Ndoa ya Wolper, Rich Mitindo yazua utata
Muktasari:
- Kauli hiyo imekuja baada ya miezi kadhaa iliyopita wawili hao kuonekana pamoja na kuzua maswali kama wamerudiana.
KWA mara nyingine, ndoa ya mwigizaji wa filamu Bongo, Jacqueline Wolper na Rich Mitindo, imeibua mjadala baada ya Wolper kuweka wazi walishaachana kitambo, huku akisisitiza kilichobaki kati yao ni jukumu la kulea watoto wao.
Kauli hiyo imekuja baada ya miezi kadhaa iliyopita wawili hao kuonekana pamoja na kuzua maswali kama wamerudiana.
Akizungumza na Mwanaspoti, Wolper alisema watu wengi wamekuwa wakichanganya ukaribu wao wa kifamilia na kudhani bado wanaishi kama mume na mke, jambo ambalo si la kweli.
Alisisitiza kuwa walimaliza uhusiano wao wa ndoa muda mrefu uliopita na kwa sasa wanashirikiana kwa jambo moja tu, malezi ya watoto wao.
"Tulishaachana kitambo, kilichobaki kati yetu ni watoto. Lazima tushirikiane kwa ajili yao, lakini hilo lisitafsiriwe kwamba bado tupo kwenye ndoa," alisema Wolper.
Mbali na mazungumzo yake na Mwanaspoti, hivi karibuni Wolper pia alizungumza kwenye mahojiano ya podcast ya A-List, ambapo aliweka wazi kuwa kwa sasa ameendelea na maisha yake na yupo kwenye mahusiano mengine.
Katika mahojiano hayo, pia alisema moja ya sababu zilizochangia kuvunjika kwa ndoa yao ni usaliti, huku akieleza kuwa alijitahidi kuiokoa ndoa hiyo lakini haikuwezekana.
Licha ya kueleza maumivu aliyopitia, Wolper hakusita kumpa heshima Rich Mitindo kama baba wa watoto wake, akisema pamoja na tofauti zao, bado anatimiza wajibu wake wa ulezi na hilo ni jambo analoliheshimu.
"Rich ni baba mzuri wa watoto wangu. Hilo siwezi kulifuta kwa sababu tu hatupo tena kwenye ndoa. Kikubwa sasa ni kuhakikisha watoto wanapata malezi bora kutoka kwetu sote."
Kauli hizo zimeibua mjadala kutokana na historia ya uhusiano wao.
Mwanzoni mwa Januari 2025, Wolper alitangaza kupitia ukurasa wake wa Instagram kuwa ameachana na Rich Mitindo na alikuwa kwenye mchakato wa talaka. Baadaye aliliambia Mwanaspoti kuwa uamuzi huo haukuwa wa kutafuta kiki, bali ulikuwa wa kweli baada ya kupitia changamoto nyingi ndani ya ndoa yao.
Hata hivyo, mwezi mmoja baadaye, Februari 2025, Wolper aliliambia tena Mwanaspoti kuwa walikuwa wamesameheana na kurudiana, akieleza kuwa migogoro ndani ya ndoa ni jambo la kawaida na waliona ni busara kuipa nafasi familia yao. Kauli hiyo iliwafanya wengi kuamini kuwa tofauti zao zilikuwa zimemalizika.
Miezi iliyofuata, wawili hao waliendelea kuonekana pamoja kwenye matukio mbalimbali ya kifamilia, jambo lililozima uvumi wa kuachana. Hata hivyo, safari hii Wolper amesema hakuna kurejeana tena, huku akisisitiza kuwa kila mmoja ameendelea na maisha yake na kilichobaki ni kuheshimiana kama wazazi.
Kwa upande wake, Rich Mitindo, alipotafutwa na Mwanaspoti kuzungumzia kauli hizo, hakutaka kuingia kwa undani kuhusu maisha yake ya ndoa. Alisema si mtu anayependa kuzungumzia masuala ya familia hadharani.
"Mimi ni mtu wa kukaa kimya, sipendi kuzungumzia mambo ya familia kwenye vyombo vya habari, kikubwa ni kumuomba Mungu kila mmoja aendelee na uzima wa afya vizuri," alisema Rich.
Wolper na Rich Mitindo walianza uhusiano wao miaka kadhaa iliyopita kabla ya kufunga ndoa ya kifahari Novemba 19, 2022, katika Kanisa la St. Peter's jijini Dar es Salaam.
Ndoa hiyo ilihudhuriwa na mastaa mbalimbali wa filamu, muziki na wafanyabiashara, huku wawili hao wakitajwa kuwa miongoni mwa wanandoa waliokuwa wakivutia macho ya wengi kutokana na namna walivyokuwa wakioneshana mapenzi hadharani.
Sasa, baada ya kauli mpya za Wolper, ndoa yao imeibua mjadala upya. Wapo wanaoamini safari hii ndiyo mwisho wa ukurasa huo, huku wengine wakikumbuka matukio ya awali ambapo walitangaza kuachana lakini baadaye wakapatanishwa. Hata hivyo, kwa mujibu wa Wolper, msimamo wake wa sasa ni kwamba ndoa hiyo imebaki kuwa historia, huku jukumu lao kubwa likiwa ni kulea watoto wao kwa ushirikiano.