Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

PIMBI: Uchambuzi wa muziki, kesi, ukaribu na staa

Muktasari:

  • Mwanaspoti limefanya mahojiano na Pimbi, ambaye amezungumzia jinsi uchambuzi wa muziki unavyomlipa, lakini wakati mwingine hujikuta akikabiliwa na changamoto za kufikishwa mahakamani kutokana na baadhi ya wasanii kuona kuwa anawadhalilisha.

MSANII wa tamthilia, mchekeshaji na mchambuzi wa muziki, Meya Shabani Mpozemenya ‘Pimbi’, amesema kazi anazofanya zina ujumbe unaoelezea mahitaji ya watu wafupi na huduma za kijamii, huku akiviwasilisha kwa njia ya vichekesho.

Mwanaspoti limefanya mahojiano na Pimbi, ambaye amezungumzia jinsi uchambuzi wa muziki unavyomlipa, lakini wakati mwingine hujikuta akikabiliwa na changamoto za kufikishwa mahakamani kutokana na baadhi ya wasanii kuona kuwa anawadhalilisha.

“Kazi ya sanaa bila ubunifu huwezi kufika popote. Lazima ufikirie namna ya kuendana na nyakati, kujua mashabiki wanataka nini na hawataki nini. Kazi zangu zote ninazozifanya hazitaki mazoea,” anasema Pimbi, ambaye ni shabiki damu wa Simba.


UCHAMBUZI UNAZINGATIA HAYA

Akielezea mambo muhimu yanayotakiwa kuzingatiwa katika uchambuzi, anasema jambo la kwanza ni kuweka uhalisia wa mambo. Ametolea mfano wa gharama za kutengeneza wimbo hadi unapokamilika, akisema kutokana na uzoefu wake, anaona wasanii wengi wakitaja gharama zisizo halisi.

“Kwa sasa wasanii wamepunguza kuongeza kiwango cha pesa. Unakuta video ametengeneza kwa Sh10 milioni, lakini anaanza kusema Sh100 milioni. Jambo hilo si zuri kwa sababu ni kuwadanganya Watanzania. Hivyo, tunakuwa tunachambua ubora ili kumpa mtazamaji uhalisia,” anasema Pimbi na kuongeza:

“Jambo lingine tunaloangalia ni ujumbe uliopo kwenye wimbo, maneno yaliyotumika, maudhui kwa ujumla, matumizi ya vyombo kama gitaa, ngoma na vinanda, kazi ya produsa na ya mwongozaji. Lengo la yote hayo ni kuwakumbusha wasanii wasijisahau na kuwapa moyo wale wanaofanya vizuri.

“Ikiwa kazi ni nzuri, lazima tutasema ni nzuri. Nina uhakika msanii anayetaka kufika mbali hawezi kuacha kuboresha kazi zake anapopata nafasi ya kukosolewa.”

Anasema mke wake amekuwa msaada mkubwa kwake kwa kumpa sapoti katika kazi na maisha ya kawaida.

“Nyumbani kwangu nina studio ndogo ninayotumia kufanya kazi zangu. Hivyo, ninapokuwa nimefanya uchambuzi kwa upendeleo, anausikiliza na kuniambia nilipokosea ili nirekebishe na kuendelea,” anasema Pimbi.


CHANGAMOTO

Anasema kabla ya kupata mwanasheria wa kumwelekeza mambo yanayotakiwa na yasiyotakiwa katika uchambuzi wake, alikuwa akijikuta akipelekwa mahakamani mara kwa mara. Aliwahi pia kulipa kiasi kikubwa cha fedha kama fidia na gharama za kushughulikia kesi.

“Mwanasheria aliniambia nisichambue kwa hisia wala ushabiki, nisikashifu watu, nielezee muziki kama muziki na nitoe maoni yangu, jambo ambalo kisheria kila Mtanzania ana uhuru wa kufanya.

“Baada ya kupata mwanasheria anayeniongoza, hata ninapokwenda mahakamani kwa sasa nimekuwa nikishinda kesi,” anasema Pimbi na kuongeza:

“Moja ya kesi nilizoshinda ni ile niliyoshitakiwa na msanii wa Bongo Fleva, Marioo, baada ya kutangazwa mshindi wa jumla wa tuzo za TMA. Mimi nilisema kuwa mwaka 2023, Diamond Platnumz na Harmonize walikuwa na nyimbo bora zilizofanya vizuri. Nilidhani mmoja wao angechukua tuzo ya mshindi wa jumla, lakini Marioo akanishitaki kwa kosa la kuchafua chapa yake. Hata hivyo, nilishinda baada ya kubainika kuwa sikumkashifu mtu,” anasema na kuongeza:

“Kwa sasa mimi na Marioo ni marafiki. Juzi, baada ya kurejea kutoka Marekani, ambako alishinda tuzo za Afrima, alinialika kwenda kusherehekea pamoja naye.”

Anasema miongoni mwa wasanii ambao hawachukii anapowachambua ni Diamond Platnumz, ambaye huchukulia uchambuzi huo kama kazi nyingine, na Harmonize, ambaye wakati mwingine hukwazika, lakini bila kufikia kiwango cha kuwa na chuki kama ilivyo kwa baadhi ya wasanii wengine.

“Ukaribu wangu na Diamond Platnumz ulitokana na uchambuzi ninaoufanya. Ananishauri njia nzuri za kupita ili niweze kufika mbali. Ananialika katika matukio ya familia yake na shoo zake za ndani na nje ya nchi. Watu waliokaa na jamaa huyo wanajua ana upendo wa hali ya juu, tofauti na anavyochukuliwa kwenye mitandao ya kijamii, ambako huonekana kama mtu katili.

“Uchambuzi huo kwa sasa unalipa na vijana wengi wamejiingiza katika kazi hiyo, wakijipatia kipato. Jambo la msingi zaidi ni kuwa na ushawishi mkubwa kwenye mitandao yao na kupata matangazo kama ambavyo wengine tumepata na kunufaika nayo.”


VIDEO YA MWIJAKU

Akizungumzia video iliyowekwa mtandaoni na influensa na mtangazaji, Mwemba Burton ‘Mwijaku’, ikimuonyesha Pimbi akiwa na miguu iliyochafuka, anasema:

“Nilikuwa Sabasaba, nilikwenda kutangaza biashara za wateja wangu. Nilitumia muda mrefu kuzunguka mle ndani, hivyo nilikuwa nimechoka na miguu yangu ilikuwa imechafuka. Nilionekana kama mtu aliyechoka na asiye na lolote. Nilipoona Mwijaku ameiposti video hiyo, nilichukulia kuwa anafanya kontenti, kwa sababu mtu anapokuwa maarufu, hata jambo dogo linaweza kuwa kubwa.”

Akizungumzia upande wa komedi, anasema anazopenda na zinazoishi kwa muda mrefu ni zile zinazotumia vitendo kuliko maneno yanayotegemea misimu inayobadilika.

“Nilitengeneza video nikiwa chooni, nimekwenda kujisaidia haja ndogo, lakini vyoo vya wanaume vya kusimama vilikuwa virefu kwangu. Licha ya kuchekesha, ujumbe wangu ulikuwa kwa wamiliki wa hoteli na wanaotengeneza vyoo vya umma, kujaribu kutengeneza vyoo vinavyofaa watu wafupi na wenye ulemavu,” anasema Pimbi na kuongeza:

“Niliwahi kukumbwa na changamoto hiyo. Nilikuwa sifiki, ikabidi nijisaidie kando ya choo, jambo ambalo si ustaarabu na linasababisha uchafuzi wa mazingira. Changamoto nyingine ni kwamba ukienda hotelini, sehemu wanapoweka sabuni au sehemu za kuweka vifaa vingine hazitupi nafasi nzuri sisi watu wafupi. Hata kwenye milango, wakati mwingine unaweza kusimama kwa kunyanyua visigino ili uweze kuufungua.”

Pimbi anasema amejaaliwa kupata watoto watatu. Mtoto wake wa kwanza anaitwa Shaban, mwenye umri wa miaka tisa, anayependa kucheza mpira wa miguu na ni shabiki wa Yanga. Watoto wengine ni Nizar, mwenye umri wa miaka sita, na Naiya.nye umri wa miaka mitatu, hao wanapenda anachokifanya na anaamini huenda huko mbeleni wakiamua kuchagua sanaa watafanya vizuri.