Sio Diamond tu... Hawa pia wameonja ladha ya injili
Muktasari:
- Wakati mwingi tunawazoea kwenye Bongo Fleva, wakitamba na nyimbo za mapenzi, maisha na burudani, lakini si kila mara wanabaki huko kwani Kuna muda wanahamia upande mwingine na kuimba kuhusu imani, kushukuru na kumsifu Mungu.
MOJAWAPO wa sifa ya msanii ni kubadilika. Msanii ni kama kioo cha jamii ana namna tofauti za kufikisha ujumbe kwa jamii iwe kwa furaha, huzuni lakini anachotaka hadhira ielewe ujumbe wake.
Wakati mwingi tunawazoea kwenye Bongo Fleva, wakitamba na nyimbo za mapenzi, maisha na burudani, lakini si kila mara wanabaki huko kwani Kuna muda wanahamia upande mwingine na kuimba kuhusu imani, kushukuru na kumsifu Mungu.
Hapo ndipo majina ya eakali kama Diamond Platnumz, Mbosso, Nandy, Phina na Abby Chams yanapoingia.
Baada ya kutamba sana katika Aina tofauti ya muziki wa Bongo Fleva wasanii hao walijikuta pia wakizigusa nyoyo za mashabiki wao na wale wa muziki wa Injili kwa kuimba nyimbo hizo.
Wapo walioanzia Injili kisha wakaingia kwenye Bongo Fleva, huku wengine wakianza Bongo Fleva na baadaye kugusa Injili, ina maana muziki unabadilika lakini kipaji kimebaki kilekile.
DIAMOND
Nasibu Abdul maarufu Diamond Platnumz amejenga jina kubwa kupitia Bongo Fleva na Afro-pop, lakini muziki wake mara nyingi umekuwa ukigusa maisha, mapenzi, mafanikio na imani.
Mfano mzuri ni wimbo wake wa “Yatapita”, ambao pamoja na kuwa na ladha ya Afro-pop na ujumbe wa maisha na mapenzi, una sehemu inayomtaja Mungu na imani ya kwamba changamoto zitapita.
Mwaka huu Diamond na ameshirikishwa na mwimbaji maarufu wa Injili, Joel Lwaga katika Wimbo ‘Nikumbuke’. Huo ni wimbo unaofundisha subira na kumtegemea Mungu uliotoka Septemba 23, 2026 huku mashabiki wakionyesha mapokezi makubwa kutokana muunganiko wa wanamuziki hao.
Kwa lugha nyingine, Diamond siyo msanii anayebaki kwenye aina moja ya muziki, bali anaweza kutoka kwenye upande wa burudani na kuingia kwenye ujumbe wa kiimani bila kuachana na nguvu yake ya muziki wa Bongo Fleva.
MBOSSO
Mbwana Yusuf maarufu Mbosso, sauti yake ikiwa kwenye mapenzi inaweza kukufanya uingie kwenye simulizi ya wapenzi, lakini upande wa nyimbo zenye ujumbe wa kiroho anabeba hisia za shukrani, matumaini na maisha.
Wasifu wake wa muziki pia unaonyesha mchanganyiko mpana wa ladha kama Bongo Fleva, Afro-pop, Singeli, Amapiano, Hip Hop pamoja na nyimbo za kidini, injili na Qaswida.
Aprili 2026 aliingia upande wa Injili kupitia wimbo “Mimi Ni Nani”, alioshirikishwa kundi la Burundi, Les Rachats Classic. Wimbo huo umebeba ujumbe wa unyenyekevu, toba na kumshukuru Mungu kwa neema, huku ukichanganya ladha ya Bongo Fleva.
Kwa hiyo kwa Mbosso, kuingia kwenye muziki wa kiroho si kama kuanza safari mpya kabisa ni sehemu ya uwezo wake wa kuzunguka kwenye ladha tofauti za muziki.
NANDY
Faustina Charles maarufu Nandy alianza safari yake ya muziki upande wa Injili akiwa sehemu ya kwaya kanisani, kabla ya kuingia kwenye Bongo Fleva na kujenga jina kupitia nyimbo za mapenzi na burudani.
Nandy alianza safari yake ya muziki upande wa Injili, kabla ya kuingia Bongo Fleva. Kwenye upande huo amewahi kufanya kazi kadhaa, ikiwemo Wanibariki, Umenifaa, Nipo Naye, Asante na Noel Ya Kwanza, zote zikiwa sehemu ya EP yake ya Wanibariki ya mwaka 2021. Pia aliwahi kufanya cover ya Nikumbushe Wema Wako ya Angel Benard na Mimi Ni Wa Juu ya Joel Lwaga.
PHINA
Phina ni mfano mwingine wa msanii ambaye upande wake wa muziki haukuibukia kwenye Bongo Fleva pekee.
Kabla ya kujulikana kimuziki, Phina alikuwa na uzoefu wa kuimba shuleni na kanisani akiwahi kuongoza kwaya na pia kushiriki kundi la kusifu na kuabudu (praise and worship).
Baadaye alijenga jina kwenye Bongo Fleva na Afro-pop, akija na nyimbo zilizomuweka kwenye ramani ya muziki wa Tanzania.
Kwa hiyo kuingia kwenye Injili kunaweza kutazamwa pia kama kugusa tena eneo ambalo tayari lilikuwa sehemu ya mizizi yake ya muziki. Ni kama kusema Phina wa Bongo Fleva siyo mtu mpya kwenye muziki wa kiroho bali ni sauti iliyokulia kwenye mazingira ambayo tayari yalikuwa na ladha hiyo.