Miaka 30 ya Bongo Flava: Sherehe yenye maswali mengi kuliko majibu
Muktasari:
- Julai 10, 2026 ikawa event ya kwanza. Ukumbi ni Mlimani City, Dar es Salaam. Unaona picha za Ruge Mutahaba, Abdul Bonge na Gadner G Habash.
Jina ni “Miaka 30 ya Bongo Flava”, swali linataka kikokotoo cha hiyo miaka 30 kupata usahihi wake. Waratibu wanaingilia huku wanatokea kule. Hiki ni kioja, unabuni jambo, unalipa jina, halafu huwezi kulitetea. Come on guys!
Julai 10, 2026 ikawa event ya kwanza. Ukumbi ni Mlimani City, Dar es Salaam. Unaona picha za Ruge Mutahaba, Abdul Bonge na Gadner G Habash.
Je, hao pekee ndiyo fallen heroes wa Bongo Flava? Adili Kumbuka “Nigga One” na Robert Mwingira “D Rob” wa Kwanza Unit. Simon Sayi “Complex” na Vivian Tillya “Vivie”, ni couple ya Bongo Flava walioaga dunia kwa ajali ya gari wakiwa pamoja.
Waongeze; Lady Lou na Mac 2 B “Simba” kutoka kundi la Wateule, Abel Loshilaa Motika “Mr Ebbo”, Albert Mangweha “Ngwair”, Zainab Lipangile “Zay B”, Moses Bushagama “Mez B”, Salum Mohammed Salum “Sam wa Ukweli”, na wengine, ni fallen heroes. Mchango wao kwenye Bongo Flava ni dhahiri. Kwa nini hawakukumbukwa, unaweza kukiweka hiki kama kioja namba mbili.
Kuelekea Mlimani City, wanamuziki walionekana wakifanya rehearsals na bendi. Ikawa kichwani kwamba total performance ingekuwa ya live band. Ukumbini shoo tofauti. Mwendo wa playback. Wanamuziki wanaimba juu ya nyimbo. Wengine nyimbo zinazunguka, wao wanazurura jukwaani.
Unapofanya sherehe za miaka ya jambo fulani hiyo ni milestone, ndani yake lazima kuwapo na hadithi. Miaka 30 ya Bongo Flava hakuna simulizi yoyote ya safari ya Bongo Flava. Inafahamika kuwa Bongo Flava ina zaidi ya miaka 30, pamoja na hivyo, waandaaji pamoja na kuukata denge utamaduni, walipaswa kuwa na hadithi ya hiyo miaka 30 waliyojitungia.
Bongo Flava haijajengwa na waimbaji na rappers peke yao. Kuna producers, DJs, watangazaji, waandishi wa habari. Unaadhimisha milestone ya Bongo Flava huna story ya Boniluv, Master Jay, P Funk, Enrico, Taji Liundi “Master T”, Joseph Kusaga, DJ Kim, Mike Mhagama, DJ John Dillinger Matlou, Aboubakar Sadiq, Mahamoud Zubeiry, Zuhura Yunus, Angetile Osiah “Ngetta”, na wengine. Mpaka hapo vioja havijafika vitano?
Watangazaji, DJs na waandishi wa habari walitumia vyombo vya habari walivyokuwa wanavifanyia kazi kuijenga Bongo Flava. Unafanya sherehe ya safari ya Bongo Flava pasipokuwa na hadithi ya vyombo vya habari na majukwaa ambayo yaliwezesha utamaduni huo kuikamata mainstream. Utakuwa unajumlisha mwenyewe. Tutafika 30 tu!
Dudubaya ni kioja kipeo cha pili. Kuanzia Mlimani City, kisha Mwanza, Dodoma hadi Arusha. Ile siku Mlimani City, alitinga jukwaani bwii bin chakalii. Hata kuimba alishindwa. Suruali haikai kiunoni. Hivyo peke yake ni vioja vitatu. Ulevi kazini, unashindwa kufanya kazi uliyolipwa, halafu kwa nini anavaa nguo yenye kiuno kikubwa? Angefunga mkanda basi.
Kioja cha nne alianza kuhutubia badala ya kuimba. Ghafla akaanza kulalamika kwamba aliumwa lakini serikali haikumtibu. Je, hicho ndicho mashabiki walilipa viingilio kushuhudia? Mwendo wa Dudubaya ni uleule wa vioja kwenda mbele. Wimbo unachezwa yeye anahangaika na suruali inayotaka kumponyoka kiunoni. Sauti haitoki. Kisha anasema “yu bera wochi yua baki”.
Kituko kikubwa ni kwamba waandaaji wamekuwa wakisafiri na Dudubaya kila tukio. Mikoa yote. Unajiuliza “Miaka 30 ya Bongo Flava” ni maadhimisho ya vioja vya wanamuziki au kusherehekea utamaduni wenyewe? Maana kama ingekuwa lengo ni muziki na utamaduni, Dudubaya alipaswa kuwa ameshawekwa kando. Hawezi kuperform, isipokuwa ananogesha jukwaa kwa vioja na vitimbi.
Arusha ikawa balaa. Alipanda jukwaani, badala ya kufanya kazi yake, kama kawaida, akawa anapambana na suruali isimvuke. Mwisho akaamua kuwashitakia mashabiki kwamba Ommy Dimpoz aliitwa kwenye Miaka 30 ya Bongo Flava kwa surprise. Akaporomosha maneno mazito dhidi ya Dimpoz, yeye akasema hapo ndipo aliyalainisha. Akazimiwa mic. Katika concerts nne za Miaka 30, Dudubaya kazimiwa mic mara mbili.
Tubaki Arusha, Chidi Beenz ninayemfahamu ni bonge la performer. Mara namwona jukwaani anakimbia mchakamchaka, wimbo unazunguka yeye anakimbiakimbia hovyo, wakati huohuo na yeye anasumbuliwa na tatizo la suruali kumvuka, kwa hiyo anasprint on stage mkono mmoja ukiwa umeshikilia trouser isitengane na kiuno ikawa zahama! Vioja gani hivi?
Baadaye, video inaonesha Chidi akiwa anaamuliwa asizipige. Vioja vinazidi kuongeza. Shida kubwa ni usimamizi holela wa events. Waratibu wanakwenda kwa oyaoya, usela badala ya professionalism. Nidhamu hakuna. Unaruhusu vipi mwanamuziki analewa tilalila halafu apande jukwaani? Mnashindwaje kuwabana wanamuziki watoe performance ya uhakika kimkataba, na kuwaacha wanageuza jukwaa la Miaka 30 ya Bongo Flava kuwa la exhibition, full maonesho?
Tuendelee kuganda Arusha. Jina ni Miaka 30 ya Bongo Flava. Uelekeo ulipokuwa Arusha, jina la Rapper Mr Cheeks wa crew ya Lost Boyz, Marekani likabamba topics zote. Mara, promotion yote haikuwa tena Bongo Flava na safari yake ya miaka 30, bali Mr Cheeks in Arusha. Matokeo yake, badala ya Cheeks kushuka Bongo kuisherehekea Bongo Flava, ikawa kinyume chake.
Bongo Flava ndiyo ilimsherehekea Cheeks Arusha. Basi, tufunike kombe mwanaharamu apite, maajabu yakadhihiri. Cheeks Arusha akagonga playback. Tena bora angekuwa anatoa sauti inasikika, kama Mr Blue na wengine, Cheeks alikuwa anafanya kitu kinachoitwa lip sync. Yaani anatikisa mdomo kuendana na lyrics za wimbo lakini hakutoa sauti. Aibu gani hii?
Kituko kingine kinachoambatana na Cheeks ni Rappar Fid Q. Mwanamuziki akiwa jukwaani pale ni ofisini kwake. Mashabiki wamelipa kiingilio waone kazi, waburudike. Cheeks akiwa jukwaani, Fid Q naye akapanda.
Akaganda jukwaani utadhani yeye ndiye alikuwa backup artist wake. Kitendo hicho ni total unprofessionalism na kilisababisha wanamuziki wengine wa Bongo Flava wawe wanapanda jukwaani na kumkumbatia Cheeks.
Hapa kuna ukweli mchungu kuwa Cheeks aligundua waratibu hawakuwa serious, walikuwa mashabiki wake kuliko kusimama kama mabosi waliomlipa na kumgharamia awepo Tanzania afanye kazi.
Bila shaka, alipoona anashobokewa zaidi, akaona hakuna haja ya kutumia nishati nyingi kupiga kazi jukwaani, akagonga lip sync bila aibu, na ikawa poa, kisha akapaa zake kurejea nyumbani kwao Queens, New York.
Misafara ya Miaka 30 ya Bongo inapambwa na watu wasiohusika na Bongo Flava wala utamaduni huo. Dalali Dotto Magari ndani ya nyumba, mkoa kwa mkoa, wakati kuna wanamuziki wenye alama kubwa na Bongo Flava lakini wameliwa bati.
Hapo kuna vioja viwili kwa mkupuo. Kutomjumuisha legend Mike T, ambaye ameshalalamika mara nyingi kutoitwa, halafu kumbeba Dotto Magari, ni vitimbi viwili, kila kimoja kinajitegemea.
Bongo Movies; Irene Uwoya, Kajala Masanja, Jacqueline Wolper na Aunty Ezekiel ni never miss matukio yote ya Miaka 30 ya Bongo Flava. Unagundua kuna uwekezaji mkubwa unafanywa na waandaaji nje ya muziki wenyewe.
Ongeza kioja kingine kuwa Arusha Mheshimiwa Diwani Janjaro “Dogo Janja”, alipanda jukwaani na Wolper. Angalau ingekuwa walifanya japo rehearsal ili watoe burudani. Ni kama walijadiliana “tupande tukiamshe”. Miaka 30 ya Bongo Flava utani ni mwingi, kazi kiduchu.
Atapanda jukwaani Mheshimiwa Naibu Waziri FA, utaona seriousness. AY, Blue, Jay Moe, na wengine wachache. Halafu wengine, tena wengi wao, wakilikwea jukwaa inakuwa aibu mpaka unatamani muziki uzimwe na kila mtu arejee nyumbani kwao. Mambo haya kwa kiasi kikubwa yanaharibu hadhi na mantiki ya matukio ya Miaka 30 ya Bongo Flava.
Katikati ya matukio, dogo mmoja anatrend anarap. Jina lake “Nyabingi”. Oooh, Nyabingi hapaa! Mratibu wa Miaka 30 ya Bongo Flava, Madee, anaandika mtandaoni, “mwenye namba yake anipe, nataka twende naye Arusha”. Unapata picha kwamba events za Miaka 30 ya Bongo Flava hazina bajeti. Wakati wowote chochote kinaweza kufanyika.
Miaka 30 ya Bongo Flava haikuandaliwa vizuri, ndiyo maana mwenendo umekuwa wa kuziba viraka. Mfano, Hardmad alipolalamika, aliongezwa. Mike T kaliwa bati. Pico wa “Kikongwe” akaongezwa, Barnaba kadhalika.
Mwisho kabisa, unaandaaje shughuli ya milestone ya Bongo Flava bila jina la Sugu “Mr II” kutambuliwa? Kwanza Unit, Saleh Jabir, Mawingu Band ya Othman Njaid, Eliud Pemba na wengine. Vipi studios zilizowezesha Bongo Flava kuwa muziki kinara, story yake ipo wapi? Hili peke yake ni vitimbi zaidi ya 30.