Mbosso atoke WCB halafu aende wapi?
Muktasari:
- Mbosso aliyeanza safari ya muziki Poteza Records chini ya Sule, alitambulishwa WCB Wasafi hapo Januari 2018 baada ya kuachana na kundi la Yamoto Band ambalo alikuwa na Enock Bella, Beka Flavour na Aslay.
Kama wiki mbili hivi kumekuwa na madai kuwa Mbosso anaondoka WCB Wasafi iliyofanya nayo kazi kwa miaka saba ila Mkurugenzi Mtendaji wa lebo hiyo, Diamond Platnumz ametupilia mbali uvumi huo.
Mbosso aliyeanza safari ya muziki Poteza Records chini ya Sule, alitambulishwa WCB Wasafi hapo Januari 2018 baada ya kuachana na kundi la Yamoto Band ambalo alikuwa na Enock Bella, Beka Flavour na Aslay.
"Tumekuwa na mazungumzo mazuri na Mbosso namna ya kuanza rasmi kusimamia kazi zake na tumekamilisha jambo lake vizuri sana," aliandika Diamond kupitia Insta Story na kuongeza:
"Tafadhali stori yoyote inayozungumzwa kuhusu jambo hili la Mbosso, naomba zipuuzwe hadi pale mimi binafsi na Mbosso tutakapotoa tamko," alisema Diamond, mshindi wa tuzo tatu za MTV EMAs.
Hata hivyo, swali la wengi ni Mbosso atoke WCB Wasafi halafu aende wapi?, chini ya lebo hiyo amefanikisha mengi ambayo ni wasanii wachache huko nje wa kizazi chake wameweza kuyafikia.
Kwa miaka Mbosso amekuwa akitoa kazi mfululizo na kushirikisha wasanii wa nje, mathalani albamu yake ya kwanza, Definition of Love (2021) iliyotoka na nyimbo 12 ilishirikisha wasanii wa kimataifa kama Mr. Flavour, Spice Diana n.k.
Mbosso ni msanii wa kwanza wa WCB Wasafi kutoa albamu na kumshirikisha Diamond kwenye nyimbo mbili kwa wakati mmoja ambao ni Baikoko (2021) na Karibu (2021). Kisha akafuata D Voice kupitia albamu yake, Swahili Kid (2023).
Ikumbukwe Rayvanny hakufanya hivyo katika albamu yake ya kwanza, Sound From Africa (2021), wala Zuchu katika EP yake, I Am Zuchu (2020).
Mwaka uliofuatia Mbosso aliachia EP yake ya kwanza - Khan (2022) yenye nyimbo sita, msanii mkubwa wa kimataifa aliyeshirikishwa ni Costa Titch wa Afrika Kusini.
Zuchu katika EP yake hakupatiwa kolabo ya kimataifa, hivyo hivyo kwa Lava Lava katika EP yake, Promise (2021), ila Mbosso alitafutiwa kolabo ya kimataifa kitu ambacho wenzake walikikosa katika EP zao.
Costa Titch alifanya kazi na Mbosso muda mfupi baaada ya kusikika katika wimbo wa Diamond 'Fresh' kutoka katika EP yake, First of All (2022), pia Focalistic na Papi Cooper walishirikishwa.
Wenzake aliokuwa nao Yamoto Band ambao ni Aslay, Enock Bella na Beka Flavour hawajafanikiwa kupiga hatua kubwa kimuziki kama yeye. Siri kubwa ya mafanikio ya Mbosso ni uwekezaji uliofanywa kwake na WCB Wasafi.
Mbosso ni msanii wa nne Tanzania kufikisha wafuasi milioni 1 YouTube baada ya Diamond, Harmonize na Rayvanny, kisha wakafuata Zuchu, Alikiba, Lava Lava, Nandy, Marioo, Aslay, Rose Muhando, Jux, Jay Melody n.k.
Katika kile kinachoonekana kuwa Diamond amedhamiria, ni kumpitisha Mbosso katika njia zake kwa kumuunganishia kolabo ambazo tayari naye kazifanya.
Mfano Mbosso alimshirikisha Chley katika wimbo wake, Sele (2023) ikiwa ni baada ya msanii huyo wa Afrika Kusini kusikika katika wimbo wa Diamond, Shu! (2023).
Pia Diamond amefanya kitu kama hicho kwa Rayvanny na Zuchu ambao wamefanikiwa kufanya kazi na Innoss'B kutoka DR Congo, vilevile kwa Rich Mavoko aliyefanya kazi na Patoranking wa Nigeria.
Na kutokana na nguvu ya ushiwishi aliyonayo Diamond, amekuwa akifanya kazi nyingi na Mbosso ili kumtangaza zaidi kimataifa, wawili hawa wameshirikiana kwenye nyimbo tano, Jibebe (2018), Baikoko (2021), Karibu (2021), Oka (2022) na Yataniua (2022).
Huyu ndiye msanii pekee wa WCB Wasafi aliyefanikiwa kufanya nyimbo mbili na wazazi wenza wa Diamond ambao ni Hamisa Mobetto na Tanasha Donna, nyimbo walizotoa pamoja ni 'Jibebe' na 'La Vie' kutoka katika EP ya Tanasha, Donnatella (2020).
Jitihada hizo za WCB Wasafi zimezaa matunda baada ya Mbosso kushinda tuzo ya muziki Tanzania (TMA) 2022 kama Msanii Bora wa Kiume wa Bongofleva ikiwa ni tuzo yake ya kwanza kubwa nchini kushinda akiwa kama solo.
Utakumbuka hapo awali Mbosso aliwahi kushinda tuzo kutoka HiPipo Awards 2019 za nchini Uganda ambapo video ya wimbo wake, Hodari (2018) ilishinda kama Video Bora ya Mwaka.
Naye Mbosso amekuwa na mchango katika muziki wa Diamond hasa upande wa uandishi, mfano wimbo wa Diamond, Loyal (2022), awali ulikuwa ni wa Mbosso ila Diamond akavutiwa nao na kumuomba uwe wake na kuujumuisha katika EP yake.
Ikumbukwe Mbosso ni msanii wa sita kutambulishwa na WCB Wasafi baada ya Harmonize (2015), Rayvanny (2016), Queen Darleen (2016), Rich Mavoko (2016) na Lala Lava (2017). Na baada ya Mbosso (2018), akafuata Zuchu (2020) na D Voice (2023).