Nandy autaka mpambano na Zuchu
Muktasari:
- Nandy alianza kujulikana zaidi kwenye muziki baada ya kushiriki mashindano ya Tecno Own The Stage mwaka 2015, huku Zuchu akianza safari yake rasmi ya muziki chini ya WCB Wasafi mwaka 2020 kabla ya kufanikiwa kuvunja rekodi mbalimbali ndani ya muda mfupi.
MSANII wa Bongo Fleva, Nandy amesema yuko tayari kupambanishwa na Zuchu ambaye wamekuwa wakijadiliwa sana katika mitandao ya kijamii.
Kwa miaka takriban sita, wawili hao wamekuwa wakishindanishwa nani mkali kati yao na Nandy amesema hana tatizo na hilo kwani wao ni wasanii na wanafanya muziki na kila mmoja ana nafasi yake kwenye tasnia hiyo.
“Kama watu wanataka kuona mpambano kati yangu na Zuchu mimi niko tayari, maana mwishowe sisi sote tunafanya muziki na mashabiki ndiyo wanaamua,” amesema Nandy.
Kwa miaka kadhaa, mashabiki wa wasanii hao wamekuwa wakiwalinganisha kutokana na mafanikio yao, uwezo wao wa kutoa ngoma kali pamoja na nguvu kubwa waliyonayo kwenye mitandao ya kijamii na majukwaa ya muziki.
Wapo waliokuwa wakiamini Nandy alikuwa akilikwepa suala hilo kimya kimya, huku Zuchu akiendelea kutajwa mara nyingi zaidi kila ilipoibuka mijadala ya wasanii wa kike wanaotikisa Bongo Fleva kwa sasa.
Hata hivyo, kauli ya Nandy imeonekana kubadili kabisa upepo na kuongeza moto wa mjadala huo, huku mashabiki wengi wakianza kutengeneza mijadala mipya kuhusu nani mwenye uwezo mkubwa zaidi kati yao.
Baadhi ya wachambuzi wa burudani wanaamini ushindani huo unaweza kuleta chachu mpya kwenye muziki wa wanawake Tanzania kutokana na kila mmoja kuwa na mashabiki wengi pamoja na mafanikio makubwa kwenye kazi zao.
Kwa upande wa mafanikio, Nandy ameendelea kufanya vizuri na nyimbo na maonyesho mbalimbali ndani na nje ya Tanzania, huku Zuchu naye akiendelea kuwa mmoja wa wasanii wa kike wenye ushawishi mkubwa kwenye muziki wa kizazi kipya Afrika Mashariki.
Nandy alianza kujulikana zaidi kwenye muziki baada ya kushiriki mashindano ya Tecno Own The Stage mwaka 2015, huku Zuchu akianza safari yake rasmi ya muziki chini ya WCB Wasafi mwaka 2020 kabla ya kufanikiwa kuvunja rekodi mbalimbali ndani ya muda mfupi.