Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yammi alivyomrejesha Nandy kwa Billnass

YAMMY Pict

Muktasari:

  • Yammi aliyevuma kupitia wimbo wake, Tiririka (2023), hapo Machi 2025 ndipo The African Princess ilitangaza kusitisha mkataba wake na msanii huyo kwa makubaliano ya pande zote mbili bila kutaja sababu iliyopelekea hasa uamuzi huo.

KUTOKANA na kitendo cha Yammi kuachana na The African Princess, lebo yake Nandy, kimemfanya mwanamuziki huyu kurejea katika mtindo wa uendeshaji lebo kama ilivyo kwa mumewe Billnass, rapa aliyetoka na kibao chake, Raha (2014).

Yammi aliyevuma kupitia wimbo wake, Tiririka (2023), hapo Machi 2025 ndipo The African Princess ilitangaza kusitisha mkataba wake na msanii huyo kwa makubaliano ya pande zote mbili bila kutaja sababu iliyopelekea hasa uamuzi huo.

The African Princess ilimtambulisha Yammi hapo Januari 20, 2023 akiwa msanii wa kwanza kusainiwa na lebo hiyo, na ujio wake uliambatana na Extended Playlist (EP), Three Hearts (2023) yenye nyimbo tatu ambazo hakumshirikisha msanii yeyote.

Hatua hiyo ni baada ya Nandy kumuona Yammi akiimba nyimbo za wasanii mbalimbali katika mtandao wa TikTok na kuvutiwa na kipaji chake, basi wakakutana na kuzungumza biashara ya muziki kisha akamsaini lakini sasa meza imepinduka.

YAM 01

Kwa sasa Nandy hamsimamii mwanamuziki yeyote chini ya lebo yake ambayo alisema ni kwa ajili ya wasanii wa kike pekee, zama hizi mpya zinafanana na za lebo ya Billnass, Mafioso Inc ambayo haijamsaini yeyote zaidi ya kusimamia kazi za rapa huyo pekee.

Licha ya hapo awali Billnass kusema mipango yake kwa siku zijazo ni kuja kusaini wasanii wapya ndani ya Mafioso Inc ambayo imekuwapo tangu mwaka 2021, hadi sasa hajafanya hivyo na huenda akaingia woga kwa hiki kichotokea kwa Nandy.

Ikumbukwe Billnass alitoka kimuziki chini ya Rada Entertainment baada ya kuachia ngoma yake, Raha (2014) ambayo aliwashirikisha TID na Naziz, mwanachama wa zamani wa kundi la Necessary Noize kutokea Kenya.

Hata hivyo, muda mfupi baadaye alikuja kuachana na Rada Entertainment kisha kufanya kazi na lebo nyingine kama L.F.L.G (Live First Live Good) na Rooftop Entertainment kabla ya kufungua yake ambayo ndio hiyo Mafioso Inc hapo mwaka 2021.

Billnass, mshindi wa TMA 2022, akizungumza na gazeti hili wakati huo, alisema alianzisha Mafioso Inc na watu wake ambao awali ndio walishirikiana kuanzisha pamoja L.F.L.G ambayo hapo awali ndio ilikuwa inamsimamia pamoja Country Wizzy.

YAM 03
YAM 03

“Mafioso Inc itakuwa upande wa muziki zaidi, mavazi pamoja na vitu wanavyopenda mashabiki wetu na mimi ni mmoja wa wasanii ambao wapo ndani yake, lengo kubwa ni kuja kusimamia wasanii wapya hapo baadaye.” alisema Billnass.

Kwa kufungua lebo, Billnass aliungana na wasanii wengine wa Hip Hop waliofanya hivyo kama Joh Makini (Makini Label), Fid Q (Cheusi Dawa Entertainment), Moni Centrozone (Majengo Sokoni), Darassa (Classic Music Group (CMG) n.k.

Utakumbuka kabla ya Mafioso Inc, Billnass alipita Rada Entertainment na L.F.L.G, ni kama ilivyo kwa mkewe Nandy ambaye kabla ya The African Princess, aliwahi kusimamiwa na Epic Records inayomilikiwa na Sony Music Entertainment.

Kwa sasa linapokuja suala la lebo, Nandy hatofautiani sana na Billnass maana wote hawasimamii msanii yeyote lakini angalau Nandy katulea mwanamuziki mmoja (Yammi) kuliko Billnass ambaye ameendelea kusonga mbele mwenyewe.

Chini ya The African Princess, Nandy alimfanya Yammi kuwa msanii mkali na maarufu ndani ya kipindi kifupi, mathalani katika Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) 2023, aliwania kipengele cha Msanii Bora Chipukizi kupitia wimbo wake, Namchukia (2023).

YAM 02

Huyu ndiye msanii wa tatu wa kike Bongo aliyesikilizwa (most streamed) zaidi katika mtandao wa Boomplay Music 2023 akiwa ametanguliwa na Zuchu na Nandy, mwanamuziki aliyetoka na kibao chake, Nagusagusa (2016) chini Tanzania House of Talent (THT).

Yammi kupitia muziki wake anaonekana kuwa na ushawishi mtandaoni zaidi, tangu ametambulishwa katika tasnia hapo Januari 2023, ameweza kuwavutia wafuasi (followers) zaidi ya milioni 1.3 Instagram, akiwa amewaacha mbali washindani wake wote wa TMA 2023.

Utakumbuka washindani wake walikuwa ni Xouh (Lalala), Appy (Watu Feki), Mocco Genius (Mi Nawe) na Chino Kidd (Gibela) aliyeibuka mshindi ikiwa ni tuzo yake ya pili kutoka TMA baada ya hapo awali kushinda kama Dansa Bora 2022.

Hadi anaachana na The African Princess, Yammi alikuwa amemshirikisha bosi wake Nandy katika wimbo mmoja tu, Lonely (2024), huku video zake zikiwa zimetazamwa YouTube zaidi ya mara milioni 50 ikiwa ni ndani ya miaka miwili.

Ikumbukwe ndani ya Bongofleva wanamuziki wa kike waliotazamwa zaidi YouTube ni Zuchu, kisha anafuata Nandy ambaye tayari ametoa EP tatu, Taste (2021), Maturity (2022) na Wanibariki (2021) pamoja na albamu moja, The African Princess (2018).