MAUAJI YA KUTISHA -04
Muktasari:
- “Mke wangu nakuomba ujikaze, kuna tukio limetokea hapa Mikocheni.”
ALIPONITHIBITISHA kuwa kweli mwanawe alikuwa ameuawa akaenda pembeni na kumpigia simu mke wake.
“Mke wangu nakuomba ujikaze, kuna tukio limetokea hapa Mikocheni.”
“Tukio gani?” Mke wake akamuuliza kwenye simu.
“Martin ameuawa!”
“Martin ameuawa?”
“Ndiyo.”
“Martin yupi?”
“Martin mtoto wetu.”
“Usiniambie! Martin ameuawa wapi?”
Almasi akamueleza kama alivyoelezwa na polisi.
“Ninakuja huko huko.”
“Usije. Mwili wake utaondolewa sasa hivi. Tafadhali subiri hapo hapo nyumbani. Nitakuwa ninakufahamisha kila kitu.”
Almasi akakata simu.
Hapo ndipo kachero Inspekta Amour alipowasili. Baada ya Amour kupata maelezio kutoka kwa polisi aliowakuta hapo alitambulishwa kwa mzee Almasi ambaye alimwambia alimuhitaji ofisini kwake watakapoondoka hapo.
Nusu saa baadaye mwili wa Martin ulipakiwa kwenye gari la polisi na kupelekwa hospitali ya Muhimbili. Polisi nao waliondoka wakiwa na mashuhuda watatu ambao walikwenda nao kituo cha polisi kuandikisha maelezo.
Inspekta Amour naye alirudi ofisini kwake.
Nusu saa tu baadaye, Almasi aliyekuwa bado akitokwa na machozi alibisha ofisini humo.
Amour alimkaribisha, Almasi aliingia na kuketi kwenye kiti.
“Mzee uliniambia kuwa yule ni mwanao.”
“Ndiyo ni mwanangu” Almasi alimjibu kabla ya kujifuta uso wake kwa kitambaa.
“Ni mwanao wa ngapi?”
“Ni mwanangu wa kwanza.”
“Anaitwa nani?”
“Anaitwa Martin Almasi.”
“Alikuwa anatoka wapi na alikuwa anakwenda wapi kabla ya kukutwa na tukio lile?”
“Nadhani alikuwa anatoka benki. Nilikuwa nimemtuma aende benkii akachukue mishahara ya wafanyakazi wetu wa kiwanda cha maji safi ambacho kipo pale pale Mikocheni.”
“Kwa hiyo lile tukio limemkuta wakati anatoka benki?”
“Nafikiri ni hivyo.”
“Hakukuwa na fedha zilizokutwa kwenye gari, huenda fedha hizo zimeporwa. Unadhani alikuwa amechukua kiasi gani kutoka benki?”
“Tulipanga kwamba angechukua shilingi milioni themanini”
“Kama kweli atakuwa amechukua pesa hizo ni kwamba shilingi milioni themanini zitakuwa zimeporwa?”
“Itakuwa ndiyo hivyo.”
“Walioshuhudia tukio hilo wameeleza kwamba waliona watu watatu ambao waliisimamisha gari yake kisha wakamfuata kwenye mlango ambapo mmoja alitoa panga na kumchinja na kisha kuchukua mkoba wake ambao unadhaniwa ndio uliokuwa na pesa…”
Almasi alliijifuta machozi kabla ya kumtazama tena Inspekta Amour.
“Kwa hiyo hilo litakuwa ni tukio la ujambazi?”
“Kwa vile kuna pesa ambazo zimeporwa litakuwa ni tukio la ujambazi lakini kinachotutatiza ni hao watu walioonekana wakifanya ujambazi huo. Hawakuwa watu wa kawaida.”
“Walikuwaje?”
“Inasemekana walikuwa watu watatu. Wawili walikuwa wamevaa mavazi meupe, mmoja alivaa mavazi meusi. Huyo aliyekuwa amevaa mavazi meusi kichwa chake kilikuwa kimechinjwa na kilikuwa kinaning’inia.”
Uso wa Almasi ulionesha mshangao.
“Kichwa chake kilikuwa kimechinjwa na nani?” Akauliza.
“Ndiyo haifahamiki. Sasa huyo ambaye ameelezwa kwamba kichwa chake kilikuwa kinaning’inia ndiye aliyemchinja marehemu na kupora mkoba wake wa fedha.”
“Sijakuelewa Inspekta. Mtu huyo angewezaje kumchinja mtu wakati yeye mwenyewe alikuwa amechinjwa?”
“Huo ndio utata uliopo katika hili tukio. Hili si tukio la kawaida ndiyo maana limeishitua serikali.”
“Si la kawaida kweli. Sijawahi kuona majambazi wa aina hiyo!”
“Na hata mimi pamoja na kufanya kazi hii kwa karibu robo tatu ya umri wangu, sijawahi kuona majambazi wa aina hiyo. Kinachokushangaza wewe ndicho kinachonishangaza mimi.”
“Kumbe mwanangu aliuawa na watu hao?”
“Watu hao ndio waliomuua mwanao.”
“Sasa baada ya kupora huo mkoba wa fedha walitoweka vipi?”
“Haifahamiki. Watu walioshuhudia tukio hilo wamesema hawajui jinsi watu hao walivyotoweka.”
“Mmh…! Hilo tukio ni la kushangaza sana.”
“Sasa sisi tunaendelea na uchunguzi wetu. Mkurugenzi wa upelelezi amenipa jukumu la kuwasaka watu hao ili wapatikane na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.”
“Sasa huyo anayedaiwa kuwa amechinjwa kisha akamchinja Martin atakuwa yuko hai kweli?”
“Maswali mengi tutakuwa tunajiuliza kwa sasa lakini hayatakuwa na majibu. Majibu yatapatikana wakati uchunguzi wetu utakapokamilika. Lakini kama mtu huyo alikuwa hai wakati akifanya tukio hilo, atakuwa hai hadi hivi sasa.”
“Mimi nawaomba muwasake hao watu ili tuwajue ni kina nani na pia washughulikiwe kwa mujibu wa sheria.”
“Tuko pamoja.”
Baada ya hapo Inspekta Amour alichukua namba ya simu ya Almasi. Alimwambia atakapomhitaji tena atampigia.
Allmasi alipoondoka ofisini humo, Inspekta Amour aliinua mkono wa simu iliyokuwa mezani kwake.
Alibonyeza tarakimu. Simu ya upande wa pili ilipopokelewa alisema.
“Inspekta Amour hapa. Ninawataka wale mashuhuda wa tukio la mauaji na ujambazi lilitokea kule Mikocheni.”
“Unawahitaji wafikishwe huko makao makuu?” Sauti ikauliza kutoka simu ya upande wa pili.
“Ndiyo. Ninawahitaji ofisini kwangu kwa mahojiano.”
“Sawa.”
Amour akaurudisha mkono wa simu.
Kama kawaida yake aliinuka na kwenda kusimama kando ya dirisha.
Kwa mara nyingine tena alijiuliza kama mashuhuda wa tukio hilo walimuona sawa sawa mtu aliyemchinja Martin. Alijiuliza hivyo baada ya kuona kuwa ilikuwa haiwezekani kwa mtu ambaye shingo yake ilikuwa imechinjwa aweze kumchinja mtu mwingine.
Kama kulikuwa na utata katika tukio hilo, Amour alijiambia, utata ulikuwa ni huo.
Alijaribu kulifananisha tukio hilo na tukio ambalo lilitokea zamani ambapo mwanamke mmoja aliuawa na uchunguzi ulikuja kuonesha kuwa mtu aliyemuua alikuwa ameshakufa mwaka mmoja uliopita.
Mashuhuda wa tukio hilo waling’ang’ania kueleza kuwa aliyemuua mwanamke huyo alikuwa Christian Bambo wakati taarifa zilizopo Bambo alishakufa kabla ya tukio hilo.
Bambo alikutwa ameungua na kuteketea kwa moto baada ya gari lake kuwaka moto huku mwenyewe akiwemo ndani.
Lakini mwaka mmoja baadaye Bambo huyo huyo alikuja kuonekana na watu akimuua mjane wake kwa kumpiga risasi na hatimaye kutoweka.
Alama za vidole zilizokutwa katika eneo la tukio zilikuwa ni za Bambo lakini Bambo mwenyewe alishathibitika kuuawa kwa moto huku mke wake akithibitishia polisi kuwa gari la mume wake lilikuwa na matatizo yaliyosababisha lilipuke na kuwaka moto uliomteketeza mwanaume huyo.
Baada ya uchunguzi wa mwaka mzima, Amor alikuja kugundua mbinu zilizotumika kumficha muuaji. Bambo alikuja kukamatwa jijini Nairobi akiwa hai.
Uchunguzi ulionesha kuwa hakuwa ameteketea kwa moto na kufa bali aliyeteketezwa alikuwa mtu mwinggine lakini aliwekewa vitambulisho vya Bambo mfukoni mwake. Hivyo mwili wake ulioungua ulipopekuliwa ulikutwa na mabaki ya vitambulisho vya Bambo. Polisi wakaamini kuwa aliyeteketea alikuwa Bambo.
Mke wake ambaye alikula njama na mume wake alilipwa bima na alirithi mali za Bambo lakini Bambo akiwa mafichoni alikuja kukorofishana na mke wake kuhsu mali, ndipo alipoamua kumuua jambo ambalo lilizua utata wa nani aliyemuua.
Kumbe yule mtu aliyeteketezwa na moto alikuwa ni ndugu yake Bambo. Bambo alimteketeza ndugu yake ili achukue mali yake kwa vile hakuwa na mke wala watoto.
Alivyokufa haikujulikana kwamba alikufa yeye. Watu hawakujua alikuwa amekwenda wapi. Badala yake walijua kuwa aliyekufa alikuwa Bambo.
Hatimaye Bambo alikamatwa na kuhukumiwa kunyongwa.
Amour alijiambia muuaji wa Martin anaweza kuwa kama Bambo.
Nusu saa tu baadaye polisi mmoja alibisha ofisini mwa Inspekta amour na alipokaribishwa alimwambia Amour kuwa amekuja na mashuhuda wa tukio la mauaji ya Mikocheni.
“Wako wangapi?” Amor alimuuliza.
“Ni watatu.”
“Wambie waingie mmoja mmoja. Nataka kuwahoji maswali.”
Polisi huyo alitoka. Baada ya dakika moja aliingia na mtu mmoja.
“Mtu wa kwanza ni huyu Afande,” alimwambia Amour kisha akatoka ofisini.
“Kaa kwenye kiti.” Amour alimwambia mtu huyo.
Alikuwa kijana wa umri usiopungua miaka ishirini na minane. Jinsi alivyonyoa nywele zake, sura yake na mavazi yake, alionesha alikuwa ni mmoja wa vijana wa mjini wanaopenda kushinda vijiweni wakisubiri wasichana wapite wawatongoze.
Kijana huyo alikaa kwenye kiti kwa taratibu kama vile aliogopa kukivunja.
Ofisi ya polisi ni ya polisi tu. Unapoingia hata kama huna kosa ni lazima unywee.
“Jina lako tafadhali.” Amour alimuulliza akiwa ameshika kalamu.
“Naitwa Shefa Ibrahim.”
Amour aliandika jina lake kabla ya kumuuliza.
“Una umri gani?”
“Mwezi ujao nitatimiza miaka ishirini na tisa.”