MB Dog afichua wimbo uliookoa ndoa ya mtu
Muktasari:
- Akizungumza na Mwanaspoti, MB Dog amesema katika safari yake ya muziki amekutana na mashabiki waliomweleza namna nyimbo zake zilivyogusa maisha yao, ikiwemo kuwasaidia kurekebisha mahusiano yaliyokuwa kwenye migogoro.
Mwanamuziki wa Bongo Fleva, Mbwana Mohamed ‘MB Dog’, amefichua namna wimbo wake mmoja ulivyokuwa sehemu ya suluhisho la mgogoro wa ndoa ya shabiki wake, baada ya mwanaume mmoja kumweleza kuwa kazi hiyo ilimsaidia kurejeana na mkewe baada ya kutengana.
Akizungumza na Mwanaspoti, MB Dog amesema katika safari yake ya muziki amekutana na mashabiki waliomweleza namna nyimbo zake zilivyogusa maisha yao, ikiwemo kuwasaidia kurekebisha mahusiano yaliyokuwa kwenye migogoro.
Katika simulizi hiyo, msanii huyo amesema mmoja wa mashabiki wake alimweleza kuwa wimbo wake wa ‘Siuliniambia’ ulimsaidia kurejesha uhusiano na mkewe baada ya ndoa yao kupitia kipindi kigumu.
Mbali na simulizi hiyo, MB Dog amesema amekuwa akikumbana na mashabiki wanaoonyesha hisia kali wanapokutana naye, kiasi cha baadhi yao kushindwa kujizuia na kuishia kulia kwa furaha au kutokana na kuguswa na kazi zake.
“Kitu kikubwa ambacho siwezi kukisahau ni kuwa kuna watu walikuwa wakiniona, wakijua ni kama MB Dog, walikuwa wanalia yaani,” amesema.
Amesema hali hiyo imemfanya atambue kuwa muziki wake haukuwa burudani pekee, bali ulikuwa na nafasi kubwa katika maisha ya watu, hasa wale waliokuwa wakipitia changamoto za kimapenzi.
“Nimeamini kuna kitu nilikifanya katika zile nyimbo, zilikuwa zinagusa mioyo ya watu kupitia hizo kazi,” amesema MB Dog.
Miongoni mwa nyimbo zake zinazokumbukwa ni ‘Mapenzi Kitu Gani’, ‘Natamani’, ‘Inamaana’ na ‘Latifa’, ambazo ni sehemu ya kazi zilizochangia kujenga safari yake ya muziki.
Kwa MB Dog, simulizi za mashabiki hao ni ushahidi wa namna muziki unavyoweza kuwa na nafasi kubwa katika jamii, si kwa kuburudisha pekee, bali pia kugusa hisia za watu na kuwa sehemu ya safari yao ya kurekebisha mahusiano.