Ukweli hakuna Destiny’s Child bila Beyonce, Kelly
Muktasari:
- Destiny’s Child, wakali wa ngoma, Survivor (2001), wasanii walioanza kupata mafanikio na kundi hilo ni Beyonce, Kelly Rowland, pamoja na LeToya Luckett na LaTavia Roberson ambao walikuja kujitoa.
Ukiwazungumzia Destiny’s Child, moja kwa moja majina mawili yanayokujia kwa haraka ni Beyonce Knowles na Kelly Rowland, ingawa kundi hilo lililoanzishwa mwaka 1990 huko Texas, Marekani, lilijumuisha na wanamuziki wengine.
Hakuna ubishi Beyonce na Kelly Rowland ndio wamesalia kama utambulisho na nguzo muhimu ya Destiny’s Child, kundi la waimbaji wa kike waliovuma zaidi katika miondoko ya RnB na Pop.
Destiny’s Child, wakali wa ngoma, Survivor (2001), wasanii walioanza kupata mafanikio na kundi hilo ni Beyonce, Kelly Rowland, pamoja na LeToya Luckett na LaTavia Roberson ambao walikuja kujitoa.
Baadaye ndipo Michelle Williams na Farrah wakajiunga na kundi hilo. Hata hivyo, Farrah naye aliondoka muda mfupi baadaye huku kundi hilo likiendelea na wanachama watatu hadi sasa.
Wazazi wa Beyonce, Mathew na Tina, walifanya kazi kwa ukaribu mkubwa na kundi hilo kuhakikisha linafanikiwa. Mathew alisimama kama meneja wa tangu mwanzo hadi mwaka 2006 ambapo Destiny’s Child ilisambaratika rasmi.
Kwa upande wake Tina, alikuwa mbunifu wa mabinti hao kuanzia mitindo ya nywele hadi mavazi. Ukimuona Kelly Rowland akimuita Tina mama katika mitandao ya kijamii, ni kwa sababu ana mchango mkubwa katika safari ya muziki wao.
Ni Kelly Rowland ambaye alifanya vizuri katika kolabo na Nelly, Dilemma (2002), ambayo video yake hadi sasa imeshatazamwa (views) YouTube zaidi ya mara Bilioni 1.8 ikiwa ni video ya tatu ya Hip Hop duniani kufikia namba hizo.
Kipindi wimbo huo umeachiwa ulipangua ratiba nyingi za Destiny’s Child, hiyo ni kwa sababu uongozi wa kundi hilo uliona wimbo huo umeibeba vizuri albamu ya Nelly, Nellyville (2002), hivyo ukaona ndio muda sahihi kwa Kelly Rowland naye kuachia albamu yake.
Beyonce ambaye alipanga kutoa albamu yake ‘Dangerously in Love’ Oktoba 2002, alisogeza mbele hadi Juni 2003 na kumpisha Kelly Rowland kutembelea upepo wa Dilemma akitoa albamu yake ‘Simply Deep’ hapo Oktoba 2002 wakati awali ilipangwa kuachiwa 2003.
Uongozi wa Destiny’s Child uliharakishwa sana kurekodiwa kwa albamu hiyo ya Kelly Rowland, na ndani ya wiki tatu tu ikawa imekamilika ili kwenda sambamba na mafanikio ya Dilemma, wimbo ambao ilijumuishwa pia katika albamu hiyo ya Kelly Rowland ukiwa kama wimbo wa kwanza kutoka.
Baada ya hapo ndipo Beyonce naye akaaachia albamu yake ya kwanza akiwa kama solo, Dangerously in Love (2003), ambayo ilikuja baada ya kushiriki kikamilifu katika albamu tano za Destiny’s Child, pamoja Extended Playlist (EP) moja.
Mradi huo ulikuwa ukurasa mpya kwa Beyonce ambaye hadi sasa ameshaachia albamu nane ambapo albamu yake ya mwisho, Cowboy Carter (2024) ilishinda tuzo ya Grammy kama Albamu Bora ya Mwaka ikiwa ni mara yake ya kwanza kushinda kipengele hicho!.
Beyonce, mshindi wa Grammy mara 35, ndiye mwanachama wa Destiny’s Child mwenye mafanikio makubwa zaidi kimuziki pamoja na kiuchumi. Ana nguvu kubwa ya ushawishi kuliko yeyote yule ndani ya kundi hilo, na hata idadi ya wafuasi alionao mtandaoni ni uthibitisho tosha wa nguvu yake.
Tunaweza kusema albamu hizo za Kelly Rowland na Beyonce, zilihashiria mwisho wa Destiny’s Child kwani tangu wakati huo kila mmoja alijikita kufanya kazi zake binafsi na kufikia mwaka 2006, ikawa ni rasmi kuwa kundi hilo halipo tena.
Hata hivyo, wawili hao pamoja na Michelle Williams, wameendelea kuwa na ukaribu na mara kadhaa wamepanda jukwaani wakitumbuiza kama kundi la Destiny’s Child kwa kuimba nyimbo zao maarufu kama Say My Name, Soldier, Cater 2 U, Lose My Breath, Bills, Bills, Bills n.k.
Watatu hao wamewahi kutumbuiza pamoja katika matukio kama Super Bowl Halftime Show 2013, tamasha la Coachella 2018, pamoja show ya mwisho ya ziara yake Beyonce, Cowboy Carter Tour 2025.
Lakini Beyonce na Kelly Rowland ndio hasa wanaendelea kufanya muziki na ndio wasanii wa Destiny’s Child waliokuja kufanikiwa zaidi nje ya kundi hilo ambalo lilishinda tuzo tatu za Grammy, huku wakiuza rekodi zaidi ya milioni 60.
Jarida la Billboard liliwataja Destiny’s Child kuwa miongoni mwa makundi matatu ya muziki yaliyowahi kuwa bora zaidi katika historia duniani, pia wamewahi kutunukiwa nyota ya heshima ya Hollywood Walk of Fame.
Mbali na muziki, Beyonce na Kelly Rowland wamekuwa marafiki wa karibu zaidi ambapo kila mmoja hushiriki katika matukio ya kifamilia ya mwenzake. Kwa mfano Kelly Rowland alihudhuria harusi ya Beyonce na Jay Z iliyofanyika New York hapo Aprili 4, 2008.
Naye Beyonce alihudhuria harusi ya Kelly Rowland na Tim Weatherspoon ambayo ilifanyika Mei 9,2014 nchini Costa Rica, pia mdogo wake Beyonce, Solange, pamoja na yao Tina, nao walikuwepo. Ikumbukwe Tim ndiye meneja wa Kelly Rowland, na aliifanya kazi hiyo tangu mwanamuziki huyo yupo Destiny’s Child.