Mauaji ya kutisha - Sehemu ya 15
UTANGULIZI
Alikaza nati ya kwanza kisha akaanza nati ya pili. Wakati anaitia spana kwenye nati ya tatu akahisi kitu chenye makali kikimtekenya shingoni mwake. Akashituka na kugeuza uso. Akamuona mtu aliyekuwa amevaa mavazi meusi nyuma yake akiwa amemshikia panga lililokuwa limesogezwa kabisa kwenye shingo yake. Cha kutisha zaidi ni kuwa shingo ya mtu huyo ilikuwa imechinjwa na kufanya kichwa chake kiwe kinaning’inia kama kilichotaka kuanguka!
Upande wa kulia na wa kushoto wa mtu huyo kulikuwa na watu wengine wawili waliovaa mavazi meupe.
SASA ENDELEA...
Hapo hapo ile picha ya mauaji ya kaka zake Martin na James ikamjia akilini. Wauaji wao walielezwa kuwa walikuwa watatu kama wale waliokuwa pale. Mmoja alikuwa amevaa mavazi meusi na wengine wawili walivaa mavazi meupe.
Kwa jinsi allivyoshituka na kugwaya, John alishindwa hata kuwauliza wale watu walikuwa kina nani na walitaka nini lakini akilini mwake alikumbuka kwamba watu hao walikuwa majambazi na walishakamatwa na wengine kuuawa.
Umbali wa kilometa moja hivi kulikuwa na gari la benki lililokuwa linakuja kutoka Dar likiwa na pesa za benki. Lilikuwa na maafisa wawili wa benki ya Handeni pamoja na polisi wawili waliokuwa na bunduki.
Kwa vile barabara ilikuwa imenyooka, waliliona gari la John lililokuwa limepata pancha likiwa pembeni mwa barabara. Walimuona pia John aliyekuwa akibadili tairi.
Lakini ghafla waliwaona watu watatu, wawili wakiwa na mavazi meupe na mmoja akiwa na mavazi meusi ambao walimvamia John. Aliyevaa mavazi meusi alikuwa ameshika upanga.
“Wewe ni mtoto wa Almasi?” Mtu aliyekuwa amevaa mavazi meusi ambaye kichwa chake kilikuwa kinaning’inia alimuuliza John.
“Ndiyo. Mimi ni mtoto wa Almasi.” John alijibu haraka na kwa kubabaika kama vile alihisi akikubali kuwa yeye ni mtoto wa Almasi angesalimika.
Gari la benki llilikuwa limeshafika karibu.
“Baba yako alikuweka kama dhamana na wewe umeshindwa kutimiza masharti ya dhamna yako…” Mtu huyo aliendelea kumwambia John.
“Dhamana gani?” John akauliza akiwa amemkazia macho mtu huyo aliyekuwa akitisha.
“Huwezi kupata jibu kwa sababu muda wako wa kuishi umeshakwisha!”
“Yesu wangu…!”
Hapo hapo upanga ukapita kwenye shingo ya John. Koo lilikatwa, damu ikamwagika kama maji ya bomba. Martin akarudi chini taratibu akiwa maiti.
Gari la benki liliwapita kabla ya kusimama. Wale polisi waliokuwa na bunduki walishuka haraka. Walipotupa macho hawakuwaona tena wale watu watatu bali walimuona John akiwa amelala chini huku damu ikimtoka shingoni.
Polisi hao walitupa macho kila upande kuwaangalia watu hao lakini hawakuwaona tena.
Polisi mmoja akasogea pale ilipokuwa maiti ya John na kugundua kuwa John alikuwa amechinjwa na tayari alikuwa ameshakufa akarudi na kumfahamisha polisi mwenzake pamoja na wale maafisa wa benki.
“Kwa hiyo wale watakuwa majambazi?” Mmoja wa maafisa hao wa benki akamuuliza.
“Watakuwa ni majambazi. Wamemchinja yule kijana kisha wamekimbia.”
“Sasa walitaka nini? Walitaka kuiba lile gari?” Afisa mwingine wa benki akauliza.
“Inawezekana walimuua ili waibe gari au pesa lakini walipotuona sisi wakakimbia.”
“Wamemchinja kabisa?”
“Wamemchinja na ameshakufa.”
“Sasa tufanyeje?”
“Tuwaarifu polisi wenzetu wa Chalinze waje hapa mara moja halafu sisi tuendelee na safari yetu. Au mnaonaje?”
“Ni sawa. Tutasubiri kidogo. Aliyeuawa ni binaadamu mwenzetu.” Afisa mmoja wa benki alisema.
Polisi huyo akatoa simu na kuwapigia polisi wa Chalinze.
“Kuna tukio la mauaji limetokea hapa mbele ya daraja la Wami” Polisi huyo alimwambia mkuu wa kituo cha polisi cha Chalinze baada ya kujitambulisha.
Akaongeza “Tulikuwa tunatokea Dar tukisindikiza pesa za benki kuelekea Handeni, tukalishuhudia tukio hilo likitokea mbele yetu.”
“Sasa nani ameuawa na ilikuwaje?” Mkuu wa kituo hicho akauliza kwa sauti ya taharuki.
Polisi huyo akamueleza tukio hilo lilivyotokea.
“Umesema mtu huyo amechinjwa na wachinjaji hao wamekimbia?”
“Amechinjwa na bado tuko naye hapa. Hao wachinjaji walikimbia baada ya kkutuona sisi.”
“Kwa hiyo mlishuhudia hilo tukio?”
“Ndiyo tulilishuhudia.”
“Na bado mko katika eneo hilo?”
“Bado tupo hapa. Tunawaomba mfike haraka ili tuweze kuendelea na safari.”
Pakatokea ukimya kidogo upande wa mkuuu wa kituo cha polisi cha Chalinze.
“Nadhani umenielewa afande?” Polisi huyo aliyepiga simu akauliza.
“Nimekuelewa.”
“Sasa naomba mfike haraka. Unajua tuna fedha za benki na tupo mahali pa hatari!”
“Sawa. Tunakuja.”
Dakika kadhaa baadaye gari la polisi kutoka Chalinze likawasili mahali hapo. Lilikuwa na polisi sita, watatu wakiwa na bunduki. Waliposhuka kwenye gari walikutana na polisi wenzao ambao walikwenda kuwaonesha maiti ya John.
“Mtu mwenyewe ni huyu hapa.” Polisi mmoja wa benki akawambia polisi hao.
“Loh…amechinjwa kweli!” Mkuu wa kituo cha polisi cha Chalinze ambaye alikuwemo kwenye msafara huo wa polisi alimaka baada ya kuiona maiti hiyo.
“Tunadhani kwamba gari lake lilipata panchari na alikuwa amebadili tairi ya gari kabla ya kuvamiwa na watu hao.” Polisi wa benki aliendelea kueleza.
“Hao watu walikimbillia upande gani?” Mkuu huyo wa kituo akauliza.
“Hatukuwaona upande waliokimbilia.”
“Si mliniambia kuwa mlilishuhudia tukio la kuuawa kwake?”
“Tulilishuhudia tukiwa kwenye gari lakini tuliposimamisha gari hao watu hatukuwaona.”
Polisi hao wa kituo cha Chalinze wakaanza uchunguzi. Walilikagua lile gari huku wengine wakiukagua mwili wa John pamoja na kumpekua.
Walikuta hati kadhaa ndani ya gari na pia walipata kitambulisho cha John pamoja na fehda zilizokuwa mfukoni mwake na kwenye mkoba wake uliokuwa ndani ya gari.
“Kwa vile nyinyi ndio mashahidi pekee wa tukio hili ningependa kupata majina yenu.” Mkuu huyo wa kituo aliwambia.
Baada ya kuandikisha majina ya polisi walioshuhudia tukio hilo pamoja na namba zao za simu, waliandikisha pia majina ya wale maafisa wa benki pamoja na namba zao.
“Sasa pelekeni pesa ila ninawaomba kesho mfike kituoni kwetu Chalinze muandikishe maelezo yenu.”
Baada ya kukubaliana hivyo polisi waliokuwa wakisindikiza pesa za benki waliondoka.
Polisi wa kituo cha Challinze waliubeba mwili wa John na kuupakia kwenye gari lao kisha wakabadili ile tairi iliyopata panchari. Baada ya kuweka tairi nyingine wakaliwasha gari la John. Gari hilo lilipowaka wakaondoka nalo.
Kitambulisho kilichopatikana mfukoni mwa John kilionesha kwamba alikuwa mkazi wa dar es Salaam na meneja wa kiwanda cha maji safi cha Almasi.
Walipofika Chalinze, polisi hao waliupeleka mwili wa John hospitali kisha wakawapigia simu polisi wa Dar es Salaam na kuwaarifu kuhusu tukio hilo.
Baada ya kupata habari kuwa kitambulisho cha mtu aliyeuawa huko Wami kina jina la John Almasi, mkazi wa Dar es Salaam na meneja wa kiwanda cha maji safi cha Almasi, haraka Inspekta Amour pamoja na polisi wengine wanne waliondokana gari kwenda Chalinze.
Walipofika walipelekwa hospitali ambako mwili wa John ulikuwa umehifadhiwa.
Alipouona tu mwili huo, Amour akautambua kuwa ulikuwa mwili wa mmoja wa watoto wa Almasi kwani alikuwa akiwafahamu.
Kitendo cha kumshuhudia mmoja wa watoto wa Almasi akiwa amechinjwa kilimshitua. Ingawa mara kwa mara alikuwa amezoea kuwashuhudia watu waliouawa, kwa mtoto wa Almasi mshituko wake ulikuwa mkubwa.
Si kwa sababu tu alikuwa amechinjwa bali kabla ya tukio hilo alikuwa akiamini kwamba alikuwa ameyatokomeza mauaji ya kikatili yaliyoiandama familia ya Almasi baada ya kuwakamata majambazi aliohisi kuwa ndio waliokuwa wakiendesha mauaji hayo..
“Ninamfahamu ni mtoto wa Bwana mmoja mwenye kiwanda cha maji safi anayefahamika kwa jina la Almasi huko Dar.” Amour alimwambia mkuu wa kituo cha polisi cha Chalinze kabla ya kumuuliza.
“Kuna maelezo uliyopata kuhusu kuuawa kwake?”
“Sisi tuliarifiwa na polisi wenzetu waliokuwa wakisindikiza pesa za benki wilaya ya Handeni. Tulipokwenda kuuchukua mwili huo pamoja na gari la marehemu, tuliwambia wafike kesho kuandikisha maelezo yao.”
“Ningehitaji nipate maelezo hata hii leo. Umechukua namba zao za simu?”
“Namba zao ninazo.”
“Nipatie.”
“Zipo ofisini.”
“Twende ukanipatie. Ninazihitaji.”
Walikwenda kituoni hapo ambapo Amour alikaa ofisini mwa mkuu wa kituo hicho na kupatiwa namba za simu za polisi walioshuhudia tukio hilo.
Mara tu alipopewa namba hizo, Amour alimpigia polisi mmojawapo.
“Unazungumza na Inspekta Amour wa makao ya polisi jijini Dar lakini kwa sasa niko Chalinze. Tumepata taarifa ya mauaji yaliyotokea hapo Wami na tumeambiwa kuwa wewe na polisi mwenzako mlishuhudia tukio hilo wakati mkiwa kwenye gari mkielekea Handeni.”
“Ndiyo afande tulishuhudia.”
“Nilihitaji malezo kwa ufupi, hebu niambie nini kilitokea?”
Amour akaelezwa kilichokuwa kimetokea.
“Hao watu walikuwa wamevaa nguo za rangi gani?” Akauliza.
“Mmoja alivaa nguo za rangi nyeusi, wengine wawili walivaa nguo za rangi nyeupe.”
Hapo hapo Amour akaamini kwamba wauaji walikuwa ni wale wale waliokuwa wakiwaua watoto wa Almasi.
“Huyo aliyevaa nguo nyeusi yukoje?” Amour aliendelea kuuliza.
“Kusema ukweli hatukuwaona vizuri.”