Bodi ya Filamu yawaonya Aunt Ezekiel, Wolper, Uwoya na Kajala
Muktasari:
- Mastaa hao ambao wanatajwa kuwa miongoni mwa waigizaji wa kundi la A-List, leo Septemba 7, 2026, wamefika katika ofisi za Bodi ya Filamu Tanzania baada ya kuitwa na Bodi hiyo.
KATIBU Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dk Gervas Kasiga amewataka waigizaji wakongwe nchini, Aunt Ezekiel, Jacqueline Wolper, Irene Uwoya na Kajala Masanja, kuwa na weledi katika kazi zao za sanaa.
Mastaa hao ambao wanatajwa kuwa miongoni mwa waigizaji wa kundi la A-List, leo Septemba 7, 2026, wamefika katika ofisi za Bodi ya Filamu Tanzania baada ya kuitwa na Bodi hiyo.
Akizungumza baada ya kukutana na wasanii hao, Dk Kasiga amesema wameitwa kwa ajili ya kupewa onyo na kukumbushwa wajibu wao kama wasanii wakongwe katika tasnia ya filamu, hususan kupitia kipindi chao cha A-List .
Amesema baadhi ya maeneo yanayoonekana katika kipindi hicho hayana maadili yanayostahili, hivyo kama wasanii wakongwe na walezi katika tasnia wana wajibu wa kuhakikisha kazi zao zinazingatia weledi.
“Tumewaita kuwapa onyo kwenye kazi zao za sanaa, pia kuwaelekeza wafanye kwa weledi kwa sababu ni wasanii wakongwe. Nyuma yao kuna mabinti wadogo ambao wanawaangalia na kujifunza kutoka kwao. Katika kipindi chao cha A-List kuna baadhi ya maeneo ambayo hayana maadili, hivyo sisi kama walezi tuna jukumu la kuwakumbusha,” amesema Dk Kasiga.
Amesema nafasi waliyonayo katika tasnia inawafanya kuwa watu wa kuigwa na kizazi kipya, hivyo wanapaswa kuzingatia mwenendo na namna wanavyotekeleza kazi zao za sanaa.
Kwa hatua hiyo, Bodi imewataka mastaa hao kutumia uzoefu wao kujenga tasnia na kuwa mfano mzuri kwa wasanii wanaochipukia nchini.