MIMI MARS: Muziki wangu sasa utazungumza
Muktasari:
- Wimbo huo ulitoka miezi michache baada ya albamu yake ya kwanza, ‘17’, baada ya changamoto, ikiwemo ajali ya gari.
MWANAMUZIKI wa Bongofleva, Marianne Namshali Mdee ‘Mimi Mars’ amerejea baada ya kuachia wimbo mpya unaokwenda kwa jina la Yeye aliomshirikisha Abdul Hamisi Mtambo 'D Voice' wa WCB Wasafi.
Wimbo huo ulitoka miezi michache baada ya albamu yake ya kwanza, ‘17’, baada ya changamoto, ikiwemo ajali ya gari.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mimi Mars anasema majina ya wasanii yanaweza kuwavutia watu kuusikiliza wimbo, lakini ubora wa muziki na kuelewana studio ndivyo vinavyowafanya waendelee kuufuatilia.
“Majina yanaweza kufanya watu wabofye nyimbo wasikilize, lakini kinachowafanya waendelee kusikiliza ni vibe la muziki wenyewe,” anasema.
17, ALBAMU ILIYOMFUNUA ZAIDI
Juni 19, mwaka huu, Mimi Mars aliachia albamu yake ya kwanza, ‘17’, yenye nyimbo 15. Mradi huo ulifuata EP zake mbili, ‘The Road’ (2018) na ‘Christmas with Mimi Mars’ (2021). Aliwashirikisha Cici na Lady Zamar pamoja na Itare wa Tanzania, akiwachagua kutokana na upekee wao kimuziki.
Anasema albamu imesaidia mashabiki kumfahamu zaidi, huku ikimpa nafasi ya kujaribu mitindo mipya na kuonyesha uwezo wake wa kuandika nyimbo mwenyewe.
ALBAMU INA NAFASI YAKE
Mimi Mars anaamini albamu bado ni muhimu licha ya wasanii wengi kujikita katika kutoa single. Anasema wimbo mmoja unaweza kumletea msanii umaarufu, lakini albamu humpa nafasi ya kujieleza na kujenga utambulisho.
Pia anapinga madai kwamba wasanii wa kike hawapendani. Anasema watu huangazia tofauti zao kuliko namna wanavyosaidiana. Anaamini muziki hauna jinsia na wasanii wanapaswa kushirikiana wanapoweza kutengeneza kazi nzuri.
AJALI ILIBADILI SAFARI
Desemba 2023, Mimi Mars alipata ajali ya gari iliyomlaza hospitalini kwa zaidi ya wiki tatu. Alipata majeraha makubwa kichwani na kovu usoni. Alijitenga na shughuli za sanaa, akakataa baadhi ya nafasi za uigizaji na matangazo, huku akijiuliza kama angeweza kurejea.
Anasema kutengeneza ‘17’ kulimsaidia kujiamini, kujaribu mambo mapya na kugundua uwezo wake wa kuandika nyimbo mwenyewe.
HATAPOA TENA?
Baada ya ‘17’ na ‘Yeye’, Mimi Mars anataka kuendelea kutoa kazi mpya bila kushindana na kasi ya wasanii wengine. Anasisitiza ubora ni muhimu kuliko wingi na hataki kutoa nyimbo kwa sababu tu wengine wanafanya hivyo.
Anataka kila kazi anayoitoa iwe anaipenda na kuiamini, huku akiendelea kuwa karibu na mashabiki. Anaamini hata nyimbo nne nzuri kwa mwaka zinaweza kuwapa sababu ya kuendelea kumfuatilia.
ANARUDI KWENYE UIGIZAJI 2027
Mimi Mars alijijengea jina katika uigizaji kupitia tamthilia ya ‘Juakali’, ambako aliigiza Maria. Baada ya ajali, shughuli zake za uigizaji zilisitishwa. Sasa anasema amekuwa akipokea ofa na anatarajia kurejea mwaka 2027 kupitia filamu au tamthilia, akiwa na nia ya kujaribu majukumu tofauti.
VANESSA BADO ANA NAFASI
Akizungumzia dada yake Vanessa Mdee, aliyempa msukumo wa kuingia muziki, Mimi Mars anasema anaheshimu maamuzi yake ya kuwa mbali na tasnia. Anaamini Vanessa ana nafasi ya kipekee ambayo haiwezi kuchukuliwa na mwingine. Mashabiki wanamkumbuka kwa kazi zake nzuri na wangependa kumuona akirejea.
Mimi Mars, aliyeanza safari ya muziki 2017, anasema amejifunza uvumilivu, kujiamini na kutokujilinganisha na wengine. Angeutaka ujumbe wake wa zamani usikate tamaa mambo yanapokuwa magumu, kwa kuwa kila changamoto imemfundisha na kumfikisha alipo.
Anasema safari yake bado inaendelea na ana mengi zaidi ya kuonyesha kwa mashabiki wake.