Professor Jay kawashika wengi mkono
Muktasari:
- Mbali na yote, sifa nyingine ya Professor Jay ni jinsi alivyowasaidia wasanii wengine au kushirikiana nao kwa lengo la kusonga mbele kwa pamoja kama ifuatavyo.
Tangu akiwa na kundi la Hard Blasters Crew (HBC) hadi aliposimama peke yake, Professor Jay ametumia sanaa yake vizuri akifikisha ujumbe wenye maudhui ya kuisaidia kijamii kwa sehemu kubwa.
Mbali na yote, sifa nyingine ya Professor Jay ni jinsi alivyowasaidia wasanii wengine au kushirikiana nao kwa lengo la kusonga mbele kwa pamoja kama ifuatavyo.
1. Siku ya kwanza tu Professor Jay alipokutana na AY katika ofisi ya HBC alimweleza anaukubali wimbo wake 'Ni Raha Tu', kisha akamwambia aende kwa P-Funk Majani akarekodi wimbo 'Nawakilisha' walioshirikiana.
Wimbo 'Nawakilisha' ulikutanisha wasanii watano ambao ni Professor Jay, Black Rhino, Adili Chapakazi, Complex na AY aliyechana vesi ya mwisho.
2. Professor Jay aliombwa kushiriki katika wimbo wa Tundaman, Neila (2006) ila akampendekeza Chid Benz ambaye alikubali, basi wimbo akarekodiwa Baucha Records kwa Bob Manecky na ulipotoka ukafanya vizuri.
3. Chid Benzi alitii pendekezo la Professor Jay kwa sababu walikuwa na ukaribu wa kikazi. Chid aliwahi kuwa msaidizi wa Jay jukwaani na walizunguka pamoja katika show mbalimbali kitu kilichomjenga kimuziki.
4. Mistari yote aliyoimba Lady Jaydee katika wimbo 'Nimeamini' kutoka katika albamu ya tatu ya Professor Jay, J.O.S.E.P.H (2006) ameandikiwa kwa sababu za kiufundi zaidi na siyo kwamba hajui kuandika.
Professor Jay alimwandikia kutokana na wimbo huo ni wa majibizano katika mtindo wa rap, hivyo akachukua jukumu hilo kwa sababu ametamba na rap tangu mwaka 1995 alipojiunga na HBC.
5. Kutokana na ushirikiano wao kimuziki kwa miaka mingi na mapambano mengine ya kisanaa, Lady Jaydee anawataja Professor Jay na Mr. II Sugu kama ndugu zake sasa na si marafiki tena.
6. Tayari Lady Jaydee ameshiriki katika nyimbo za Sugu kama 'Mambo ya Fedha' na 'Muda Mrefu', huku kwa Professor Jay zikiwa ni 'Bongo Dar es Salaam', 'Ndio Mzee' na 'Nimeamini'.
7. Ni Professor Jay na Sugu ambao wameshirikiana katika wimbo 'Inatosha' kutoka katika albamu, J.O.S.E.P.H (2006). Katika wimbo huu ameeleza baadhi ya mambo ambayo hayapaswi kuwepo katika Bongo Fleva.
8. Ziara ya kwanza ya AY kimuziki alipewa nafasi ya Professor Jay, ni katika ziara ya albamu yake ya kwanza, Machozi Jasho na Damu (2001), na hapa ndipo AY alipozunguka sana nchini kwa mara ya kwanza.
9. Kundi la Wagosi wa Kaya wakati linataka kurekodi kwa mara ya kwanza, lilienda ofisi aliyokuwa anafanyia kazi Professor Jay huko Tanga na kumwomba awaelekeze zilipo studio za MJ Production, sasa MJ Records.
10. Basi Professor Jay akachukua kalamu na karatasi na kuwachorea ramani ya kufika katika studio hizo jijini Dar es Salaam na kuwaelekeza waende kuonana na Prof. Ludingo.
Huyu Prof. Ludingo ndiye alitengeneza midundo yote ya albamu ya kwanza ya HBC iliyorekodiwa MJ Records, Funga Kazi (2000) ambayo ilikuwa na nyimbo kali kama Mamsapu na Chemsha Bongo.