Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mauaji ya kutisha - Sehemu ya 16

MAUAJI 16 Pict

UTANGULIZI

“Nilihitaji  malezo kwa ufupi, hebu niambie nini kilitokea?”

Amour akaelezwa kilichokuwa  kimetokea.

“Hao watu walikuwa wamevaa nguo za  rangi gani?” Akauliza.

“Mmoja alivaa nguo za  rangi nyeusi,  wengine wawili walivaa nguo za rangi nyeupe.”

Hapo hapo Amour akaamini  kwamba wauaji  walikuwa ni wale wale waliokuwa wakiwaua watoto wa Almasi.

“Huyo aliyevaa nguo nyeusi yukoje?” Amour aliendelea kuuliza.

“Kusema ukweli hatukuwaona  vizuri.”

SASA ENDELEA...



“Namfananisha na mtu mmoja ambaye anaonekana kama vile shingo yake imechinjwa.”

“Kusema kweli huyo mtu ndivyo alivyokuwa akionekana. Kichwa chake kilikuwa kinaning’inia.”

Hao ndio wauaji wale  wale wa watoto wa Almasi! Amour akajiambia kimoyomoyo.

Alijiambia kudhani kwake kuwa alikuwa amewakamata majambazi hao kulikuwa sivyo kabisa.  Aliowakamata walikuwa majambazi wengine.

Amour akajiuliza atakwenda kumueleza nini Mkurugenzi wa Upelelezi kuhusiana na kuuawa kwa kijana huyo?

Alijiuliza hivyo baada ya kufahamu kuwa alishamueleza kuwa majambazi waliokuwa wameiandama familia ya Almasi alikuwa amewakamata na wengine kuwaua.

“Lakini yule mganga alikiri kuwapa dawa za uchawi majambazi wale!” Amour alikuwa akiendelea kusema na moyo wake.

Wakati huo akizungumza na polisi wa benki kwenye simu alikuwa amenyamaza kidogo akitafakari.

“Natumaini umenielewa afande?” Sauti ya upande wa pili wa simu ikamuuliza Amour.

“Nimekuelewa isipokuwa muhakikishe kuwa kesho  mnafika hapa kuandikisha maelezo yenu.”

Amour alikata simu na kumtazama mkuu wa kituo cha polisi cha Chalinze ambaye naye alikuwa akimtazama.

“Kama hawa askari watakuja hapa Chalinze kesho hakikisha unaandikisha maelezo yao na kisha uniletee ofisini kwangu,” akamwambia.

“Nitafanya hivyo.”

Ndipo Amour na makachero wenzake walipoanza ,msafara wa  kurudi Dar wakiwa na mwili wa John. Gari la John halikuachwa Chalinze. Kulikuwa na polisi  mmoja aliyeliendesha kulipeleka Dar.

Walipofika Dar es Salaam mwili wa John ulipelekwa hospitali ya Muhimbili. Gari la marehemu liliachwa katika eneo la kuegesha la makao ya polisi.

Baada ya kuupeleka mwili wa John hospitalini Amour alirudi ofisini kwake na kumpigia simu mzee Almasi.

“Inspekata habari yako?” Sauti ya Almasi ikasikika kwa uchangamfu mara tu simu ilipopokelewa.

“Nzuri Bwana Almasi. Uko wapi?”

“Hapa niko ofisini Mikocheni. Kuna  tatizo lolote?”

“Ninakuhitaji ofisini kwangu.”

“Nije ofisini kwako?”

“Ndiyo. Kuna tatizo limetokea.”

“Tatizo gani tena. Mwanangu ameenda Arusha kwenye mkutano. Kulikuwa na kazi ameziacha, ninazimalizia.”

Amour aliposikia kauli hiyo aligutuka na kumuuliza.

“Mwanao gani aliyekwenda Arusha?”

“John. Ameondoka asubuhi kwenda Arusha, kwa hiyo imebidi nimshikie ofisi yake hadi atakaporudi.”

“Sawa, sasa acha kazi uliyonayo uje mara moja, kuna kitu muhimu.”

“Sawa. Ninakuja.”

Amour akakata simu huku akijua kuwa John aliyemtaja Almasi ndiye yule aliyeuawa.

Alijiuliza atawezaje kumueleza baba yake kuwa mwanawe ameuawa njiani wakati akielekea huko Arusha?

Aliogopa kwamba angemshitua kumjulisha kuwa mwanawe huyo ameuawa. Lakini pia kauli yake ingemsuta mwenyewe kwa sababu alishamhakikishia Almasi kuwa wauaji wa watoto wake alishawakamata.

Amour alitikisa kichwa peke yake kusikitika.

Almasi aliondoka  ofisini  akiwa hajui kilichotokea. Alijipakia kwenye gari lake akaondoka kuelekea makao ya polisi.

Wakati analiegesha gari kwenye eneo la kuegesha la makao ya polisi alishituka allipoliona gari la ,mwanawe John likiwa limeegeshwa mahali hapo.

Aliposhuka  kwenye  gari alikwenda kuliangalia vizuri akahakikisha lilikuwa ni gari na mwanawe John ambalo aliondoka  nalo asubuhi kuelekea Arusha.

“Limefikaje hapa?” Akajiuliza.

“John  mwenyewe yuko wapi?” Akaendelea kujiuliza  bila  kupata  jibu.

Alipogeuka nyuma alimuona polisi mmoja akiwa na hamsini zake, akamuita.

Polisi  huyo  alipofika  alimuuliza.

“Hili gari la mwanangu, limefikaje hapa?”

“Nenda ukawaulize wanaohusika humo ndani.” Ndilo lililokuwa jibu la polisi huyo.

Almasi akawa ameanza kuchanganyikiwa. Baada ya kusita sita kwa sekunde kadhaa akilitazama gari hilo, aliondoka kuelekea ofisini kwa Inspekta  Amour.

“Karibu kiti.” Amour alimwambia mara tu alipomuona akiingia ofisini kwake.

Almasi hakukaa kwenye kiti.

“Nimeona gari la mwanangu John hapo nje, kumetokea nini? Na John  mwenyewe yuko wapi?”

“Kaa kwenye kiti. Nimekuita kukueleza matatizo ya mwanao John. Naomba unisikize kwa makini.”

Almasi alikaa lakini alikuwa ameshakosa amani.

Amour alianza kumueleza jinsi alivyopigiwa simu kutoka  kwa mkuu wa kituo cha polisi  cha  Chalinze na kuarifiwa kuhusu mtu aliyeuawa huko  Wami.

“Tulifika Chalinze tukaouona mwili  wa mtu huyo ambao ulikuwa umeshafikishwa hospitalini. Tuliona pia na gari lake. Nikagundua kuwa mwili huo  ulikuwa ni wa John pamoja na hilo gari uliloliona hapo  nje.”

Uso wa  Almasi ulianza kubadilika rangi. Mwanzo  ulikuwa  mweusi sasa ukawa mwekundu.

“Tulivyoelezwa na polisi  ni kwamba gari la John lilipata pancha lilipofika  Wami. John akalisimamisha pemebeni mwa  barabara na kudadili tairi lakini hapo hapo  walitokea watu ambao walimchinja na kutoweka.” Amour alinyamaza akamtazama Almasi kuona  jinsi alivyokuwa akiyapokea maelezo yake.

“Unataka uniambbie kuwa mwanangu John  naye amechinjwa?” Almasi akauliza kwa sauti ambayo haikuwa  tulivu  hata chembe.

“Ukweli ndio  huo na inabidi tukueleze kilichotokea. Kulikuwa na polisi  wawili  waliokuwa  katika gari  jingine ambao waliona hilo tukio. Lakini waliposimamisha gari ili kutoa  msaada, watu hao walitoweka ghafla.”

“Hao wauaji ni kina nani?”

“Hatujawafahamu na tunaendelea na uchunguzi.”

“Inspekata uliniambia kuwa umeyakomesha mauaji ya watoto wangu  na  kwamba majambazi waliohusika umeshawakamata!”

“Tunafanya uchunguzi kujua kama wauaji ni wale wale au ni wengine.”

“Haiwezekani wawe ni wale wale wakati ulishawakamata.”

“Ndio tunafanya uchunguzi ili tuweze kujua. Tukio lenyewe limetokea mbali. Tumefanya kuarifiwa na polisi  wenzetu. Kesho tunatarajia polisi  walioshuhudia tukio hilo watafika hapa  ili tuweze kuwahoji.”

“Unajua sielewi chochote unachonieleza. Nataka kwanza niuone mwili wa mwanangu, John uko  wapi?”

“Uko hospitali ya Muhimbili.”

“Naomba kwenda kuuona.”

Dakika  chache baadaye,  Amour na Almasi wakiwa katika magari  tofauti walikuwa njiani kuelekea hospitali ya Muhimbili.

Amour alikuwa akiendesha kwa umakini lakini  haikuwa hivyo  kwa Almasi ambaye taharuki lilimfanya atetemeke mwili  mzima. Presha ilikuwa juu na alikuwa akifoka peke yake akimlaumu Inspekta Amour.

Walipofika  Muhimbili walikwenda mochwari ambapo  walitolewa mwili wa John. Almasi aliuona akaangua kilio.

Alitoa kitambaa akaufuta uso  wake kisha kwa macho yaliyokuwa  mekundu alimtazama Amour.

“Unanieleza nini kuhusu kuuawa kwa mwanangu?” Akamuuliza.

“Tutatoa taarifa yetu baada ya uchunguzi wetu kukamilika.”

“Ni kwanini watoto  wangu wanauawa ovyo?. Huo  uchunguzi wenu utakamilika lini?”

“Jaribu kutuliza hasira mzee wangu. Sisi pia tunasikitika kuona watu wetu wanauawa kila siku na tunahangaika usiku na mchana kuhakikisha usalama wa watu wetu….”

“Lakini wewe hushangai kuona  watoto wangu wanaandamwa namna hii? Mtu alikuwa anaenda safari anafuatwa na kuuawa bila sababu. Kama walitaka pesa au gari si wangechukua tu na  kumuacha mwanangu! Ukatili gani huu?”

Amour alitikisa kichwa.

“Umeouona mwili wa mwanao, naomba turudi ofisini.” alimwambia Almasi aliyeonekana kuchanganyikiwa.

Waliporudi tena ofisini, Amour  alimuuliza Almasi  kama  marehemu alikuwa na kiasi chochote cha pesa ndani ya gari.

“Alikuwa amechukua pesa za matumizi yake tu akiwa  huko Arusha. Hakuwa amechukua pesa nyingi. Sijui  walimuua kwa  sababu gani?”

“Sisi tulikuta shilinggi milioni moja kwenye mifuko yake pamoja  na  vitu vyake  vingine ambavyo tutakukabidhi.”

“Shilingi  milioni mmoja  zitanisaidia nini  mimi wakati roho ya mwanangu imeshatoka, amelala  kama walivyolala kaka  zake.” Almasi alisema kisha  alitoa kitambaa na kuufuta uso wake uliokuwa umetota.

Amour aliona alikuwa amekabiliwa  na wakati  mgumu kuelewana na mtu huyo wakati ule.

Alijiambia alipaswa amruhusu aende zake kisha amuite wakati  mwingine atakapokuwa ametulizana na kuzungumza naye.

“Sasa mzee Almasi unaweza kurudi nyumbani ukatoe taarifa kwa ndugu na jamaa. Nadhani baada ya maziko nitakuita tena.” Amour alimwambia Almasi.

Almasi aliinuka kwenye kiti huku akilia kama mtoto mdogo. Kitambaa kilikuwa kwenye uso wake. Amour alimbembeleza na kutoka  naye ofisini.  Alimuagiza polisi mmoja amsindikize hadi nyumbani kwake.

Aliporudi tena ofisini kwake simu yake  ikaita.  Alipotazama  namba inayompigia akaona namba za Mkurugenzi wa Upelelezi.

Akajua kuwa bosi wake alikuwa anampigia baada ya kupata taarifa ya mauaji ya mtoto mwingine wa Almasi.

Siku chache tu zilizopita, Amour alimwambia bosi wake huyo kuwa aliwakamata watu waliokuwa  wakiwaua  watoto  wa Almasi na bosi huyo aliamini kuwa tatizo hilo lilikuwa limekwisha.