Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

HADITHI: Zindiko (sehemu ya 24)

Muktasari:

  • Huu ni mwendelezo wa hadithi ya ZINDIKO iliyojaa visa na mikasa ya kimaisha kutoka kwa mtunzi mahiri wa riwaya, SULTAN TAMBA. Twende naye...

RAS Kim akacheka.

“Inawezekana ee, kweli – uwepo wa maisha ya Joka la Zindiko kumesaidia kuliweka jengo hili kwenye hali ya usalama hadi leo nimekuja na kulikuta hivi.”

Kisha Mzee Zimataa akatulia kimya, kama anayewaza kitu. Simanzi zilimrudia! Kila alipomkumbuka Zaka, alikuwa anajikuta amekumbuka kitu kikubwa sana.

“Bw. Kim. Umefanya vizuri sana kuja. Kwa sababu umekuja wakati muafaka. Umekuja wakati wa vita.”

Ras Kim akamgeukia Mzee Zimataa.

“Unaposema vita unamaanisha nini.”

“Diwani ameapa kuhakikisha jengo hili linavunjwa au zindiko linaondolewa ili watu wawe huru kufika hapa.”

Kim anatabasamu.

“Bila shaka yeye sio wa kwanza kufanya hivyo. Kuna majabali na majabali yaliyojaribu lakini waliishia njiani. Ila kuna mahali nimeshangaa, watu wawe huru kufika hapa? Kwa nini... Kwani ni lazima kila mtu afike hapa. Tumeweka na uzio kwamba wapite kule kwingine. Kwa nini hapa?”

“Labda yeye mwenyewe anaweza kufafanua. Lakini hili jambo limenikosesha amani sana, hata hapa akili yangu inawaza jambo hili ndio maana nimeharakisha kukwambia.”

“Anajidanganya. Hawezi kufanya chochote, wala asikupe wasiwasi. Wataishia kulekule walikoishia wenzake!”

“Inawezekana unachosema ni kweli, lakini amefika mbali sana. Ameweza kuvunja mwiko ambao sikuwahi kuwaza kama wataweza. Na kwa kukuongezea tu, anashirikiana na Mbunge wa jimbo hili. Anataka kujimilikisha jengo hili kwa udi na uvumba.”

Kim anarudia kukataa kwa kutingisha kichwa. Kisha analiangalia jengo kwa hisia. Ni katika hali ya kujiamini. Anajiamini kwa sababu anafahamu sifa za Jiwe Jekundu. Anafahamu nguvu ya Jiwe Jekundu, kwamba hata siku moja halisaliti ahadi yake.

Jiwe Jekundu ndilo nguzo iliyoko pale, ndiyo nguzo iliyoleta Joka la Zindiko pale. Kwa hiyo alikuwa anajiamini kwa kitu anachokijua.

“Hawawezi. Usiwe na wasiwasi. Na wala wasikutishe.”

Mzee Zimataa anamtazama kwa hisia. Kisha anageuza shingo na kuangalia mtungi.

Mtungi umelala kidogo, hauko sawa.

Mzee Zimataa anashangaa.

Mzee Zimataa anarudi kwenye jengo na kuuangalia vizuri ule mtungi. Anapojiridhisha, anauweka sawa na kumfuata tena Mzee Zimataa.

“Joka lilitoka. Nahisi itakuwa ni usiku wa jana. Sijui limemdhuru nani.”

“Kumbe? Lakini huwa unajuaje kama joka lilitoka.”

“Kuna ishara huwa naiona. Mtungi huwa unakaa upande kidogo. Na ndivyo nilivyokuta. Na hii sio kawaida. Imenishangaza kwa kweli.”

Wakati Mzee Zimataa akionyesha kushangaa kwa jambo hilo, Ras Kim naye alikuwa anamshangaa yeye!

“Mbona kama unanishangaza. Ina maana Joka la Zindiko kutoka na kuchukua maisha ya wanaojaribu kuingia humu ndio jambo linalokushangaza? Mbona sijakuelewa.”

Mzee Zimataa hakuacha kushangaa. Sura yake ilionekana wazi kwamba lile jambo limemduwaza.

“Nisikilize bosi, Joka la Zindiko hutoka nje kwa sababu mbili tu, moja ya kuzindika dawa zangu na pili ni kumchukua mtu yeyote anayeingia humu. Lakini likitoka mimi ntajua tu. Mtungi lazima utakaa vibaya, kama vile nilivyoukuta.”

“Sasa kinachokushangaza ni nini. Mbona unaniweka kwenye mabano. Kama halikutokea kwa ajili ya kuzindika dawa zako, basi labda kuna mtu alikatiza, likamshambulia, au hilo kwako ndiyo jambo la kukushangaza?”

Mzee Zimataa akakubali kwa kichwa, lakini bado sura yake bado ilikuwa imeuvaa mshangao uleule.

“Lakini... Mbona kama sio kawaida... Hisia zangu hazinipeleki huko, yaani naona kama vile lipo jambo jingine lililolitoa joka nje. Inanichanganya kidogo!”

“Bwana Zimataa, ujue unaniweka kwenye maswali sana. Mbona kama unataka kumaanisha aina ya jambo ambalo halieleweki. Joka la Zindiko kutoka nje imekuwa ni ajabu kwako? Uko sawa kweli lakini wewe?”

Mzee Zimataa alikuwa kama vile hamsikilizi Ras Kim! Akili yake ilikuwa mbali.

Muhuri aliouona kwa Zaka ulimfanya aanze kuhisi kitu kingine zaidi. Labda joka lilitoka kwa ajili yake?

“Au inawezekana limetoka kwa ajili yake? Ina maana dawa alizokuja nazo zina nguvu kiasi hiki?”

Kim alimtazama kwa mshangao zaidi.

“Lilitoka kwa ajili yake? Mbona sikuelewi. Nani huyo?”

Mzee Zimataa alikuwa kama aliyekabwa na dukuduku! Yaani ile hali ya kuwa na kitu kinachokuwashawasha kukisema! Mdomo hautulii na akili haitulii – lakini aidha alikuwa anasubiri ruhusa au pa kusemea!”

Sasa akawa amepata!

“Bw. Kim. Ngoja nikwambie kitu.”

Akaweka pozi kidogo ili akili yake ipate sentensi nzuri za kumwambia Kim ambaye alikuwa akimtazama katika hali ya shauku ya kusikia kile ambacho anataka kumwambia.

“Mimi sishangai kwa bahati mbaya. Nina uzoefu wa kuwa hapa kwa miaka 20. Kwa wiki nafika hapa mara tatu au nne! Huwa naleta dawa hapa mara moja au mbili kwa wiki! Mambo haya nayafanya kwa miaka 20 sasa. Kwa hiyo unaponiona nashangaa kama hivi, ujue mshangao wangu una maana kubwa!”

Ras Kim alitulia akimtazama.

“Tangu niwe msimamizi wa jengo hili miaka 20 iliyopita, sijawahi kuona mtu akifika hadi hapa kisha akatoka salama. Mtu yeyote akikanyaga ndani ya usio, ghafla atajikuta anatazamana na Joka la Zindiko! Na hapo unakuwa mwisho wa maisha yake! Kwao wanaishia kuweka matanga tu kwa sababu mwili unakuwa umeshazikwa ndani ya tumbo la joka hili.

“Lakini uadui ulioingizwa hapa kwa sasa unanitisha, ni uadui mkubwa na wenye nguvu kubwa sana. Hivi unaweza kuamini nikikwambia kwamba maadui wamemwogesha dawa kijana mmoja, ili aweze kufika hapa bila kudhurika ili kuweka au kufanya uchawi ndani ya jengo kwa lengo la kupunguza makali ya zindiko. Unaweza kuamini hilo?

Kim akakataa kwa kutingisha kichwa chake.

“Hilo haliwezekani. Huyo kijana akikanyaga hapa atapoteza maisha yake papo kwa hapo. Kama unamfahamu mwambie asithubutu kufanya hivyo, watamponza,” Ras Kim aliongea kwa kujiamini.

“Unaongea kitu kisichowezekana Mzee. Hata wafanye nini hawezi kugusa mtu ardhi hii iwe kwa ubaya au uzuri. Iwe ndani au nje. Joka la Zindiko lina nguvu za ziada za Jiwe Jekundu, na wewe unajua hilo. Jiwe Jekundu halijawahi kukiuka kiapo. Lilishindikana tangu zama hizo ambazo walikuwepo watu wenye nguvu na uwezo wa kila aina. Litashindwa nguvu leo?

“Labda leo nikupe elimu ambayo imekupita mbali kidogo kuhusu Jiwe Jekundu. Hili jiwe mojawapo kati ya mawe matatu yaliyokuwa na nguvu kubwa sana katika zama za wafalme wa Misri ya kale. Zama za wale mafirauni. Haya mawe, yalikuwa yanachimbwa kwa ajili ya matumizi mbalimbali na yalikuwa ndani ya jiwe moja.

“Yaani kulikuwa na jiwe moja kubwa sana na lilikuwa na rangi tatu. Yaani limegawanyika kwa rangi tatu – rangi ya katikati ilikuwa nyekundu, hizo nyingine mbili sitazisema kwa sababu Mwandishi Sultan Tamba atasimulia mwenyewe kwenye riwaya na filamu zake – maana yeye anayajua hayo kwa vizuri sana.

“Kuna hadithi nyingi ambazo Sultan Tamba anazo kuhusu mawe haya, mtafute yeye atakusimulia – mimi nakwambia kuhusu hili Jiwe Jekundu. Lina nguvu sana na nguvu zenyewe zinahusu uhai wa binadamu. Lina uwezo wa kukatisha maisha ya mtu yeyote na kurudisha uhai wa yeyote.

“Wapo watu waliopotea au kufa zamani sana, lakini walikuja kuonekana baadaye katika maisha ya kawaida – japo wanaporudi, wanakuwa katika hali nyingine, si hali ya ukamilifu wa mwili na akili kama mimi na wewe tulivyo. Ipo hadithi inayoitwa Jiwe Jekundu ambayo mwandishi Sultan Tamba atakuja kuisimulia hapo mbele, yenyewe ilimhusu mwanamke aliyekufa miaka 20 iliyopita na akazikwa hadi kaburi lake linajulikana lilipo, lakini alirudi duniani na kuja kuleta balaa kubwa kwa mumewe wa zamani ambaye tayari alikuwa ana mke mwingine.

“Hata hapa, ikijulikana kwamba nguvu zinazolinda jengo hili ni nguvu za Jiwe Jekundu tunaweza kuingia kwenye shida kubwa kwa sababu serikali zote duniani zimekubaliana kwamba popote pale akikutwa mtu na Jiwe Jekundu basi hukumu yake ni kifo.”

Mzee Zimataa alimtazama kwa makini aliyokuwa akiyaongea.

Kisha Kim anaonekana kusita kuzungumza, anatuliza macho kwenye jengo. Akili yake inaonekana kuhama, inakwenda mbali!

“Lakini hebu tuliache hilo. Nataka nikwambia jambo. Matokeo haya ya miaka 20 ya jengo kuishi bila mtu na kutotokea kitu nilichokitegemea, yananipa simanzi kubwa sana.”

Inaendelea...