
Herman na Deo walikuwa wakitazamana mara kwa mara waliposikia maneno yaliyokuwa yakimsakama Rais Shanga.
Walifahamu na kuamini kuwa kazi nzito ilikuwa inawasubiri, kwani watu hao walionekana kutotii serikali.
Wakati makachero hao wakiyatafakari maneno yaliyokuwa yakizungumzwa, walishitushwa walipoisikia ile sauti ikisema:
“Leo kuna sura mbili ngeni. Tungependa watu hao ambao wanajifahamu kuwa hawahusiki humu ndani wafike hapa mbele!”