Harmonize, Kajala waasibua gumzo Kenya
Muktasari:
- Gumzo hilo limeibuka baada ya video inayosambaa mitandaoni kuwaonyesha wawili hao wakikutana katika uwanja wa mchezo wa kikapu, ambapo Harmonize alionekana akimfuata Kajala aliyekuwa amekaa pamoja na mastaa wenzake, Jacqueline Wolper, Aunty Ezekiel na Irene Uwoya.
Wakati Dar City ikianza vizuri kampeni yake ya kusaka tiketi ya kucheza Ligi ya Kikapu Afrika (BAL) 2027 kwa ushindi wa pointi 96-76 dhidi ya Ferroviário da Beira ya Msumbiji, msanii wa Bongo Fleva, Harmonize na mwigizaji Kajala wamekuwa gumzo huko Nairobi Kenya, ambako yanaendelea mashindano ya Road to BAL 2027.
Gumzo hilo limeibuka baada ya video inayosambaa mitandaoni kuwaonyesha wawili hao wakikutana katika uwanja wa mchezo wa kikapu, ambapo Harmonize alionekana akimfuata Kajala aliyekuwa amekaa pamoja na mastaa wenzake, Jacqueline Wolper, Aunty Ezekiel na Irene Uwoya.
Katika video hiyo, Harmonize anafika eneo walilokaa mastaa hao na kuanza kuwasalimia, lakini alipomfikia Kajala, hali inaonekana kuwa tofauti, huku mwigizaji huyo akionekana kutokuwa tayari kumpokea salamu zake.
Kajala akataa salamu?
Harmonize anaonekana kujaribu kumvuta Kajala ili wasalimiane, lakini Kajala anaonekana kutokuwa tayari kwa kitendo hicho, hali inayomfanya Harmonize aendelee kumvuta-vuta huku akijaribu kumkaribisha kwenye salamu.
Kitendo hicho kimezua gumzo mitandaoni, huku baadhi ya watu wakijiuliza ni kwa nini Kajala alionekana kutokuwa tayari kusalimiana na Harmonize, ambaye amekuwa na historia ndefu ya kimapenzi naye.
Baada ya hali hiyo, Harmonize anaonekana kuendelea kuwasalimia watu wengine waliokuwa eneo hilo, huku video hiyo ikiendelea kusambaa na kuwafanya mashabiki kuibua mijadala kuhusu hali ya uhusiano wao.
Waliachana Septemba
Tukio hilo limeibuka wakati wawili hao wakihusishwa na taarifa za kutengana kwa mara nyingine baada ya uhusiano wao kuwa na historia ya kuachana na kurudiana mara kadhaa.
Septemba mwaka huu, Harmonize alithibitisha kuwa yeye na Kajala hawakuwa pamoja, akisema walikuwa wametengana kwa takribani miezi mitatu na kwamba uamuzi huo ulifanyika kwa maelewano.
Alisema hawakuwa na ugomvi wa kihisia, bali walifikia hatua ya kuamua kuwa uhusiano wao haukuwa ukienda vizuri, huku akimsifia Kajala na kusema hataki kuzungumza mambo ambayo yanaweza kumchafua.
Hata hivyo, Novemba 4, Kajala alipofanya mazungumzo na Mwanaspoti, alisema hajawahi kutangaza rasmi kuachana na Harmonize tangu waliporudiana, kauli iliyozua maswali kuhusu hali halisi ya uhusiano wao.
Historia ya kurudiana
Harmonize na Kajala wamekuwa na uhusiano wenye misukosuko tangu mwaka 2020, wakiachana na kurudiana mara kadhaa, huku kurudiana kwao kwa mara ya mwisho kukiwa mwishoni mwa mwaka 2025.
Mwaka huu, uhusiano wao ulionekana kuingia hatua nyingine baada ya Harmonize kumvisha Kajala pete ya uchumba, jambo lililozua matumaini kwa mashabiki kuwa huenda safari hii wakafikia hatua ya ndoa.
Sasa, video ya Nairobi imeongeza maswali mapya kuhusu ukaribu wao, huku mashabiki wakitafsiri namna Kajala alivyopokea salamu za Harmonize na kujiuliza kama wawili hao wamebaki na mawasiliano ya kawaida baada ya kutengana.