Garcia kwenye penzi na Lamine Yamal
Muktasari:
- Yamal ambaye kwa miezi ya hivi karibuni alikuwa bize zaidi na maisha ya soka baada ya kuachana kwake na rapa na mwimbaji kutoka Argentina, Nicki Nicole, sasa anaonekana kuanza maisha ya uhusiano na mwanadada huyo maarufu mwenye miaka 21.
MWANAMITINDO na mwanamitandao maarufu, Inés García kutoka Sevilla, Hispania, ameonekana kwenye sherehe za ubingwa wa La Liga na kiungo mshambuliaji wa Barcelona, Lamine Yamal.
Yamal ambaye kwa miezi ya hivi karibuni alikuwa bize zaidi na maisha ya soka baada ya kuachana kwake na rapa na mwimbaji kutoka Argentina, Nicki Nicole, sasa anaonekana kuanza maisha ya uhusiano na mwanadada huyo maarufu mwenye miaka 21.
Mei 20, 2026, Barcelona iliandaa hafla maalumu ya kusherehekea kutwaa ubingwa wa La Liga na baadhi ya wachezaji walifika sambamba na wenzi wao.
Hata hivyo, ujio wa Yamal akiwa na Inés ndiyo uliogeuka gumzo kubwa zaidi miongoni mwa mashabiki na vyombo vya habari vya Hispania baada ya siku chache wawili hao kuhusishwa kuwa kwenye penzi zito.
Ingawa wawili hao walijitahidi kuwa watulivu na kuepuka kuvuta hisia nyingi kwa vyombo vya habari, lakini mashabiki waligundua haraka ukaribu wao jambo lililoonekana kuthibitisha uvumi uliokuwa ukisambaa siku za hivi karibuni.
Sherehe hiyo ambayo awali ilikuwa maalumu kwa ajili ya mafanikio ya Barcelona msimu huu, ilibadilika na kuwa usiku wa kipekee kwa staa huyo kijana ambaye anaendelea kung’ara ndani ya kikosi hicho.
Wawili hao walionekana kwa mara ya kwanza Ugiriki wiki iliyopita wakati wa mapumziko kabla ya ubingwa huo na kuzua mjadala mkubwa mitandaoni.
Mbali na hilo, Inés aliwahi kuweka picha akiwa La Cúpula del Garraf jijini Barcelona kabla ya wawili hao kuonekana wakiondoka pamoja ndani ya gari aina ya Van nyeusi.
Baadhi ya mashabiki wamekuwa wakijadili tofauti ya umri kati yao kwani Inés ana umri mkubwa akimzidi kinda huyo wa timu ya Taifa ya Hispania zaidi ya miaka miwili, lakini hilo linaonekana siyo kikwazo kwao.
Awali nyota huyo alikuwa kwenye uhusiano na Nick Nicole, rapa na mwimbaji kutoka Argentina ambaye alimzidi zaidi ya miaka mitano.
Pamoja na gumzo linaloendelea kuhusu maisha yake binafsi, Yamal anaendelea kuwa mmoja wa wachezaji muhimu Barcelona na anatarajiwa kurejea uwanjani hivi karibuni baada ya kutoka kwenye majeraha.
Yamal amejumuishwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Hispania kwa maandalizi ya Fainali za Kombe la Dunia 2026 zitakazofanyika Marekani, Mexico na Canada, lakini ataikosa mechi ya kwanza ya kundi H dhidi ya Cape Verde itakayopigwa Juni 15, mwaka huu.