Waliondoka mapema, lakini nyimbo zao bado zinaishi
Muktasari:
- Mjadala huo umeongezeka kufuatia ujio wa mwanamuziki wa Nigeria, Davido, nchini Tanzania Novemba 10 mwaka huu, ambapo alikutana na Diamond na kuibua matarajio ya kufanya mradi mwingine wa pamoja, miaka 12 baada ya wawili hao kufanya wimbo ‘Number One Remix’.
KATIKA muziki, kuna majina ambayo huondoka duniani lakini kazi zao zinaendelea kuishi kwa miaka mingi. Ni wasanii waliokuwa wameanza kujenga majina, kuvutia mashabiki na kuonesha uwezo mkubwa wa kufika mbali zaidi, lakini safari zao zikakatishwa na vifo wakiwa bado na mengi ya kufanya.
Wengine walikuwa wameanza kuvuka mipaka ya nchi zao, kufanya ushirikiano na mastaa wakubwa na kuingiza muziki wao katika masoko mapya lakini vifo vyao viliacha maswali kuhusu kazi ambazo wangeendelea kuzifanya na ukubwa ambao wangeweza kuufikia.
Kutoka Afrika Kusini hadi Nigeria, kisha Tanzania, kuna simulizi za wasanii ambao majina yao yanaendelea kukumbukwa kupitia nyimbo walizoacha. Miongoni mwao ni Thami Shobede, Costa Titch, AKA, Mohbad, Haitham Kim na Nezo B.
THAMI SHOBEDE
Thami Shobede alianzia katika mashindano ya Idols South Africa, alikoshiriki mwaka 2015 lakini akaishia hatua ya Top 16, hakukata tamaa, kwani alirejea tena mwaka 2016 na safari hiyo akafika fainali, akimaliza nafasi ya pili.
Mafanikio hayo yalimfungulia milango ya kupata mkataba na Gallo Records na kuanza kujenga safari yake binafsi ya muziki.
Mwaka 2017 aliachia albamu yake ya kwanza, Never Lost, iliyokuwa na nyimbo 11 zikiwemo Sthandwa, My Heart Is Yours, Letting Go aliyoshirikishwa Brenda Mtambo, Night and Day, Ngiyakuthanda na I Love You.
Albamu hiyo ilikuwa na ladha ya Afro-soul na Pop, huku nyimbo zake nyingi zikizungumzia mapenzi na hisia.
Miongoni mwa kazi zinazomfanya Thami aendelee kukumbukwa ni I Love You, wimbo ambao bado unatajwa na mashabiki wanapozungumzia muziki wake na umefikisha views million 5 YouTube.
Septemba 12, 2019, akiwa na miaka 31, Thami alifariki katika Hospitali ya Kalafong, Pretoria, Gallo Records ilithibitisha kifo chake na kueleza kuwa alifariki baada ya kuugua kwa muda mfupi na kupata matatizo yaliyosababisha kushindwa kufanya kazi viungo vya mwili.
COSTA TITCH
Costantinos Tsobanoglou maarufu Costa Titch, alikuwa miongoni mwa wasanii waliokuwa wakipanua ushawishi wa Amapiano kimataifa.
Alianza kujulikana pia kupitia uchezaji na kuonekana kwenye video za wasanii mbalimbali kabla ya kujikita zaidi kwenye muziki. Baadaye alijijengea jina kupitia nyimbo kama Nkalakatha Remix, Activate na Big Flexa, ambayo ilipata mafanikio makubwa na kuvuka mipaka ya Afrika Kusini.
Mwaka 2020 aliachia albamu Made in Africa, kisha mwaka 2022 akatoa mradi wa Mr Big Flexa.
Kilichomfanya Costa kuwa na uhusiano wa karibu zaidi na mashabiki wa Tanzania ni ushirikiano wake na Diamond Platnumz kwenye wimbo ‘Superstar’, uliotolewa Oktoba 7, 2022. Wimbo huo uliwekwa pia kwenye Albamu ya Mr Big Flexa na kuwaunganisha wasanii hao wawili katika ladha ya Amapiano.
Costa pia alifanya kazi na Mbosso wakati akiwa lebo ya WCB kupitia nyimbo ‘Moyo’ na ‘Shetani’, akiwa pamoja na wasanii wengine wa Afrika. Mbosso aliwahi kueleza kuwa walirekodi wimbo wa ‘Moyo’ ndani ya muda mfupi, chini ya saa moja, na akamsifu Costa kwa umakini wake studio.
Machi 11, 2023, Costa alifariki baada ya kuanguka akiwa anatumbuiza kwenye tamasha la Ultra South Africa jijini Johannesburg. Kifo chake kilishtua mashabiki na tasnia ya muziki, hasa kwa kuwa alikuwa bado anapanua ushirikiano wake kimataifa.
AKA
Kiernan Jarryd Forbes maarufu AKA alikuwa mmoja wa marapa waliokuwa na ushawishi mkubwa Afrika Kusini na Afrika kwa ujumla.
Safari yake ilipata nguvu zaidi kupitia albamu yake ya kwanza Altar Ego ya mwaka 2011, iliyokuwa na nyimbo kama Victory Lap, I Want It All na All I Know. Albamu hiyo ilimletea tuzo na kutambuliwa zaidi, huku baadaye akiendelea kutoa miradi mingine iliyofanikiwa kama Levels, Touch My Blood na Bhovamania. Pia alifanya nyimbo zilizopata umaarufu mkubwa kama Congratulate, The World Is Yours na Fela in Versace, zilizomjengea nafasi ya kuwa miongoni mwa majina makubwa ya Hip Hop Afrika.
Februari 10, 2023, AKA alipigwa risasi na kufariki akiwa na miaka 35 nje ya mgahawa mjini Durban. Taarifa ya Serikali ya Afrika Kusini ilithibitisha kifo chake na kutambua mchango wake kama rapa, mtunzi, mtayarishaji wa muziki na mfanyabiashara.
Kuondoka kwake kulikuwa pigo kwa Hip Hop ya Afrika Kusini, hasa kutokana na uwezo wake wa kuandika na kutengeneza muziki uliokuwa na utambulisho wake.
MOHBAD
Ilerioluwa Oladimeji Aloba, maarufu kama Mohbad au Imole, alikuwa msanii aliyeanza kupata umaarufu kupitia Afrobeats nchini Nigeria.
Mwaka 2020 alitoa EP yake ya kwanza Light, iliyomsaidia kuimarisha nafasi yake katika muziki wa Nigeria. Baadhi ya nyimbo zilizompa umaarufu ni ‘Ponmo’ aliyoshirikishwa Naira Marley na Lil Kesh.
Mwaka 2023 aliachia EP Blessed, ikiwa ni miongoni mwa kazi zake baada ya kuondoka Marlian Records na kuanza kujitegemea kupitia lebo yake ya Imolenization.
Kilichovutia zaidi ni namna ambavyo nyimbo zake zilivyoongeza usikilizwaji baada ya kifo chake.
Mohbad alifariki Septemba 12, 2023, akiwa na miaka 27. Kifo chake kilizua mjadala mkubwa nchini Nigeria na kusababisha maandamano ya wananchi waliotaka uchunguzi wa kina na Shirika la habari la Associated Press liliripoti kuwa polisi walifukua mwili wake kwa ajili ya uchunguzi wa kitabibu.
HAITHAM KIM
Ni miongoni mwa wasanii wa kike walioanza kujenga majina katika Bongo Fleva kabla ya kufariki dunia Septemba 1, 2023.
Alikuwa akitambulika kupitia nyimbo kama Hakutaki, Dubai, I Wish, Utamu aliyomshirikisha Young Lunya na I Love You.
Haitham alifariki katika Hospitali ya Temeke jijini Dar es Salaam baada ya kuugua matatizo ya mfumo wa upumuaji, ikiwemo nimonia.
Wakati huo alikuwa bado katika hatua ya kujenga jina lake, huku wasanii wenzake na wadau wa muziki wakijitokeza kuchangia gharama za matibabu yake.