Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Lava lava; Baada ya WCB, sasa anapigana mwenyewe

LAVA Pict

Muktasari:

  • Baada ya takribani miaka minane ndani ya WCB Wasafi, Lava Lava aliondoka rasmi kwenye lebo hiyo mwaka 2025 na kuanza safari yake nje ya mfumo uliomlea na kumpa nafasi ya kutambulika kwenye soko la Bongo Fleva. Lakini sasa kimya hicho kimeanza kuvunjwa.

KUNA wakati msanii anapoondoka kwenye lebo kubwa, kinachobaki si jina pekee, bali swali ni kama anaweza kuendelea na muziki akiwa mwenyewe. Kwa Lava Lava, hilo ndilo swali lililo mbele yake sasa.

Baada ya takribani miaka minane ndani ya WCB Wasafi, Lava Lava aliondoka rasmi kwenye lebo hiyo mwaka 2025 na kuanza safari yake nje ya mfumo uliomlea na kumpa nafasi ya kutambulika kwenye soko la Bongo Fleva. Lakini sasa kimya hicho kimeanza kuvunjwa.

Agosti 2026, Lava Lava alirudi na ‘Maneno’, kazi iliyotolewa chini ya Bite Gang, timu yake inayosimamia shughuli zake baada ya WCB. Video ya wimbo huo ilitoka Agosti 17, huku taarifa za muziki zikionyesha kazi hiyo imetolewa chini ya Bite Gang.


LAV 01

ALIVYOANZA WCB

Lava Lava hakufika WCB akiwa mtu asiyejua muziki. Kabla ya kusainiwa, alipitia Tanzania House of Talent (THT), taasisi iliyowahi kutoa wasanii mbalimbali wa Tanzania. Baadaye, WCB ilimsainisha mwaka 2017 na akaanza kujenga jina lake kupitia nyimbo kama ‘Tuachane’, ‘Go Gaga’, ‘Niuwe’, ‘Wanga’, ‘Tajiri’ na nyingine.

‘Tuachane’ ndiyo ilikuwa mwanzo wake rasmi wa kutambulishwa kwa nguvu kwenye soko hilo. Video yake ya mwaka 2017 sasa imevuka milioni 29 za YouTube views, ishara kwamba kazi hiyo haikuwa tu hit ya kipindi chake cha mwanzo, bali imeendelea kuwa sehemu muhimu katika safari yake.

Hapo ndipo Lava Lava alipata kitu muhimu katika utambulisho wake. Sauti yake ilikuwa na upande wa mapenzi, melody na nyimbo zilizokuwa rahisi kuingia kwa mashabiki wa Bongo Fleva.


NYIMBO ZAKE ZILISEMA NINI?

Ukiangalia katalogi yake kwenye Spotify, nyimbo kama ‘Ng’ari Ng’ari’, ‘Zilipendwa’, ‘Tajiri’, ‘Basi Tu’, ‘Tuachane’, ‘Utatulia’, ‘Maneno’, ‘Go Gaga’, ‘Tuna Kikao’ na ‘Inatosha’ bado zinaonekana miongoni mwa kazi zinazotafutwa zaidi kwenye ukurasa wake.

Hii inaonyesha jambo moja, Lava Lava hakujengwa kwa wimbo mmoja. Alikuwa na mkusanyiko wa nyimbo ambao uliweza kumweka kwenye ramani kwa miaka kadhaa. ‘Tajiri’ pekee, iliyotoka mwaka 2023, imefikisha zaidi ya views milioni 8.3 za YouTube.


LAV 02

BAADA YA WCB, NINI KILITOKEA?

Hapa ndipo story ya Lava Lava inakuwa ya kuvutia.

Baada ya kuondoka WCB, ukimya wake ulikuwa mkubwa kuliko ilivyozoeleka kwake. Kiu kubwa ilikuwa kuona kama angeweza kuendelea bila nguvu ya lebo iliyomlea.

Na baadaye ukimya huo ukaendelea hadi zaidi ya miezi 10 bila kazi mpya. Kwa msanii ambaye alikuwa amezoea kuonekana kupitia mfumo wa WCB, hiyo ilikuwa nafasi ya kuuliza:

Lava Lava anapoteza nguvu au anajipanga upya?

Jibu bado halijafungwa, lakini ‘Maneno’ imeanza kutoa ishara ya kwanza.


‘MANENO’ NDILO JARIBIO LA KWANZA

‘Maneno’ si kurudi tu na wimbo mpya. Ni kama Lava Lava anajaribu kuanza kujenga sura yake mpya.

Kazi hiyo ilitoka chini ya Bite Gang, ambayo Lava Lava amekuwa akiitumia kusimamia kazi na miradi yake baada ya WCB. Mwaka 2025 alisisitiza Bite Gang haikuwa lebo ya muziki wakati huo, bali timu yake ya kusimamia kazi na miradi yake, huku akisema ana mpango wa kuanzisha lebo baadaye.

Hivyo, tofauti kubwa hapa ni kwamba sasa Lava Lava anapaswa kubeba mzigo ambao awali ulikuwa unagawanywa na mfumo mkubwa wa WCB: kutengeneza kazi, kuitangaza, kujenga mashabiki na kuhakikisha jina lake linaendelea kuwa kubwa.


LAV 03

NAMBA ZINASEMA NINI SASA?

Kwa takwimu za Spotify zilizokusanywa Septemba 2026, Lava Lava ana karibu wasikilizaji 120,000 wa mwezi. Kwenye orodha hiyo ya wasanii wa Tanzania, Rayvanny ana takribani 769K, Harmonize 760K, Mbosso 406K, wakati Rich Mavoko yuko karibu 108K.

Hii si kusema muziki unapimwa na Spotify pekee, kwa sababu YouTube, TikTok, radio, streams za platforms nyingine, shows na mashabiki wa moja kwa moja nazo zina nafasi.

Lakini namba hizi zinatoa picha ya sehemu Lava Lava alipo kwenye streaming kwa sasa.


JE, ANAFANANA NA RICH MAVOKO?

Hapa ndipo mjadala unakuwa mzito. Ndiyo, kuna sehemu zinazofanana, lakini safari zao si sawa kabisa.

Wote ni wasanii waliowahi kuwa sehemu ya WCB na wote walikuwa na msingi wa mashabiki kabla ya safari zao za baada ya WCB.

Rich Mavoko alikuwa mmoja wa wasanii wa mwanzo kabisa wa WCB, kabla ya kuondoka kwenye lebo hiyo. Lava Lava naye alikuwa sehemu muhimu ya kizazi cha wasanii waliokuja kujenga WCB kama brandi kubwa. Tofauti kubwa iko kwenye namna walivyoondoka na hatua walizochukua baada ya hapo.

Kwa Lava Lava, Diamond amesema mwaka 2025 kuwa alimuachia aende bila kumtoza fedha, akieleza alimpa nafasi ya kujisimamia mwenyewe. Kwa upande wa Rich Mavoko, historia ya kuondoka kwake ilikuwa tofauti.

Na leo, namba za Spotify zinaonyesha Rich Mavoko na Lava Lava wako karibu kwenye wasikilizaji wa mwezi, takribani 108K dhidi ya 120K kwa takwimu zilizokusanywa sasa.


LAV 04

HAPO NDIPO SWALI LINAPOZALIWA

Je, Lava Lava anaweza kuvunja mzunguko wa baadhi ya waliotoka WCB na baadaye kupunguza kasi ya muziki? Jibu litaonekana zaidi kwenye kazi zake zinazofuata, si ‘Maneno’ pekee.


WALIOONDOKA WCB, WAMEFANYA NINI?

Historia ya WCB yenyewe inaonyesha kuondoka kwenye lebo hakumaanishi wote watafuata njia moja.

Harmonize aliendelea kujenga kazi yake binafsi hadi Septemba 2026 ana takribani 760K Spotify, katika katalogi yake pia ana nyimbo zenye mamilioni ya streams kama ‘Falling For U’ na nyingine.

Rayvanny naye ameendelea kuwa na mashabiki kubwa ya wanaosikiliza kazi zake, akiwa karibu 769K kwenye takwimu za sasa. Kazi kama ‘Tetema’ na ushirikiano wake mbalimbali bado zinaendelea kuvuta streams.

Mbosso ambaye naye aliondoka WCB, ana takribani 406K wasikilizaji kwenye Spotify kwa sasa. Huku Rich Mavoko yuko karibu 108K.

Kwa hiyo, historia ya waliotoka WCB haijawa mstari mmoja. Wapo walioendelea na kasi kubwa, wengine wakapungua kwenye baadhi ya vipimo, na wengine bado wanajenga upya.

Jambo kubwa kwake si kuthibitisha anaweza kutoa wimbo mmoja. Anatakiwa kuthibitisha anaweza kujenga jina jipya. ‘Maneno’ ni mwanzo.


LAV 05

UKIMYA WAKE UMEKUWA ADUI AU SILAHA?

Kwa upande mmoja, ukimya wa zaidi ya miezi 10 ulikuwa na gharama kwa sababu muziki ni soko linalobadilika haraka. Msanii akikaa muda mrefu bila kutoa kazi, nafasi yake kwenye mazungumzo ya mashabiki inaweza kuchukuliwa na kizazi kingine.

Lakini upande mwingine, ukimya unaweza kumpa msanii nafasi ya kurudi akiwa na kitu kipya. Sasa Lava Lava amerudi.

‘Maneno’ tayari imeingia kwenye YouTube na kwenye platforms za streaming, lakini namba zake bado zinahitaji muda ili kupima kama huu ni mwanzo wa comeback kubwa au ni kurudi kwa muda mfupi. Video hiyo ina zaidi ya wafuasi 400,000 kwa takwimu zilizokusanywa hivi karibuni, huku ikiwahi kuingia kwenye chati za Popnable Tanzania.


LAVA LAVA BADO ANA KAZI MBELE

Lava Lava hawezi tena kupimwa kwa jina la WCB pekee. Sasa anaingia kwenye kipimo kingine, Lava Lava akiwa yeye mwenyewe.

Akiwa WCB, alikuwa sehemu ya mfumo uliokuwa na Diamond, Harmonize, Rayvanny, Rich Mavoko, Mbosso na wengine waliounda historia ya lebo hiyo.

Leo, baadhi ya majina hayo yamejenga njia zao binafsi.

Harmonize ana Konde Gang, Rayvanny ana Next Level Music, Mbosso anaendelea na safari yake binafsi, huku Lava Lava akiwa anajenga upande wake kupitia Bite Gang. Kwa hiyo, hatua inayofuata si kuhusu alikotoka tu, bali atakakokwenda.

Na hapa ndipo ‘Maneno’ inapata maana nyingine. Baada ya ukimya mrefu, sasa ni wakati wa Lava Lava kuacha muziki uzungumze.