Jay Melody aiteka Kenya, zamu ya Mombasa
Muktasari:
- Msanii huyo anayetamba na nyimbo mbalimbali kama ‘Sugar’, Nitasema, Sawa, Nakupenda na nyingine nyingi, anatarajiwa kufanya shoo jijini Mombasa katika tamasha kubwa la Pwani Gat Talent 2026, kwenye viwanja vya Coast Gym Khana.
MSANII wa Bongo Fleva, Sharif Said ‘Jay Melody’, anatarajiwa kufanya shoo nyingine nchini Kenya na kuzidi kujitengenezea jina nje ya mipaka ya Tanzania.
Msanii huyo anayetamba na nyimbo mbalimbali kama ‘Sugar’, Nitasema, Sawa, Nakupenda na nyingine nyingi, anatarajiwa kufanya shoo jijini Mombasa katika tamasha kubwa la Pwani Gat Talent 2026, kwenye viwanja vya Coast Gym Khana.
Jay Melody ambaye amekuwa miongoni mwa wasanii wanaofanya vizuri katika kizazi cha sasa cha Bongo Fleva, amekuwa akipanua wingi wa mashabiki wake katika muziki na shoo jambo linalomfanya azidi kutambulika katika soko la Afrika Mashariki.
Safari yake ya kimataifa mwaka huu imehusisha Kenya, ambako amepata nafasi ya kutumbuiza pia katika maeneo mbalimbali, ikiwemo Lodwar, Eldoret na Nairobi.
Maonyesho hayo yamekuwa sehemu ya safari yake ya kujenga jina nje ya Tanzania, huku mashabiki wa muziki wa Kiswahili nchini humo wakizidi kupata nafasi ya kumuona msanii huyo akifanya kile anachokijua zaidi, kuimba na kuburudisha mashabiki zake.
Tamasha hilo lililoandaliwa na Swahilipot Hub Foundation linatarajiwa kuanza saa 8:00 mchana hadi usiku wa manane, likiwa na burudani zinazohusisha muziki, ngoma, vichekesho, mitindo na mashairi, huku Jay Melody amepewa nafasi ya kuwa msanii mwalikwa mkuu wa kimataifa.
ANAJENGA SOKO
Kutokana na shoo hizo, Kwa Jay Melody anazidi kujenga soko jipya na kuimarisha uhusiano wake na wasanii na mashabiki.
Pia shoo hizo zinampa nafasi ya kukutana na mashabiki wapya ambao huenda walikuwa wakimfahamu kupitia mitandao ya kijamii na majukwaa ya kusikiliza muziki pekee.
Jay Melody pia anaendelea kuwa sehemu ya kizazi cha wasanii wa Bongo Fleva wanaotafuta nafasi ya kuifanya Tanzania isibaki kuwa soko la muziki pekee, bali iwe chanzo cha burudani kinachoweza kuvuka mipaka.
Hivyo, jukwaa la Pwani Gat Talent litakuwa sehemu nyingine ya kuimarisha jina lake katika soko la Kenya na Afrika Mashariki kwa jumla kama ilivyo kwa waliomtangulia akiwamo Diamond Platnumz, Zuchu,Harmonize, Rayvanny, Alikiba na wasanii wengine.