Mauaji ya kutisha - Sehemu ya 14
UTANGULIZI
“Yule mganga alikuwa anawapa dawa ili wanapofanya ujambazi wasikamatwe na polisi.”
“Alikuwa anawapa na dawa gani nyingine?’
“Ni hizo hizo tu za kufanikisha ujambazi wao.”
“Huyo mganga unamfahamu vizuri?”
“Ndiyo namfahamu.”
“Ukimuona unaweza kumtambua?”
“Ndiyo naweza kumtambua.”
“Sawa. Hebu mtazame yule mtu aliyekaa pale chini.”
Amour alimuonesha yule mganga kisha akamuuliza.
“Unamjua yule?”
Mwanamke huyo baada ya kumtazama mganga huyo alisema.
“Ndiyo namjua.”
SASA ENDELEA...
“NI nani?”
“Ndiye huyo mganga uliyekuwa unaniambia.”
“Ndiye yeye aliyekuwa akiwapa dawa za uchawi?”
“Ndiyo.”
Amour akamuita yule mganga.
“Hebu simama uje hapa.”
Mganga akainuka na kusogea kwenye meza.
“Unasema ulikuwa huwapi dawa za uchawi?” Amour akamuuliza.
Kabla ya mganga huyo kujibu mwanamke huyo alidakia.
“Alikuwa akiwapa hizo dawa. Siku nyingine alikuwa akiwaagiza mbuzi. Kuna siku aliwaagiza mafuta ya nguruwe na pua ya nguruwe ili awatengezee dawa wasikamatwe na polisi.”
“Alikuwa akiwambia wavae nguo gani wakati wakienda kufanya ujambazi wao?” Amour akaendelea kumuuliza.
“Sijui. Wakati akizungumza nao walikuwa wanaingia katika chumba kingine.”
Amour akayapeleka macho yake kwa mganga huyo.
“Walikuwa wanakulipa shilingi ngapi?” Akamuuliza.
Mganga hakujibu. Alikuwa ametahayari.
“Walikuwa wanamlipa shilingi milioni moja. Siku nyingine milioni mbili.” mwanamke akasema.
“Ulikuwa unakataa, sasa unasikia maneno hayo?” Amour akamuuliza mganga huyo aliyekuwa ameinamisha kichwa chake chini.
“Kama ni kweli nilikuwa nawapa dawa wasikamatwe mbona wamekamatwa?” Sauti ya mganga huyo ikasikika kwa mbali.
“Usiulize mbona wamekamatwa, hata wewe mganga mwenyewe pia umekamatwa!” Amour akamwambia.
Mganga akabaki amemkodolea macho Amour.
Dakika chache baadaye Inspekta huyo aliwasili ofisini mwa Mkurugenzi wa Upelelezi akiwa na nguvu.
“Afande napenda kukufahamisha kuwa wale majambazi tumewakamata jana usiku,” akamwambia.
“Unakusudia wale mliokuwa mnawatafuta?”
“Ndiyo afande. Na ni wale waliohusika na mauaji ya watoto wa Almasi.”
“Una ushahidi unaoonesha kuwa ni wao?”
“Ninao. Imebainika sasa kuwa walikuwa wanatumia uchawi, hata mganga wao tumemkamata. Ni mganga wa Bagamoyo na amekiri kuwa alikuwa anawapa dawa kwa ajili ya kufanya vitendo vya ujambazi.”
“Vizuri sana. Umefanya kazi nzuri. Mliwakamata wapi?”
“Tuliwakamata Buguruni jana usiku. Tuliwavamia katika nyumba waliyokuwa wanaishi. Katika majibizano ya risasi askari wetu wawili walipoteza maisha na majambazi watatu waliuawa. Majambazi wengine wawili tuliwajeruhi kwa risasi, wanatibiwa hospitalini.”
“Kwa jumla walikuwa majambazi wangapi?”
“Walikuwa watano. Tumewaua watatu.”
“Wameeleza wamehusika katika matukio mangapi ya ujambazi?”
“Kwanza ni yale matukio yanayowahusu watoto wa Almasi na matukio mengine. Bado tunaendelea kuwahoji. Tuliwakamata pia wasichana zao watatu. Mmoja aliuawa kwa risasi.”
“Sasa mkikamilisha uchunguzi wenu wafikisheni mahakamani haraka ili wananchi wajenge imani na jeshi lapolisi.
Uhalifu unapokuwa mwingi wananchi wanakosa imani na jeshi letu na tunapata lawama nyingi kutoka kwa viongozi wetu.” Mkurugenzi wa Upelelezi alimwambia Inspekta Amour.
“Naamini wiki hii hii tutawafikisha mahakamani pamoja na yule mganga wao aliyekuwa akiwapa dawa za uchawi.”
“Na yeye amekiri kwamba alikuwa akiwafanyia uchawi ili kufanikisha ujambazi wao?” Mkurugenzi allimuuliza.
“Ndiyo amekiri ingawa alituambia kwamba alikuwa akiwadanganya tu.”
“Yeye pia ni mhalifu. Anapaswa ashitakiwe. Msiwasahau na hao wasichana wawili.”
“Wote tutawajumuisha pamoja. Mahakama ndio yenye maamuzi.”
“Ni sawa. Nataka nikwambie kuwa leo umenipa furaha. Hao watu watatu mliowakamata walikuwa wakisumbua kichwa changu.”
“Ni kweli afande. Hata mimi nimefurahi wale watu kupatikana.”
“Tukifanya kazi namna hii tutalijengea heshima kubwa jeshi letu.”
“Ni kweli afande. Sasa mimi narudi kuendelea na kazi yangu. Nilikuja kukufahamisha hilo tu.”
“Sawa. Unaweza kwenda.”
Inspekta Amour alipoondoka ofisini kwa Mkurugenzi wa Upelelezi alikwenda moja kwa moja nyumbani kwa Almasi.
Alipokaribishwa ndani alimwambia Almasi kuwa wale majambazi watatu waliowaua wanawe wamekamatwa. Almasi na mke wake walishituka.
“Mmeshawakamata?” Almasi akamuuliza.
“Tuliwakamata jana usiku na tutawafikisha mahakamani hivi karibuni.”
“Mliwakamata wapi?”
“Tuliwakamata kwenye nyumba moja iliyopo Buguruni lakini haikuwa rahisi kuwatia mikononi. Walikuwa na bunduki na tulirushiana risasi. Polisi wetu wawili waliuawa na majambazi wawili pia waliuawa.”
Almasi akatikisa kichwa kusikitika.
“Hii ni hatari!” Akasema na kuongeza.
“Hawa wanataka waishinde dola!”
“Na dola haitashindwa. Tutaendelea kupambana nao mpaka tuhakikishe kuwa Dar es Salaam ni salama na ni mhali bora pa kuishi katika majiji ya Afrika.”
Almasi akampa mkono Amour.
“Ningali nawakumbuka wanangu lakini pia nimefurahi kusikia kuwa majambazi hao wamekamatwa.”
“Tutawafikisha mahakamani muda si mrefu na wewe umo katika orodha ya mashahidi wetu.”
“Kwa hiyo na mimi nitaitwa mahakamani?”
“Ndiyo. Lakini si kwa sasa, ni mpaka usikilizwaji kesi utakapoanza. Wakati ukiwadia tutakufahamisha.”
“Nashukuru sana.”
Inspekta Amour baada ya kuwafahamisha kuhusu kukamatwa kwa majambazi hao aliaga na kuondoka.
*************
Kulikuwa kuna mkutano wa wamiliki wa makampuni ya kuzalisha maji safi yanayouzwa kwenye chupa za plastiki. Mkutano huo uliandaliwa kufanyika Arusha na taarifa ilitolewa wiki mbili kabla ya kufanyika kwa mkutano huo.
Almasi alipopata taarifa ya kufanyika kwa mkutano huo alimtaka mwanawe John ahudhurie mkutano huo kwa vile yeye ndiye aliyekuwa meneja wa kampuni.
Alikuwa amefanywa meneja tangu kaka yake James aliyekuwa mhasibu wa kampuni hiyo alipouawa na majambazi.
Baba yake aliona yeye awe meneja na akaajiri mhasibu mwingine.
“Itabidi uondooke kesho alfajiri kwa gari.” Almasi alimwambia mwanawe nyumbani kwake.
“Ndiyo baba. Nitaondoka alfajiri, mpaka saa sita nitakuwa nimeshafika.” John alimwambia.
“Mkutano utakuwa keshokutwa, kwa hiyo utakuwa na muda wa kutosha wa kupumzika kabla ya kurudi.”
“Baada ya mkutano nitalala tena. Alfajiri ya siku itakayofuata nitaanza safari ya kurudi.”
“Ni sawa. Kawasikilize. Kama kutakuwa na cha kuchangia utatoa mchango wako.”
“Sawa baba.”
Alfajiri ya siku iliyofuata ndipo John alipoanza safari. Alikuwa na uzoevu wa kusafiri na gari. Alishawahi kwenda Arusha mara kadhaa huku akiendesha mwenyewe.
Aliwahi pia kwenda Dodoma na Tanga. Ingawa mara kadhaa baba yake aliwahi kumshauri kutumia usafiri wa ndege kwa safari ndefu kama za kwenda Arusha au Dodoma lakini John alikataa.
Alikuwa akimuuliza baba yake.
“Kwani hii gari ni ya kazi gani? Kama ninao usafiri wangu siwezi kutumia usafiri mwingine.”
Baba yake alishamzoea, hivyo inapotokea safari anajua kuwa usafiri wa john ni wa gari na si vinginevyo. Na ndiyo sababu ilipotokea safari ya kwenda Arusha alimshauri aondoke saa kumi na moja alfajiri, sio tu kukwepa jua bali pia kuwahi kufika mapema.
John alipita barabara ya Bagamoyo na kutokea Msata. Kisha akakanyaga mafuta kuelekea Njiapanda ya Segera iliyoko mkoani Tanga. Alijua akifika Tanga atakamata barabara ya Korogwe kuelekea Arusha.
Baada ya kulivuka daraja la Mto Wami alihisi usukani wa gari ukicheza mikononi mwake. Akapunguza mwendo kisha akaisimamisha gari pembeni mwa barabara mahali penye msitu.
Alifungua mlango na kushuka. Alirudi nyuma ya gari na kuzikagua tairi za nyuma za gari hilo. Akagundua tairi ya upande wa kushoto haikuwa na upepo. Ilikuwa imepata panchari!
Alipoukubali ukweli huo kwamba tairi moja ilikuwa imepata pancha na kwamba asingeweza kuendelea na safari bila kubadili tairi ndipo aliponza kushughulika.
Alitoa tairi moja ya akiba akatoa sanduku la spana pamoja na jeki.
Aliiweka jeki chini ya gari upande ule uliokuwa na tairi iliyopata panchari akaiinua gari kisha akaitoa tairi hiyo na kuipachika nyingine na kuanza kukaza nati.
Alikaza nati ya kwanza kisha akaanza nati ya pili. Wakati anaitia spana kwenye nati ya tatu akahisi kitu chenye makali kikimtekenya shingoni mwake. Akashituka na kugeuza uso. Akamuona mtu aliyekuwa amevaa mavazi meusi nyuma yake akiwa amemshikia panga lililokuwa limesogezwa kabisa kwenye shingo yake.
Cha kutisha zaidi ni kuwa shingo ya mtu huyo ilikuwa imechinjwa na kufanya kichwa chake kiwe kinaning’inia kama kilichotaka kuanguka!
Upande wa kulia na wa kushoto wa mtu huyo kulikuwa na watu wengine wawili waliovaa mavazi meupe.