Mauaji ya kutisha - Sehemu ya 20
UTANGULIZI
Amour alikuwa ameinamisha uso wake huku akiinua macho mara moja moja akiwatazama watu hao. Aliamini mengi yasiyo na ukweli yalikuwa yakizungumzwa mitaani na polisi kulaumiwa kutokana na kadhia ya kuuawa kwa watoto wa Almasi.
Kwa vile mazungumzo yale ya kulaumiwa polisi yalimkera aliinuka na kwenda kuosha mikono yake. Baada ya kulipa aliondoka kwenye mkahawa huo.
Wakati anajipakia kwenye gari lake alijiambia, hakuna watu ambao watafanya uhalifu daima bila kukamatwa. Kama hawatakamatwa ni kwa kipindi fulani tu cha kufanya uhalifu wao lakini ni lazima watu hao watakamatwa tu.
Alikaa kwenye siti ya gari akafunga mlango huku maneno ya yule mtu yakipita akilini mwake.
“Wao na serikali nani mwenye uwezo zaidi…”
Bila shaka yoyote serikali ndio yenye uwezo zaidi, alijiambia kabla ya kulipiga moto gari hilo na kuondoka.
Alipofika ofisini kwake akakutana na Anjela.
“Karibu ofisini,” alimkaribisha.
“Asante.”
SASA ENDELEA
“KAA kwenye kiti.”
Anjela alikaa.
“Unajisikiaje hali yako?” Amour alimuuliza huku akimtazama kwa makini.
“Sijambo.”
“Umetoka hospitalini asubuhi hii?”
“Ndiyo. Baba alikuja kunichukua.”
“Yuko wapi?”
“Nimemuacha kwenye gari.”
“Sawa. Sasa nilichokuitia hapa ni kwamba wewe ndiye shahidi muhimu wa tukio la kuuawa kwa yule kijana. Kwa hiyo nilikuwa ninahitaji kuandikisha maelezo yako.”
“Sawa.”
Amour alitoa faili ambalo alikuwa ameweka kumbukumbu za matukio ya kuuawa kwa watu wa familia ya Almasi. Alipachika karatasi mpya na kuandika jina la Anjela.
“Unaitwa Anjela nani?”
“Naitwa Anjela Thomas.”
“Una umri gani?”
“Miaka ishirini na minne.”
“Unafanya kazi?”
“Ndiyo”
“Unafanya kazi gani?”
“Mimi ni mwalimu wa kompyuta”
“Umefahamiana na marehemu tangu lini?”
“Unafika mwaka mmoja sasa?”
“Unafahamu kwamba kaka zake marehemu waliuawa?”
“Nafahamu.”
“Marehemu aliwahi kukueleza nini kuhusu kuuawa kwa ndugu zake hao?”
“Alinieleza kuwa wameuawa na majambazi.”
“Alikuwa anaamini kwamba ndugu zake waliuawa na majambazi?”
“Ndiyo.”
“Aliwahi kukutajia hao majambazi walikuwa wakivaa mavazi gani na wakoje?’
“Kusema kweli jinsi alivyokuwa akinieleza ni kama wale niliowaona jana.”
“Majambazi huwa wanaua mtu na kupora mali, kwanini wale majambazi wa jana hawakupora kitu?”
“Sijui ni kwanini lakini nafikiri labda ni kwa sababu niliwahi kupiga kelele.”
“Unahisi kama usingetokea na kupiga kelele, wangempora nini marehemu?”
Msichana akatikisa kichwa.
“Hapo siwezi kujua.”
“Kulikuwa na watu wengine kadhaa, unadhani ni kwanini watu hao walimfuata marehemu?”
“Mimi nadhani wale majambazi ndio wale wale waliowaua kaka zake. Wameamua kumuua na yeye.”
“Unadhani ni kwanini?”
“Sijui.”
“Tuendeleea na tukio la jana usiku, hebu nieleze nini kilitokea….?”
Anjela akaanza kulieleza tukio lilitokea usiku uliopita hadi Alex alipouawa na yeye kupotewa na fahamu.
Amour aliandikisha maelezo yake kisha akamwambia aweke saini. Anjela alipoweka saini alimwambia.
“Utaniachia namba yako ya simu, nitakapokuhitaji nitakuita.”
Mara tu Anjela alipomalizana na Inspekta Amour na kutoka ofisini mwake, Amour alifahamishwa kwamba Almasi alikuwa amefika hapo akiwa na mke wake na mtoto wao aliyeitwa Benjamin.
Amour alipowaruhusu waingie ofisini, watu hao waliingia wakiwa wamejaa machozi kuanzia Almasi, mke wake na mtoto wao Benjamin. Walikuwa wanalia.
“Inspekta! Mwanangu Alex ameuawa jana usiku na waliomuua ni watu wale wale waliowaua wenzake.” Almasi alimwambia Amour huku akilia.
“Ninazo taarifa. Nilifahamishwa usiku huo huo na hilo suala ninalishughulikia.” Amour aliwambia na kuongeza.
“Ninachowaomba muwe na subira.”
“Tuwe na subira hadi lini Inspekta? Mwanangu sasa amebaki mmoja na sina hakika ataishi hadi lini?”
“Una maana gani kuuliza kuwa ataishi hadi lini?”
“Nina maana kwamba kaka zake wote wameshauawa, sasa unadhani kuwa yeye ataachwa?”
“Kuna wakati mlituambia kwamba hao majambazi wamekamatwa. Matokeo yake tunaona watoto wanaendelea kuuawa na wauaji ni wale wale” Mke wa Almasi naye akakita msumari wa moto kwenye kidonda.
Ilibidi Amour ainuke kwenye kiti na kuzungumza akiwa amesimama.
“Ndiyo maana nikawambia muwe na subira. Polisi pia ni wanadamu si malaika. Tunafanya kazi zetu kwa kutumia uwezo wetu wa kibinaadamu. Hatuna miujiza na inaaminika kwamba hao wauaji wanatumia nguvu za kiza…”
“Inspekta unaingiza ushirikina….” Almasi alimkatiza. Akaongeza.
“Sisi tunaamini wale ni watu wa kawaida tu lakini tunashangaa ni kwanini hawakamatwi.”
“Mtoto wetu sasa amebaki huyu mmmoja, ndiyo tumekuja naye mumpe ulinzi.” Mke wa Almasi alikoleza moto.
Amour hakujua ajibu lipi na awatulize vipi watu hao ambao walikuwa wamemchachamalia kama vile yeye ndiye aliyekuwa muuaji wao.
Ilibidi awaite maafisa wenzake na kuzungumza na watu hao kwa utaratibu mpaka wakakubali kuwa suala hilo wawaachie polisi.
Almasi, mke wake na Benjamin wakasindikizwa na polisi hadi walipoliegesha gari lao. Wakajipakia na kuondoka.
Baada ya watu hao kuondoka, maafisa wa polisi waliweka kikao kulizungumzia suala la kuuawa kwa watu wa familia ya Almasi.
Kila afisa aliruuhusiwa kutoa mawazo yake kuhusiana na suala hilo na kueleza ni mkakati upi ambao ungefaa kutumika kuwakamata majambazi hao.
Polisi na makachero mbalimbali walitoa mawazo yao ya busara ambayo Inspekta Amour aliyaandika yakiwa kama mkakati wa kipolisi wa kuhakiksha mauaji ya watu wa familia ya Almasi yanakomeshwa na wauaji hao wanakamatwa.
**********
Baada ya maziko ya Alex, Almasi alimuweka kikao mwanawe aliyebaki ambaye alikuwa ni Benjamin pamoja na mke wake.
“Mke wangu na mwanangu Alex hivi sasa tumebaki peke yetu.” Almasi alimwambia mke wake na mwanawe katika kikao hicho.
Aliendelea kuwambia. “Sisikitikii Mungu kuchukua mtu wake aliyemtaka ila nasikitikia matukio yaliyowatokea wanangu. Wanangu wameuawa kinyama na wametolewa roho zao kikatili bila ya hatia. Na mpaka sasa sijatambua ni akina nani wanaonifanyia unyama huu.
“Jukumu lakuwalinda wananchi pamoja na mali zao ni la polisi lakini inaonekana polisi wameshindwa si tu kuzuia mauaji ya wanangu bali pia wameshindwa hata kuwatambua hawa watu ni kina nani. Kwa kweli inauma.
“Kwa vile sijui watu hawa wana lengo gani na mimi, ninakutahadharisha mwanangu Benjamin uwe makini sana. Ukitutoka wewe tutabaki wakiwa. Jana usiku nilikufikiria sana. Na mwisho wa fikira zangu niliamua ili kukulinda wewe nikuwekee mlinzi wa kukulinda wakati wote.
“Tutatafuta mlinzi hodari katika makampuni ya ulinzi, utakuwa ukitembea naye iwe kwenye gari au kwa miguu. Kadhalika nyumba yako itakuwa na walinzi kwa masaa ishirini na nne. Kama uwezo huo wa kukulinda ninao nitatumia pesa zangu kuhakikisha unabaki salama hadi hapo watu hawa watakapotambulika na kutiwa mikononi.
“Na yote hii ni wivu tu na kijicho cha binaadamu. Wameona nina mali, nina watoto, basi wameona waanze kuwaua na kunitia hasara ili nirudi kuwa masikini na nisiwe na mtoto lakini naamini kama kusudio lao ni hilo halitatimia.”
Alipofika hapo Almasi akamtazama Benjamin.
“Kweli unajhisi kuwa salama wakati kaka zako wameshaondoka?” akamuuliza.
Benjamin akatikisa kichwa.
“Hapana baba, sijisikii kuwa salama.”
“Kwa hiyo unakubaliana na miimi kwamba tukuwekee mlinzi?”
“Ninakubaliana na ndilo lililokuwa wazo langu.”
“Unadhani tutampata wapi mlinzi?”
“Kwenye makampuni ya ulinzi.”
“Sitaki awe na sare, nataka mlinzi ambaye atavaa kiraia ili asitambulike.”
“Hao walinzi wa makampuni pia wanaweza kuvaa kiraia.”
“Tukutafutie sisi au utamtafuta mwenyewe?”
“Nitamtafuta mwenyewe.”
“Sawa. Nataka mpaka kesho kutwa nimuone mlinzi huyo na mshahara wake nitaulipa mimi.”
“Sawa baba, nitajitahidi kumpata haraka iwezekanavyo.”
Almasi akamtazama mke wake. “Je una lolote la kusema?” Akamuuliza.
“Ninalo. Nataka nimwambie Benjamin ajifunze kutokana na yale yaliyomkuta mwenzake. Alex alikuwa akiishi maisha tofauti kabisa na mwenendo wetu sisi. Alex mbele ya macho yetu alikuwa mkimya sana lakini tumekuwa tukisikia kwamba alikuwa anakunywa pombe, anabadili wasichana kama mashati na anakesha kwenye vilabu hadi usiku wa manane.
“Tumeambiwa na daktari kwamba damu ya Alex ilionyesha kwamba alikuwa amelewa wakati anauawa. Pengine kama asingelewa angeweza kujihami au pengine kama usiku ule asingekwenda klabu asingekutana na mauti yale.
“Sasa nakuhadharisha wewe. Acha matembezi ya usiku na acha kujihusisha na makundi ya marafiki wasioeleweka. Umenielewa mwanangu?”
“Nimekuelewa mama. Nyinyi wenyewe mnanijua tangu zamani. Sina marafiki kama alivyokuwa Alex na muda mwingi nakuwa nyumbani tu,” Benjamin aliwaambia.