Mauaji ya kutisha - Sehemu ya 19
UTANGULIZI
Anjela alikuwa anatoka kujisaidia akawaona watu wamemshika mpenzi wake. Alimuona aliyekuwa ameshika upanga akimchinja Alex.
Anjela akapiga ukulele.
“Jamani watu wanamchinja mume wangu!”
Alirudia kusema hivyo mara tatu akiwa amesimama hatua kadhaa kutoka lilipokuwa gari la Alex. Wale watu watatu aliowaona waliondoka taratibu na hakuweza kujua walielekea wapi.
SASA ENDELEA
Alipoona watu hao wameondoka, Anjela alipiga hatua hadi lilipokuwa gari hilo akamtazama Alex aliyekuwa ameanguka kando ya gari baada ya kuchinjwa. Anjela alipoiona shingo ya Alex iliyokuwa imetapaa damu alipiga ukulele mwingine akaanguka chini na kupoteza fahamu.
Inspekta Amour aliamshwa usingizini kwa mlio wa simu aliyokuwa ameiweka kwenye kimeza cha mchagoni mwa kitanda.
Alikuwa akipendelea kuiweka simu yake mahali hapo ili aweze kuisikia kirahisi pindi inapoita wakati akiwa amelala.
Alipozinduka aliwasha taa akautoa mkono wake ndani ya chandarua na kuichukua simu hiyo.
Aliona namba ya mmoja wa makachero wa idara yake aliye chini yake, akaipokea simu.
“Afande kuna tukio limetokea usiku huu. Kuna kijana amechinjwa nje ya jumba moja la starehe usiku huu na inasemekana ni mtoto wa Bwana Almasi…”
Amour akashituka na kuuliza.
“Amechinjwa na nani?”
“Haijafahamika bado. Imeelezwa kuwa huyo kijana alikuwa na mchumba wake ambaye alipiga kelele kuita watu wakati Alex anachinjwa lakini watu walipofika walimkuta msichana huyo amepoteza fahamu.”
“Huyo msichana yuko wapi?”
“Amepelekwa hospitali ya Muhimbili.”
“Mpaka sasa hajazinduka?”
“Hajazinduka.”
“Hao watu waliomchiunja wamekamatwa?”
“Hawakupatikana. Waliwahi kukimbia.”
“Mwili wa huyo kijana umepelekwa wapi?”
“Pia umepelekwa hospitali ya Muhimbili.”
Baada ya kupata taarifa hiyo Amour hakulala tena. Alishuka kitandani akavaa nguo zake na kutoka. Alijipakia kwenye gari lake na kuelekea hospitali ya Muhimbili.
Alipofika alikwenda mochwari ambako aliomba kuoneshwa mwili wa kijana aliyechinjwa. Akatolewa mwili huo. Alipoutazama alithibitisha kuwa ni mwili wa Alex mtoto wa Almasi.
Amour akatikisa kichwa kusikitika.
“Wauaji hawa wamedhamiria nini?” Akajiuliza kimoyomoyo bila kupata jibu.
Baada ya kutoka mochwari, Amour aliomba apelekwe katika chumba alicholazwa msichana aliyezirai ambaye alikuwa pamoja na marehemu.
Alipopelekwa katika chumba hicho alikuta watu wanne, daktari aliyekuwa akimpima Anjela mapigo ya moyo, polisi wawili na mtu mwingine mmoja ambaye hakumfahamu.
Vile Amour anaingia tu katika chumba hicho, Anjela naye akafungua macho. Fahamu zilikuwa zinaanza kumjia. Kwanza alishituka kujiona yuko katika chumba hicho cha hospitali.
Kisha akashituka kuwaona watu wamesimama kando ya kitanda alicholazwa akiwemo daktari. Aliwapitishia macho watu hao na kugundua kuwa walikuwa polisi wawili na mtu mwingine alikuwa ni baba yake.
Alipomuona baba yake alimuita.
“Baba!”
“Ndiyo mwanangu” Mtu alliyekuwa amesimama na wale polisi akamuitikia.
“Kuna nini?”
“Utafahamu kila kitu. Ninakuomba utulie kidogo.” Daktari alimwambia Anjela.
“Nimefanya nini dokta?”
“Uko salama tu isipokuwa ulipoteza fahamu ulipokuwa mahali fulani. Tunafurahi kuwa umezinduka.”
Hapohapo kumbukumbu zikaanza kumjia Anjela. Alikumbuka kutoka na mpenzi wake Alex. Alikumbuka walivyokuwa katika ukumbi fulani na akakumbuka alipojisikia kupatwa na haja ndogo wakati walipokuwa wanatoka na Alex.
Baada ya hapo kumbukumbu zikaanza kumjia vizuri. Alikumbuka kumuacha Alex kwenye gari na kwenda kujisaidia kitendo ambacho kilichukua dakika tatu hivi. Akakumbuka wakati anatoka aliona watu wakimchinja Alex kwenye gari kisha akakumbuka kuuona mwili wa Alex uliokuwa umelala chini ukiwa umechinjwa!
Baada ya hapo hakukumbuka tena kilichoendelea. Lakini hata hivyo alitambua kuwa Alex alikuwa ameuawa. Huzuni zikaanza upya ndani ya moyo wake. Machozi yakaanza kumtiririka.
Amour alipoingia katika chumba hicho alisimama na kumtazama msichana huyo kisha akajitambulisha kwa daktari na kuomba kuzungumza na msichana huyo mawili, matatu.
Aliketi pemebeni mwa kitanda na kuanza kumhoji maswali Anjela.
“Unaitwa nani?”
“Naitwa Anjela Amin.”
“Una umri gani?”
“Nina mika ishirini na minne”
“Unamfahamu Alex?”
“Ndiyo namfahamu.”
“Hebu nieleze nini kimetokea?”
Msichana huyo akaeleza kilichotokea hadi alipopotewa na fahamu.
“Hao watu uliowaona wakimchunja marehemu uliwaona vizuri?’
“Sikuwaona vizuri lakini walikuwa watatu, wawili walivaa nguo nyeupe, mmoja alivaa nguo nyeusi na huyo ndiye aliyemchinja …”
Anjela alianza kulia kwa sauti.
“Usilie. Nyamaza uendelee kutueleza. Hao watu baada ya kufanya kitendo hicho walikwenda wapi?’
“Nilipotoka kujisaidia na kuwaona nilipiga kelele. Wakati huo ndio walikuwa wanamchinja. Walipoona napiga kelele wakaondoka.”
“Walipoondoka walikwenda wapi?”
“Sikuweza kuzingatia walikwenda wapi lakini waliondoka ghafla.”
“Uliona wanaondoka au walitoweka mbele ya macho yako?”
“Pale kwenye gari waliondoka halafu sikuwaona tena.”
“Walikupotea?”
“Ndiyo.”
“Wakati unaletwa hapa hospitali ulikuwa umepoteza fahamu?”
“Ndiyo.”
Amour akawatazama wale polisi.
“Gari lao liko wapi?” Akawauliza.
“Gari lao limeondolewa. Lipo makao ya polisi.” Polisi mmoja akamjibu.
“Sawa.”
Amour akamtazama yule mtu mwingine aliyekuwa amesimama.
“Wewe ndiye baba wa huyu binti?” Akamuuliza.
“Ndiye mimi?” Yule mtu alimjibu kwa haraka.
“Wakati tukio hili linatokea ulikuwa wapi?”
“Nilikuwa nyumbani. Nilipigiwa simu nikaamshwa usingizini. Kuna mtu aliniambia binti yako ameuawa. Nikafika hapa na kuambiwa kwamba aliyeuawa ni mwenzake. Kwa kweli ni jambo ambalo limenisikitisha sana.”
“Tutawatafuta wauaji hao na ninaamini kuwa tutawapata tu.”
Amour akainuka na kumtazama Anjela.
“Utakapotoka hospitali nataka uripoti ofisini kwangu makao ya polisi. Uliza Inspekta Amour.”
“Sawa. Nitafanya hivyo.”
Baada ya hapo Inspekta Amour aliaga na kuondoka. Hakurudi tena nyumbani kwake. Alikwenda ofisini kwake makao ya polisi. Muda huo wa usiku harakati za kazi zilikuwa zikiendelea ndani ya makao ya polisi kama vile ulikuwa mchana.
Makachero na polisi waliokuwa na zamu ya usiku na wale ambao hawakuwa na zamu maalum kama Inspekta Amour, walikuwa wakiendelea na kazi.
Amour alipoingia ofisini kwake aliendelea na kazi zake hadi saa kumi na mbili asubuhi ambapo aliondoka kurudi nyumbani kwake. Alipofika alioga na kubadili nguo kisha alitoka tena. Alikwenda kwenye mkahawa kunywa supu.
Wakati anakunywa aliwasikia watu waliokuwa wamekaa karibu na meza yake wakiongelea kuhusu mauaji yaliyotokea usiku uliopita.
Amour alishangaa jinsi watu wa jiji hilo walivyokuwa wadaku wa kupata mambo kwa haraka. Tukio lilitokea usiku lakini tayari lilikuwa linazungumzwa kama vile lilitokea asubuhi ile.
Hata hivyo watu hao hawakuwa wakilizungumzia tukio hilo kwa usahihi. Habari ilikuwa imepotoshwa sana. Walisema kijana mmoja pamoja na mpenzi wake waliuawa kwa kuchinjwa na gari lao kuporwa.
Kilichomchoma Amour ni kusikia kuwa watu waliofanya tukio hilo ni majambazi ambao walikuwa wameiandama familia ya tajiri mmoja aliyefahamika kwa jina la Almasi.
“Majambazi hao wameshaua watoto wengi wa tajiri huyo akiwemo huyo aliyechinjwa usiku.” Mtu mmoja aliwambia wenzake.
“Sasa ni kwanini wameiandama familia hiyo?” Mtu mwingine akauliza.
“Haijulikani. Wakati mwingine wanawaua bila kuchukua kitu chochote.”
“Tuseme polisi bado hawajawagundua watu hao?”
“Inaelekea polisi wameshindwa kuwapata. Inasemekana hao watu wanatumia uchawi ili wasikamatwe.”
“Basi watawamaliza.”
“Huyo tajiri mwenyewe anawalaumu polisi. Anawambia majambazi wote wanakamatwa, kwanini hao hawakamatwi. Wao na serikali nani mwenye uwezo zaidi?”
Amour alikuwa ameinamisha uso wake huku akiinua macho mara moja moja akiwatazama watu hao. Aliamini mengi yasiyo na ukweli yalikuwa yakizungumzwa mitaani na polisi kulaumiwa kutokana na kadhia ya kuuawa kwa watoto wa Almasi.
Kwa vile mazungumzo yale ya kulaumiwa polisi yalimkera aliinuka na kwenda kuosha mikono yake. Baada ya kulipa aliondoka kwenye mkahawa huo.
Wakati anajipakia kwenye gari lake alijiambia, hakuna watu ambao watafanya uhalifu daima bila kukamatwa. Kama hawatakamatwa ni kwa kipindi fulani tu cha kufanya uhalifu wao lakini ni lazima watu hao watakamatwa tu.
Alikaa kwenye siti ya gari akafunga mlango huku maneno ya yule mtu yakipita akilini mwake.
“Wao na serikali nani mwenye uwezo zaidi…”
Bila shaka yoyote serikali ndio yenye uwezo zaidi, alijiambia kabla ya kulipiga moto gari hilo na kuondoka.
Alipofika ofisini kwake akakutana na Anjela.
“Karibu ofisini,” alimkaribisha.
“Asante.”