Tuzo ya Marioo Afrimma yawaibua 'mashemeji' wa Jux Nigeria
Muktasari:
- Katika tuzo hizo zilizofanyika Septemba 12, Dallas, Texas, Marekani, Marioo ameendelea kuongeza orodha ya wasanii wa Bongo walioshinda huku pia zikiibua mjadala na mashabiki kutoka Nigeria wamemtaja Jux ndiye aliyestahili kushinda tuzo hiyo na si Marioo.
NI zamu ya Marioo. Ndiyo, mwaka 2026 Tuzo ya Afrimma ipo mikononi mwake akishinda kipengele cha Msanii Bora wa Kiume Afika Mashariki 'Best Male East Africa'.
Katika tuzo hizo zilizofanyika Septemba 12, Dallas, Texas, Marekani, Marioo ameendelea kuongeza orodha ya wasanii wa Bongo walioshinda huku pia zikiibua mjadala na mashabiki kutoka Nigeria wamemtaja Jux ndiye aliyestahili kushinda tuzo hiyo na si Marioo.
MARIOO NA HISTORIA MPYA
African Muzik Magazine Awards (AFRIMMA) ni tuzo zilizoanzishwa mwaka 2014 Marekani, zikilenga kutambua muziki na wasanii wa Afrika pamoja na wanaofanya kazi kwenye mataifa mengine 'diaspora'.
Washindi hupatikana kutokana na mchakato wa uteuzi na upigaji kura pamoja na tathmini ya waandaaji na majaji kulingana na kipengele husika, hivyo si suala la ukubwa wa jina pekee.
Kwenye kipengele hicho cha 'Best Male East Africa 2026', Tanzania ilikuwa na majina matano ambayo ni Marioo, Juma Jux, Diamond Platnumz, Mbosso na Barnaba, huku nchi nyingine zikiwakilishwa na Bien wa Kenya, Eddy Kenzo na Joshua Baraka wa Uganda, Lij Michael wa Ethiopia na Single Dee wa Sudan Kusini.
Kwa hiyo Marioo hakushindana na Jux peke yake, bali alikuwa kwenye kinyang’anyiro kilichokuwa na majina kadhaa makubwa ya Afrika Mashariki.
TANZANIA NA AFRIMMA
Ushindi wa Marioo unaendeleza historia ya Tanzania kwenye tuzo hizo. Diamond Platnumz alishinda kipengele hicho mwaka 2014, 2015 na 2016, wakati Ommy Dimpoz alitwaa mwaka 2019. Diamond alirudi kushinda mwaka 2020, Nandy akawakilisha wanawake kwa kutwaa mwaka 2021 na Rayvanny akachukua taji hilo mwaka 2022.
MARIOO ANA NINI MWAKA HUU?
Mwaka huu Marioo ametoa albamu MMMCXII, yenye nyimbo tisa, iliyotoka Mei 29. Ndani yake kuna kazi kama Mombasa, Priority akiwa na Bruce Melodie, Doucement na Ya Levis, UA na Sofiya Nzau, Watu na D Voice pamoja na Pombe I na Harmonize.
Mbali na muziki huo, Marioo amekuwa na ushirikiano mbalimbali na wasanii wa Tanzania na nje ya nchi, huku YouTube ikiwa moja ya majukwaa anayoonekana kuwa na nguvu.
JUX HANA CHA KUJIFICHA
Jux anaingia kwenye mjadala huu akiwa na tuzo yake ya kimataifa. Januari 2026 alitwaa Best Male Artist in Eastern Africa kwenye All Africa Music Awards (AFRIMA), zilizofanyika Lagos, Nigeria.
AFRIMA ni tuzo tofauti na AFRIMMA. Jux alimshinda Marioo na wasanii wengine katika kipengele hicho.
Mwaka huu Jux pia ametoa kazi kama Kipepeo, Joy akiwa na Diamond Platnumz na Sexy & Bad.
Hivyo, kwa upande wa tuzo za mwaka huu, kila mmoja ana ushindi wa kimataifa kutoka kwenye jukwaa tofauti; Marioo ana AFRIMMA, wakati Jux ana AFRIMA.
YOUTUBE INAWATOFAUTISHA
Kwa takwimu za YouTube Marioo ana wafuatiliaji takribani milioni 2.43 na watazamaji milioni 695.1, wakati Jux ana wafuatiliaji takribani milioni 2.11 na watazamaji milioni 500.8.
Hiyo inamweka Marioo mbele kwa karibu wafuatiliaji 320,000 na zaidi ya watazamaji milioni 194.
Hata hivyo, namba za YouTube haziwezi peke yake kuamua nani alikuwa bora. Zinatoa picha ya ukubwa wa mashabiki kwenye jukwaa hilo, wakati tuzo huangalia vigezo vingine.
'MASHEMEJI' WA NIGERIA WAJA JUU
Jux amekuwa akitajwa sana Nigeria, hasa baada ya ndoa yake na mwanamitindo maarufu kutoka nchini huko, Priscilla Ojo, jambo lililoongeza ukaribu wake na soko hilo.
Ndiyo maana ushindi wa Marioo umewavuruga na kuijadili huku wengi wakiikosoa na kuona aliyestahili ni Jux ambaye ni shemeji yao kwa Priscilla.
Shabiki wa kwanza aliandika kwenye mtandao wa Instagram "Huyu jamaa hapa ni mzuri hata ana kwa ana.. Mfalme safi wa Africa yeye ndiye anafaa kwa ile tuzo na sio yule waliomchagua."
Mwingine aliandika, "Walidhani wamekunyima haki bila kujua wanapoteza uaminifu. Wakati watu wanapopiga kura na kura zao hazihesabiwi, watu watapoteza hamu nao."
Mwingine alisema "Nadhani acha kuwaheshimu afrimmamusicfest, hii ni mara ya pili wanakudharau. Unaweza kuona unapendwa, lakini huwa hawakuhitaji."
Msikie huyu, anasema, "Mnyenyekevu sana! Maonyesho ya ajabu! Ilikuwa ya kushangaza kushuhudia! Endelea kung'ara!!! Wewe ndio mshindi wetu mkwe."
Mwingine aliongeza; Msicheze na mashabiki wa Nigeria. Msituchezee. Juma ni msanii wetu na tunampenda yeye."
Hata hivyo, ni wazi mashabiki hao hawajamaanisha kumtetea kwa sababu ya 'Ushemeji' bali kwa kazi zao, lakini ukweli unabaki pale pale, Jux ana nguvu ya kimuziki Nigeria kuliko Marioo.
Kwa upande mwingine, Marioo pia si mgeni kwenye tuzo za kimataifa na amewahi kuingia kwenye vinyang'anyiro mbalimbali na tuzo ya sasa ni nyongeza kwenye rekodi zake.