Lava Lava avunja ukimya nyumba ya mama yake
Muktasari:
- Msanii huyo amesema hajawahi kuishi maisha ya kufeki na haelewi kwa nini baadhi ya watu wanashindwa kuamini maendeleo anayoyafanya.
BAADA ya picha na video zinazoonyesha nyumba aliyodai kumjengea mama yake kusambaa kwa kasi mitandaoni, mwanamuziki wa Bongo Fleva, Lava Lava, ameamua kuvunja ukimya na kujibu wanaotilia shaka mafanikio yake.
Msanii huyo amesema hajawahi kuishi maisha ya kufeki na haelewi kwa nini baadhi ya watu wanashindwa kuamini maendeleo anayoyafanya.
Utata huo ulianza baada ya Lava Lava kuposti kwenye ukurasa wake wa Instagram picha na video za nyumba hiyo akimuonyesha mama yake, hatua iliyopokelewa kwa pongezi na mashabiki wengi. Hata hivyo, muda mfupi baadaye baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii waliibua mjadala wakidai huenda nyumba hiyo si ya Lava Lava au si yeye aliyeigharamia, huku wengine wakimtaka kutoa ushahidi zaidi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Lava Lava alisema ameshangazwa na namna watu wanavyokuwa wepesi kutilia shaka kila anachofanya, akisisitiza kuwa hajawahi kujijengea jina kwa kuonyesha maisha ya uongo.
"Mimi sina tabia ya kufeki maisha. Kwa nini watu wanashindwa kuniamini? Au ukimya wangu ndiyo unawafanya waone siwezi kufanya kitu cha maendeleo?" amesema Lava Lava.
Msanii huyo amesema si mtu anayependa kutangaza kila hatua ya maisha yake binafsi, akieleza kuwa kuna mambo mengi amekuwa akiyafanya kimya kimya bila kuyaweka hadharani. Aliongeza kuwa kitendo cha kumpatia mama yake makazi bora ni sehemu ya ndoto alizokuwa nazo kwa muda mrefu na hakukifanya ili kupata sifa kutoka kwa watu.
"Si kila jambo lazima nilitangaze. Kuna mengi nimekuwa nikifanya kimya, ila nikiamua kushare jambo moja ndiyo linaanza kuhojiwa. Hilo linanishangaza," amesema.
Lava Lava alijiunga na WCB Wasafi mwaka 2015, ambako alijizolea umaarufu kupitia nyimbo kama Tuachane, Saula, Go Gaga, Tekenya na nyingine zilizomfanya kuwa miongoni mwa wasanii tegemeo wa lebo hiyo.
Baada ya kuitumikia WCB kwa takribani miaka tisa, aliondoka mwaka 2025 na kuamua kuendelea na safari yake ya muziki akiwa huru.
Tangu aondoke WCB, Lava Lava amekuwa akisimamia kazi zake kupitia upande wake binafsi, akitoa nyimbo na kufanya maonyesho ndani na nje ya Tanzania, ingawa amekuwa si mzungumzaji sana wa maisha yake binafsi tofauti na ilivyokuwa awali. Ukimya wake huo ndiyo ambao baadhi ya wadau wamekuwa wakiutafsiri kama kushuka kwa mafanikio, jambo ambalo yeye analipinga.
Kwa upande wa mashabiki, wapo waliompongeza kwa kumuenzi mama yake kwa kumjengea nyumba, wakisema mafanikio ya msanii hupimwa pia kwa namna anavyowakumbuka wazazi wake. Hata hivyo, wengine wameendelea kubaki na mashaka, wakidai ni kawaida kwa baadhi ya watu maarufu kuposti mali ambazo si zao, hali iliyochochea mjadala mkubwa kwenye Instagram, YouTube na majukwaa mengine ya burudani.
Licha ya mjadala huo kuendelea, Lava Lava amesema hana mpango wa kubishana na mtu yeyote kuhusu mafanikio yake. Kwake, jambo la muhimu ni kuona mama yake anaishi maisha bora, huku akiamini muda utaendelea kuthibitisha kuwa maendeleo yake ni ya kweli na si sehemu ya maigizo ya mitandaoni.