Msondo, Twanga, Bogoss kutikisa Salute 5
Muktasari:
- Kundi hilo lililoanzishwa mwaka 2016 na mpenzi wa muziki wa dansi, Said Mdoe, sasa limejijengea heshima kubwa miongoni mwa wadau wa muziki huo kutokana na uwezo wake wa kuwakutanisha mashabiki, wanamuziki na wadau mbalimbali wa dansi kwenye mijadala na shughuli za kijamii.
KATIKA kipindi ambacho muziki wa dansi unaendelea kurejesha taratibu mvuto wake kwa mashabiki wa kizazi kipya, kundi la WhatsApp la Salute 5 limeendelea kuwa moja ya majukwaa yanayobeba nguvu kubwa ya kuuenzi na kuukuza muziki huo hapa nchini.
Kundi hilo lililoanzishwa mwaka 2016 na mpenzi wa muziki wa dansi, Said Mdoe, sasa limejijengea heshima kubwa miongoni mwa wadau wa muziki huo kutokana na uwezo wake wa kuwakutanisha mashabiki, wanamuziki na wadau mbalimbali wa dansi kwenye mijadala na shughuli za kijamii.
Safari hiyo sasa inaenda kushuhudia kilele kingine baada ya kundi hilo kuandaa pati maalumu ya muziki wa dansi itakayowakutanisha mashabiki pamoja na bendi mbalimbali kongwe na maarufu nchini.
Katika tukio hilo, bendi za Msondo Ngoma, Twanga Pepeta na Bogoss Musica zinatarajiwa kuwa sehemu ya burudani kubwa itakayopambwa pia na Swahili Classic Band huku wasanii Jimmy Manzaka na Ashura Kitenge wakitarajiwa kuongeza hamasa ya usiku huo wa dansi.
Akizungumza kuhusu kundi hilo, Mdoe alisema Salute 5 ilianzishwa kwa lengo la kuwakutanisha watu wenye mapenzi ya muziki wa dansi na kujenga urafiki kupitia burudani.
“Tulianza kama kundi la kawaida la mashabiki wa dansi, lakini kadri muda ulivyokwenda watu wakaendelea kuongezeka na kuwa familia moja kubwa inayopenda muziki huu,” anasema Mdoe.
JUKWAA LA MIJADALA YA DANSI
Kwa miaka kadhaa sasa, Salute 5 imekuwa sehemu ya mijadala mbalimbali inayohusu muziki wa dansi, historia ya bendi kongwe pamoja na maendel eo ya muziki huo katika kizazi cha sasa.
Kupitia kundi hilo, mashabiki wamekuwa wakibadilishana mawazo kuhusu nyimbo za zamani, ubora wa wanamuziki na namna ya kuhakikisha muziki wa dansi unaendelea kuwa hai.
Mdoe anasema moja ya jambo analojivunia ni kuona kundi hilo likiwa sehemu ya kurejesha hamasa ya dansi kwa mashabiki wengi.
“Kwa karibu miaka 10, Salute 5 imekuwa jukwaa la hoja zenye tija kuhusu muziki wa dansi. Tunaamini mchango wetu umeongeza nguvu ya muziki huu kuendelea kupendwa,” anasema.
Kwa mujibu wa wadau mbalimbali wa muziki huo, makundi kama Salute 5 yamekuwa msaada mkubwa katika kuwakutanisha mashabiki waliokuwa wamepotezana kutokana na mabadiliko ya teknolojia na mitindo mipya ya muziki.
TAMASHA LA MASHABIKI
Mbali na mazungumzo ya kila siku mtandaoni, Salute 5 sasa imeamua kupeleka nguvu hiyo kwenye matukio ya moja kwa moja kupitia tamasha hilo ambalo limeandaliwa kwa ushirikiano wa wanachama wa kundi hilo.
Mdoe anasema wanachama wamechangishana fedha kwa viwango tofauti ili kuhakikisha tukio hilo linafanikiwa na mashabiki wanapata burudani bora bila gharama ya kiingilio.
“Hii ni zawadi kwa mashabiki wa dansi. Wanachama wamejitolea kuhakikisha watu wanapata nafasi ya kufurahia muziki huu bure huku tukijenga mshikamano wetu,” anasema.
Mbali na burudani kutoka kwa bendi mbalimbali, tukio hilo pia litakuwa na shughuli nyingine za kijamii zikiwemo kukata keki huku mashabiki wakipata nafasi ya kufahamiana zaidi.
MITANDAO YABEBA DANSI
Ukuaji wa Salute 5 unaonyesha namna ambavyo mitandao ya kijamii imekuwa na mchango mkubwa katika kuendeleza muziki wa dansi ambao kwa miaka mingi ulionekana kupoteza mvuto mbele ya muziki wa kizazi kipya.
Kupitia vikundi vya mtandaoni, video za nyimbo za zamani, kumbukumbu za wanamuziki pamoja na taarifa za matamasha zimeendelea kuwafikia mashabiki wengi zaidi wakiwemo vijana ambao hawakupata nafasi ya kushuhudia enzi za dhahabu za dansi.
Kwa sasa, dansi inaonekana kurejea kwa kasi huku matamasha yake yakianza kuvutia tena mashabiki wa rika tofauti.
Kwa Salute 5, hiyo inaonekana kuwa sehemu ya dhamira yao ya kuhakikisha muziki wa dansi unaendelea kuishi na kuunganisha watu kupitia burudani.
WASANII WAFUNGUKA
Mwanamuziki wa dansi, Luiza Mbutu amesema mashabiki wa muziki wa dansi wanapaswa kujitokeza kwa wingi kwenye tamasha la Salute 5 litakalofanyika Juni 1, 2026, katika Ukumbi wa Suma JKT Mwenge, akieleza kuwa maandalizi yamekamilika na burudani ya kiwango cha juu inatarajiwa kutolewa jukwaani.
“Hii ni shoo maalumu kwa wapenda muziki wa dansi, tumewaandalia burudani nzuri na kila bendi imejipanga kuhakikisha mashabiki wanapata kitu cha tofauti,” anasema Luiza.
Kwa upande wake, Nyoshi El Saadat wa bendi ya Bogoss Musica amesema Salute 5 ni jukwaa muhimu la kuendeleza muziki wa dansi nchini huku akiahidi mashabiki kupata ladha ya kipekee kutoka kwa bendi yake siku hiyo.
“Bogoss Musica tupo tayari kuwapa watu burudani ya nguvu, mashabiki waje waone kazi kubwa ambayo tumeiandaa kwa ajili yao,” anasema Nyoshi.
Juma Katundu kutoka bendi ya Msondo Ngoma amesema tamasha hilo litakuwa nafasi ya kuonyesha ubora na ushindani wa muziki wa dansi, huku akiwataka mashabiki wa muziki huo kutokukosa tukio hilo litakalofanyika Suma JKT Mwenge.
“Msondo Ngoma ipo vizuri na tumejipanga kuhakikisha mashabiki wetu wanaburudika usiku mzima,” anasema Katundu.