Kama si Tiwa Savage nani mwingine tena?
Muktasari:
- Tiwa Savage, mkali wa kibao cha Eminado (2013) akimshirkisha na Don Jazzy, licha ya changamoto za maisha binafsi, bado ameweza kufanya mengi kupitia muziki wake.
MWIMBAJI wa Afrobeat na RnB kutokea Nigeria, Tiwa Savage, 46, ni kati ya mwanamuziki wanaotangaza vizuri muziki wa Afrika duniani akiwa na nyimbo zinazovuma kimataifa lakini haikuwa rahisi kufika alipo kwa sasa.
Tiwa Savage, mkali wa kibao cha Eminado (2013) akimshirkisha na Don Jazzy, licha ya changamoto za maisha binafsi, bado ameweza kufanya mengi kupitia muziki wake.
Akiwa na umri miaka 11, Tiwa Savage alihamia London, Uingereza kwa ajili ya masomo, miaka mitano baadaye alianza kazi yake ya muziki.
Kwa kipindi chote alijifunza kwa kuimba nyimbo za wasanii maarufu duniani kama vile George Michael na Mary J. Blige hadi alipokuja kuhitimu chuo cha muziki cha Berklee.
Mwaka 2012, alirejea Nigeria na kusainiwa na Mavin Records inayomilikiwa na Don Jazzy. Tiwa Savage ni miongoni mwa wasanii wa mwanzo kuchukuliwa na lebo hiyo, wengine ni Wande Coal, Reekado Banks na Iyanya.
Baada ya kusaini Mavin Records, haikuchukua muda akaachia albamu yake ya kwanza, Once Upon a Time (2013) ikiwa na nyimbo kali kama Kele Kele Love na Eminado.
Wimbo wake Eminado, ulifanya vizuri ukishika nafasi ya pili kwenye chati ya MTV Base, Official Naija Top 10, huku Jarida la Vanguard likiuweka nafasi ya 10 katika orodha ya nyimbo zilizofanya vizuri mwaka 2013.
Kwa ujumla hadi sasa Tiwa Savage ameachia albamu nne, nyingine ni R.E.D (2015), Celia (2020) na This One Is Personal (2025). Kwa upande wa Extended Playlist (EP) ni mbili, Sugarcane (2017), na Water & Garri (2021).
Hata hivyo, ndoto ya kwanza maishani haikuwa muziki bali uigizaji. Mnano Aprili 2024, katika mahojiano na ABC, alisema amejisikia vizuri baada ya kuigiza filamu ya Water and Garri (2024), kitu ambacho kimemkumbusha ndoto zake.
"Siku zote nilitaka kuwa mwigizaji, siku zote nilitaka kucheza filamu. Hilo ndilo lilikuwa chaguo langu la kwanza kabla ya muziki.
"Hatimaye nilihisi ni wakati sahihi kuigia huko, sikuwahi kutaka kuacha muziki, kwa hiyo ni njia nzuri kwangu kuendelea kuigiza," alisema Tiwa Savage.
Tiwa Savage ameandika na kuimba wimbo wa filamu hiyo ambayo inasimulia kisa cha Aisha, mbunifu wa mitindo kutokea Marekani ambaye anarudi katika nchi yake ya asili kufuatia msiba wa ndugu wa familia.
Utakumbuka pia Tiwa Savage ni miongoni mwa wasanii wa Afrika walioshirikishwa na Beyonce katika albamu yake, The Lion King: The Gift (2019) ambayo ilikuwa maalamu kwa ajili ya filamu ya The Lion King (2019).
Mastaa wengine walioshiriki katika mradi huo ni Yemi Alade Burna Boy, Mr. Eazi, Tekno, Busiswa, Moonchild Sanelly, Salatiel na Wizkid ambaye wimbo alioshirikishwa na Beyonce, Brown Skin Girl (2019) ulishinda tuzo ya Grammy 2021.
Mwaka 2018, Tiwa Savage alishinda tuzo ya MTV EMAs katika kipengele cha Msanii Bora Afrika, ushindi huo ulimfanya kuandika rekodi kama mwanamuziki wa kwanza wa kike Afrika kushinda tuzo hiyo.
Hadi sasa hiyo ndio tuzo ya hadhi ya juu zaidi ambayo Tiwa Savage amewahi kushinda katika safari yake ya muziki tangu alipovuma kwa mara ya kwanza miaka 13 iliyopita.
Tuzo za MTV EMAs chini ya Paramount International Networks zilianza kutolewa Novemba 1994 katika ukumbi wa Brandenburg Gate huko Berlin, Ujerumani. Kwa sasa hufanyika kila mwaka katika nchi yoyote ndani ya bara la Ulaya.
Na kipindi hicho ndipo alishirikishwa na staa wa Bongofleva, Diamond Platnumz katika wimbo wake 'Fire' ambao ulijumuishwa katika albamu yake ya tatu na ya mwisho, A Boy From Tandale (2018) chini ya Universal Music Group (UMG).
Mwanzoni mwa safari yake ya muziki, Tiwa Savage alipendana na meneja wake, Tee Billz ambaye walifunga ndoa Novemba 2013, kisha harusi ikafanyika Aprili 2014 huko Dubai.
Mwaka 2015, wawili hao walijaliwa kupata mtoto wao wa kwanza na wa pekee kwa Tiwa Savage hadi sasa, Jamil Balogun.
Ndoa hii ilikuwa na visanga vingi, na kufikia mwaka 2018 wakaachana rasmi kwa talaka. Tiwa Savage alitaja sababu ya kuachana kwao na kuacha kufanya kazi na Tee Billz kama meneja wake.
Alisema aliachana na Tee Billz kutokana alimuibia, alimuingiza katika madeni pamoja na matumizi ya dawa za kulevya, huku Tee Billz akidai kwa Tiwa Savage alikuwa akimsaliti kwa kutoka na Don Jazzy na 2Face.
Katika mahojiano yake ya hivi karibuni, Tiwa Savage amesema ana mpango wa kuolewa tena lakini kwa umri wake wa miaka 46, anaona mwanaume sahihi kwake anapaswa kuwa na umri walau kuanzia miaka 50 hivi.