Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Zifahamu albamu sita zake Harmonize!

Muktasari:

  • Harmonize, mwanzilishi wa Konde Music Worldwide, ameachia albamu hiyo mpya, 31 (2026) bila kujumuisha wimbo wowote uliotoka kitambo, hivyo mikwaju yote humu ni mipya kabisa.

Wikiendi iliyopita Harmonize aliwapatia mashabiki albamu mpya ambayo ilisubiriwa kwa muda mrefu ukiwa ni mradi wake sita tangu ametoka rasmi kimuziki miaka zaidi ya 10 iliyopita kupitia wimbo wake, Aiyola (2015).


Harmonize, mwanzilishi wa Konde Music Worldwide, ameachia albamu hiyo mpya, 31 (2026) bila kujumuisha wimbo wowote uliotoka kitambo, hivyo mikwaju yote humu ni mipya kabisa.

Akiwa ameipigania heshima yake kwa zaidi ya miaka sita akiwa kama mwanamuziki huru chini ya Konde Music au Konde Gang, hizi zifuatazo ni albamu zake sita ambazo ameziachia ndani ya wakati huo.

1. Afro East - 2020

Harmonize alijitahidi kuipa heshima inayostahili kama albamu yake ya kwanza ambapo uzinduzi wake ulifanyika kwa viwango ukiongozwa na Rais Mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete katika ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.

Albamu hiyo yenye nyimbo 18, ilishirikisha wanamuziki kama Lady Jaydee, Mr. Blue, Khaligraph Jones, Skales, Yemi Alade, Morgan Heritage, Phyno, Mr. Eazi na Burna Boy, mshindi wa Grammy 2021.

Hata hivyo, albamu hii kwenye baadhi ya mitandao ikiwemo Spotify inaonekana kuwa na nyimbo 17, hii ni kwa sababu wimbo 'Your Body' aliyomshirikisha Burna Boy uliondolea kwa madai ya kusampo wimbo wa Papa Wemba, Show Me the Way (1995) bila kufuata taratibu za hakimiliki.

2. High School - 2021

Hadi sasa hii ndio albamu ya Harmonize ambayo imetoka ikiwa na idadi kubwa zaidi ya nyimbo ambazo zinafika 20, na ndio albamu pekee aliyowapa nafasi wasanii aliyokuwa akiwasimamia chini ya Konde Music.

Ilikuwa miongoni mwa albamu zilizochaguliwa kuwania Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) 2021, ikiwa ni mara ya kwanza kwa Harmonize kutajwa katika tuzo hizo.

Wanamuziki walioshirikishwa ni Naira Marley, Busiwa na Sholo Mwamba, vilevile walikuwepo Ibraah na Anjella ambao ni wasanii wa kwanza Harmonize kuwasaini ndani ya Konde Music.

3. Made For Us - 2022

Ilikuwa na nyimbo 14 ambazo zilibeba miondoko mbalimbali ikiwemo Bongofleva, Afrobeats na Amapiano, muziki kutokea Afrika Kusini ambao kwa wakati ulikuwa ukivuma zaidi hapa Bongo.

Albamu hii ilitoa wimbo wake maarufu 'Nitaubeba' ambao katika video yake alitokea Kajala Masanja. Kwa sasa ni wimbo ni wake namba tano kufanya vizuri zaidi YouTube ukiwa umetazamwa mara milioni 49.

Baadhi ya wanamuziki walioshirikishwa katika albamu hii ni Abigail Chams, Bruce Melodie, Spice, Mabantu na Ntosh Gazi, mkali wa Amapiano kutokea Afrika Kusini.

4. Visit Bongo - 2023

Ni albamu yenye nyimbo 14 zikiwemo 'Single Again Remix' akimshirikisha Nkosazana Daughter kutokea Afrika Kusini, pamoja na wimbo wa utangulizi 'Zanzibar' ambao alishirikiana na Bruce Melodie kutokea Rwanda.

Albamu hiyo ilishinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) 2023 kama Albamu Bora ya Mwaka, baada ya Harmonize kuwania kipengele hicho mara mbili mfululizo bila ushindi wowote kupitia albamu ya High School (2021) na Made For Us (2022).

Kwa ujumla albamu hiyo ilishirikisha wanamuziki hao wawili tu, hivyo hakuna msanii wa Bongofleva aliyepata nafasi katika katika Visit Bongo (2023) hata wale waliokuwepo Konde Music, lebo ambayo ilianza rasmi Oktoba 2019.

5. Muziki wa Samia - 2024

Ni albamu ambayo ilijikita kuelezea mambo yaliyofanyika chini ya utawala wa Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan tangu alipoingia madarakani mwaka 2021.

Albamu hii yenye nyimbo 10, uzinduzi wake uliongozwa na Rais Samia pale Mlimani City, huku Harmonize akiwa ni mwanamuziki wa kwanza wa Bongofleva kupata heshima ya albamu yake kuzinduliwa na Rais.

Pia albamu hii ilishirikisha wanamuziki wawili tu ambao ni H. Baba na Awilo Longomba kutokea DR Congo, wote hawa walisikika katika wimbo mmoja uitwao 'Kazi Iendelee' ambao ni refix ya ngoma yao ya awali, Attitude.

6. 31 - 2026

Albamu ilipaswa kutoka mwaka uliopita ambapo Harmonize alitimiza umri wa miaka 31 lakini ikasogezwa mbele hadi Septemba 4, 2026, licha ya kuwa tarehe hiyo tayari msanii huyo alikuwa na miaka 32 bado jina lake lilibaki kuwa lile la mwanzo.

Kwa mujibu wa Harmonize, albamu hiyo yenye nyimbo 10, si albamu tu, bali ni taswira ya safari yake kimuziki, ukuaji wake, hisia zake na matukio yaliyomjenga hadi kuwa msanii tunayemuona leo.

Humu ndani Harmonize amewashirikisha wanamuziki kama Rayvanny, Marioo, Jay Melody, Yemi Alade, Mayorkun, Stonebwoy, Mohamed Ramadan, Sofiya Nzau, na Young Lunya, rapa ambaye ameshatoa naye kolabo tatu hadi kufikia sasa.