Kuanzia AFRIMA hadi AFRIMMA, kote Jux ananyoosha!
Muktasari:
- Ushindi huu wa Jux AFRIMMA, unakuja mwaka mmoja tangu aliposhinda tuzo nyingine kubwa Afrika za All Africa Music Awards (AFRIMA) 2025, hatua inayozidi kumuweka daraja la juu zaidi kimuziki.
STAA wa Bongofleva, Jux ameendelea kufanya vizuri upande wa tuzo akishinda kuanzia Tanzania, Afrika na hata nje ya bara hili kama alivyofanya hivi karibuni katika tuzo za African Muzik Magazine Awards (AFRIMMA) 2026.
Ushindi huu wa Jux AFRIMMA, unakuja mwaka mmoja tangu aliposhinda tuzo nyingine kubwa Afrika za All Africa Music Awards (AFRIMA) 2025, hatua inayozidi kumuweka daraja la juu zaidi kimuziki.
Jux, mwanzilishi wa chapa ya African Boy, wikiendi iliyopita alikuwa miongoni mwa wanamuziki na mastaa wa filamu na michezo Afrika waliotunzwa katika tuzo za AFRIMMA zilizofanyika huko Dallas, Texas, Marekani.
Hizi tuzo za AFRIMMA zilianzishwa na mfanyabiashara wa Nigeria, Anderson Obiagwu. Kwa mara ya kwanza zilitolewa Julai 2014 nchini Marekani zikiwa na lengo la kusherekea kazi za muziki, vipaji na ubunifu kote Afrika.
Katika AFRIMMA 2026, Jux ameshinda kipengele cha Muziki Uliovuka Mipaka akiwabwaga mastaa kutokea Nigeria kama Burna Boy, Rema, Davido, Mr. Flavour, Wizkid na Odel. Wengine ni Aya Nakamura kutokea Mali, na Fally Ipupa wa DR Congo.
Haikuishia hapo, wimbo aliyoshirikishwa na Diamond Platnumz, Joy (2026) maarufu kama Ikweji, ulishinda kipengele cha Wimbo Bora wa Kushirikiana. Joy ni wimbo uliotayarishwa na S2kizzy, huku video yake ikiongozwa na Director Joma.
Hapa Diamond na Jux wamezibwaga kolabo za mastaa kama Bien & Alikiba (Finale), BNXN & Sarz (Back Outside), Davido & Omah Lay (With You), na Patoranking & Ruger (Shake That).
Wengine ni Fally Ipupa & Wizkid (Jam), Jazzworx & Tukuthela (Bengicela), Mr. Flavour & Baaba Maal (Afroculture), na Marvais Djo & Kano Choir (Pile).
Kwa kuwa kipengele cha Wimbo Bora wa Kushirikiana wahusika wote wanapokea tuzo, basi katika AFRIMMA 2026, Jux akawa ameondoka na tuzo zake mbili, hivyo safari yake ya kuzifuata huko Marekani ikawa imefanikiwa kwa asilimia 100.
“Sichukulii hatua hii kama jambo la kawaida, shukrani kwa kila ambaye amekuwa pamoja nami na kuniunga mkono katika safari hii. Huu ni ushindi wenu pia. Juhudi zenu na kuniamini ndivyo zimenifikisha hapa,” alisema Jux baada ya ushindi huo.
Kwa msimu huu ni wanamuziki wawili tu wa Bongofleva walioshinda AFRIMMA, mbali na Jux, mwingine ni Marioo aliyetakata kipengele cha Mwanamuziki Bora wa Kiume Afrika Mashariki, ikiwa ni mara yake ya kwanza pia.
Jux na Marioo wanaungana na mastaa wengine wa Bongofleva kama Diamond, Vanessa Mdee, Ommy Dimpoz, Harmonize na Zuchu, ambao kwa nyakati tofauti walishinda tuzo ya AFRIMMA.
Ikumbukwe wimbo (Joy) uliompatia Jux tuzo ya AFRIMMA 2026, ni kolabo ya nne kufanya na Diamond baada ya hapo awali kuachia ngoma kama Sugua (2019), Enjoy (2023) na Ololufe Mi (2024).
Ushindi huo ni mwendelezo wa Jux kuzinyakuwa tuzo kubwa za Afrika baada ya mwaka uliopita kushinda AFRIMA, tuzo nyingine kwa ajili ya muziki na wasanii wa Afrika ambazo zimekuwa zikifananishwa na AFRIMMA lakini kuna utofauti.
AFRIMMA hufanyika Marekani, wakati AFRIMA hufanyika ndani ya bara la Afrika hasa katika nchi za Nigeria na Ghana. Majina yake ni kama yanataka kufanana ila kuna utofauti ingawa ni mdogo sana!.
Mnamo Januari 2025 huko Lagos, Nigeria, Jux alishinda tuzo ya AFRIMA kama Msanii Bora wa Kiume Afrika Mashariki 2025 baada ya kuwashinda wakali kama Diamond, Marioo na Mbosso kutokea Tanzania.
Wengine ni Bruce Melodie na Element Eleen kutokea Rwanda, Bien (Kenya), Sat-B (Burundi), Yared Negu (Ethiopia), na Joshua Baraka.
Ikumbukwe tuzo za AFRIMA zilianzishwa mwaka 2014 na Mike Dada kutokea Nigeria, na hufanyika kila mwaka na hushirikisha wasanii kutoka nchi zote za Afrika, chini ya ushirikiano na Umoja wa Afrika (AU).
Lengo kubwa la tuzo za AFRIMA ni kutambua na kuthamini vipaji vya muziki barani Afrika pamoja na wanamuziki wenye asili ya Afrika ili wao na kazi zao zipewe nafasi na heshima kwenye soko la dunia.
Ikumbukwe mbali na AFRIMA, mwaka uliopita Jux alishinda tuzo nyingine za kimataifa ikiwemo Jayli zilizofanyika Abidjan, Ivory Coast, alishinda The Headies zilizofanyika Lagos, Nigeria, pia alishinda Trace zilizofanyika Zanzibar.