Rekodi 10 Diamond akishika namba moja...!
Muktasari:
- Kwa Tanzania, hakuna ubishi kuwa Diamond ndiye mwanamuziki namba moja linapokuja suala la mafanikio ya kazi za muziki kupitia YouTube, na hizi ni rekodi zake 10 katika mtandao huo ulioanzishwa mwaka 2005.
STAA wa Bongofleva, Diamond Platnumz ni miongoni mwa wanamuziki kutokea Afrika ambao nyimbo zao zinafanya vizuri katika mtandao wa YouTube ambapo video zao zinapata mamilioni ya watazamaji.
Kwa Tanzania, hakuna ubishi kuwa Diamond ndiye mwanamuziki namba moja linapokuja suala la mafanikio ya kazi za muziki kupitia YouTube, na hizi ni rekodi zake 10 katika mtandao huo ulioanzishwa mwaka 2005.
1. Diamond ndiye mwanamuziki wa kwanza wa Bongofleva ambaye wimbo wake ulitazamwa mara nyingi zaidi YouTube ndani ya muda mfupi mara baada tu ya video yake kuachiwa. Ni kupitia video ya wimbo wake na Koffi Olomide kutokea nchini DR Congo, Waah! (2020) ambayo ilitazamwa mara milioni 1 ndani ya saa nane pekee.
2. Diamond ndiye msanii pekee wa Bongofleva ambaye hajawahi kutoa video rasmi ya wimbo wake halafu isitazamwe walau mara milioni 1 YouTube. Yaani hana wimbo ambao video yake haijafikisha walau views milioni 1.
3. Diamond ndiye mwanamuziki wa kwanza wa Bongofleva kwa kazi zake kutazamwa (views) mara bilioni 1 YouTube, kisha wakafuatia Rayvanny, Harmonize, Zuchu na Mbosso. Hao ndio wasanii pekee kwa hapa Bongo waliofikisha views zaidi ya bilioni 1 YouTube, na wote wamesimamiwa na Diamond kimuziki kupitia rekodi lebo yake ya WCB Wasafi.
4. Wimbo wa kwanza wa staa wa Nigeria, Mr Flavour kutazamwa mara milioni 100 YouTube, ni ule aliyomshirikisha Diamond, Time To Party (2018) ikiwa ni kolabo ya pili kufikia namba hizo kati ya tatu walizofanya hadi sasa.
5. Diamond ndiye mwanamuziki wa kwanza kusini mwa jangwa la Sahara kupokea tuzo kutokea YouTube ijulikanayo kama Diamond Creator Award, na alikabidhiwa tuzo hiyo katika makao makuu ya mtandao huo nchini Marekani. Tuzo hiyo hutolewa kwa mtengeneza maudhui ambaye chaneli yake ya YouTube imefikisha wafuatiliaji au wafuasi (subscribers) milioni 10. Kwa sasa Diamond amefikisha subscribers milioni 11.9.
6. Hadi sasa Diamond ana video 20 za nyimbo zake ambazo zimeshatazamwa YouTube zaidi ya mara milioni 50, akiwa ndiye mwanamuziki pekee wa Bongofleva na Afrika Mashariki kwa ujumla mwenye rekodi hiyo.
7. Diamond ndiye msanii wa kwanza wa Bongofleva kuwa na video sita ambazo zimetazamwa YouTube mara milioni 100. Wanaomfutia ni Rayvanny na Zuchu ambao kila mmoja ana video mbili yenye views milioni 100.
8. Video sita za Diamond zenye views zaidi ya milioni 100 YouTube ni za nyimbo hizi zifuatazo; Yope Remix (2019), Inama (2019), Waah! (2020), Nana (2015), Jeje (2020) na African Beauty (2018).
9. Diamond ndiye msanii pekee ambaye nyimbo nyingi alizoshirikishwa na wasanii wenzake wa Bongofleva, video zake zimekuwa namba moja kwa kutazamwa YouTube kwa muda wote kwa wasanii hao. Diamond amefanya hivyo kwa Chege (Waache Waoane), Linex (Salima), Harmonize (Kwangwaru), Navy Kenzo (Katika), Jux (Enjoy), G Nako (Komando), Barnaba (Salama), AY (Zigo Remix) na kadhalika.
10. Diamond ndiye mwanamuziki wa kwanza Afrika kwa video zake kutazamwa YouTube mara bilioni 2, na wa pili kwa video zake zimetazamwa mara bilioni 3, akiwa ametanguliwa na mshindi wa Grammy kutokea Nigeria, Burna Boy. Hadi sasa Burna Boy kazi zake zimetazamwa mara bilioni 4 YouTube, huku Diamond akiwa na bilioni 3.8. Burna Boy akiwa ametoa albamu nane, wakati Diamond akiwa ametoa albamu tatu pamoja na Extended Playlist (EP) moja.