Yammy afunguka baada ya kuachana
Muktasari:
- Kauli hiyo ya Yammy inakuja baada ya msanii huyo kuweka wazi hivi karibuni, kwa sasa yupo singo baada ya kuvunjika kwa uhusiano wake na aliyekuwa mpenzi wake, Ahmed.
MWANAMUZIKI wa Bongo Fleva, Yasirun Yasin Shaban ‘Yammy’, amesema mtu anapotoka kwenye uhusiano, anapaswa kuangalia mbele badala ya kuendelea kushikilia yaliyopita.
Kauli hiyo ya Yammy inakuja baada ya msanii huyo kuweka wazi hivi karibuni, kwa sasa yupo singo baada ya kuvunjika kwa uhusiano wake na aliyekuwa mpenzi wake, Ahmed.
Akizungumza na Mwanaspoti, Yammy amesema mtu anapofikia uamuzi wa kuachana na mwenza wake, hakuna sababu ya kuendelea kujadili mambo yake au kutumia muda mwingi kumkumbuka, bali ni muhimu kila mmoja akaendelea na maisha yake.
“Kama umechana na mtu hakuna sababu ya kujadiliana na wenzako mambo yake, wewe songa mbele,” amesema Yammy.
Yammy amesema mara nyingi mtu anapotoka kwenye uhusiano anaweza kupitia kipindi kigumu, lakini hilo halipaswi kuwa sababu ya kushindwa kuendelea na maisha baada ya uhusiano huo kufikia mwisho.
Hata hivyo, Yammy hajaweka wazi sababu za uhusiano huo kuvunjika, jambo ambalo limeacha kila mmoja na tafsiri yake kuhusu kilichotokea kati yao na kwa sasa anaendelea na shughuli zake za muziki.