Mfahamu Jihan Dimack,Miss Grand International 2026
Muktasari:
- Jihan ni mrembo wa Kitanzania mwenye uzoefu mkubwa katika ulimwengu wa mitindo na mashindano ya urembo. Mwaka 2026, amerudi tena kwenye jukwaa la kimataifa baada ya kutwaa taji la Miss Grand Tanzania 2026, akiwakilisha Mkoa wa Mwanza. Ushindi ambao ulimpa nafasi ya kuiwakilisha Tanzania katika Miss Grand International 2026, Thailand.
Jina la Miss Grand Tanzania Jihan Dimack limeendelea kujizolea umaarufu kutokana na mrembo huyo kuiwakilisha vyema bendera ya Tanzania hadi kunyakua taji la Miss Grand International leo Oktoba 10,2026 nchini Thailandi. Mfahamu zaidi
Jihan ni mrembo wa Kitanzania mwenye uzoefu mkubwa katika ulimwengu wa mitindo na mashindano ya urembo. Mwaka 2026, amerudi tena kwenye jukwaa la kimataifa baada ya kutwaa taji la Miss Grand Tanzania 2026, akiwakilisha Mkoa wa Mwanza. Ushindi ambao ulimpa nafasi ya kuiwakilisha Tanzania katika Miss Grand International 2026, Thailand.
Jihan ana asili ya Kitanzania na Lebanon, jambo ambalo limempa nafasi ya kukulia na kuishi katika mazingira yenye mchanganyiko wa tamaduni. Kwa mujibu wa wasifu wake rasmi, ameishi Tanzania, Lebanon na Msumbiji, na kwa sasa amekuwa akifanya kazi nchini China katika maeneo ya modeling, mauzo na live commerce.
Safari yake ya modeling ilianza akiwa na umri wa miaka 17, ambapo alianza pia kujifunza umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii, kujitegemea, nidhamu na kuwajibika. Anaeleza kuwa uzoefu wa kuishi katika tamaduni tofauti umemjengea mtazamo mpana kuhusu utofauti wa watu na tamaduni duniani.
SAFARI YAKE KATIKA MASHINDANO YA UREMBO
Jihan si mgeni katika mashindano ya urembo. Amewahi kushiriki katika mashindano kadhaa ikiwemo,
Miss Tanzania 2014
Jihan alishiriki Miss Tanzania 2014, ambapo alifanikiwa kumaliza katika nafasi ya Second Runner-Up (mshindi wa tatu). Uzoefu huu ulikuwa miongoni mwa hatua muhimu zilizomjenga katika safari yake ya urembo.
Miss Universe Tanzania 2016
Mwaka 2016, Jihan alirejea kwenye mashindano na kutwaa taji la Miss Universe Tanzania 2016. Ushindi huo ulimfungulia milango ya kuiwakilisha Tanzania kwenye jukwaa kubwa la kimataifa.
Miss Universe 2016/2017
Baada ya kushinda Miss Universe Tanzania 2016, Jihan alipewa nafasi ya kuiwakilisha Tanzania katika Miss Universe, iliyofanyika nchini Philippines Januari 2017. Uzoefu huo ulimpa nafasi ya kukutana na washiriki kutoka mataifa mbalimbali na kujifunza zaidi kuhusu uwakilishi wa nchi katika mashindano ya kimataifa.
Miss Grand Tanzania 2026
Baada ya karibu muongo mmoja tangu kuonekana kwake kwenye jukwaa la Miss Universe, Jihan alirejea kwenye mashindano ya kitaifa mwaka 2026. Akiwakilisha Mwanza, alitwaa taji la Miss Grand Tanzania 2026 mnamo Agosti 8, 2026.
Ushindi huu ulimrudisha tena kwenye jukwaa la kimataifa, safari hii akawa mwakilishi wa Tanzania katika Miss Grand International 2026 ambayo hatimaye ameibuka mshindi.
Jihan katika Miss Grand International 2026
Katika Miss Grand International 2026, Jihan amejikita katika kuwakilisha Tanzania kupitia ujumbe wa amani, umoja, uvumilivu na kuheshimu tofauti za watu.
Katika kampeni ya “Stop the War and Violence”, amesisitiza umuhimu wa vijana kukataa vurugu na kuchagua mazungumzo, huruma na kuheshimu utu wa kila mwanadamu.
Pia anaamini katika dhana ya 4Bs – Body, Beauty, Brain and Business, akieleza kuwa mwanamke wa kisasa anapaswa kuwa na afya na kujiamini, uzuri wenye tabia njema, elimu na uwezo wa kufikiri, pamoja na kujitegemea na kuwa na uwezo wa kujenga fursa.
Kwa sasa, Jihan anaendelea kuiwakilisha Tanzania katika Miss Grand International 2026, akiwa na uzoefu wa zaidi ya muongo mmoja katika ulimwengu wa modeling na pageantry. Safari yake kutoka Miss Tanzania, Miss Universe Tanzania hadi Miss Grand Tanzania inaifanya historia yake kuwa ya kurudi tena kwenye jukwaa la kimataifa akiwa na uzoefu mpya na malengo mapya.