Irene Uwoya: A-List ya kweli ni hii!
Muktasari:
- Kipindi hicho kilianza kuonekana kwenye mitandao ya kijamii kabla ya kutinga kwenye televisheni.
KUTOKANA na kuanzishwa kwa kipindi cha A-List kinachofanywa na waigizaji wakongwe Irene Uwoya, Jacqline Wolper, Aunt Ezekiel na Kajala Masanja, kumekuwapo na kuibuka kwa vipindi vya wasanii wengine vinavyofanana na hicho.
Akizungumzia hilo, leo Septemba 7, 2026, Irene Uwoya baada ya kuitikia wito wa Bodi ya Filamu nchini, amesema wao wanaitambua A-List yao na siyo vipindi vingine vinavyojitokeza baada yao.
“Tunachokijua sisi ni A-List yetu na sio vilivyokuja baada ya sisi lakini wanaotuiga tunawakubali wanachofanya, "amesema Irene.
Pia amesema kuwa A-List ya kiume iliyoanzishwa na wachekeshaji maarufu akiwemo Azaboi, Mtumishi Obama, Kipotoshi na Ngosha, ndio wanayoitambua kwa sasa.
A-List ni kipindi ambacho kinawakutanisha waigizaji hao wanne, kuwapa nafasi ya kuzungumza kwa uwazi kuhusu maisha yao, urafiki, kazi na mambo mbalimbali ambayo yamekuwa yakizungumzwa kuhusu wao.
Kipindi hicho kilianza kuonekana kwenye mitandao ya kijamii kabla ya kutinga kwenye televisheni.
Hata hivyo, maudhui ya kipindi hicho yamekuwa yakileta mjadala kutokana na baadhi ya mazungumzo yao kugusa maisha yao binafsi, mahusiano na mambo ambayo awali hayakuwa yakijulikana kwa umma.