Chidi Benz arekodi ngoma sita na Mond, Kiba
Muktasari:
- Chidi Benz ni mmoja wa wasanii walioshirikishwa sana katika Bongofleva, na moja ya kolabo hizo ilishinda tuzo mbili kwa mpigo. Je, ni ipi hiyo? Twende pamoja!
MWANAMUZIKI Chidi Benz ni rapa mwenye ushawishi na heshima kubwa katika muziki wa Hip Hop hapa Bongo kutokana na kile ambacho amekifanya kwa miaka zaidi ya 20 katika tasnia.
Chidi Benz ni mmoja wa wasanii walioshirikishwa sana katika Bongofleva, na moja ya kolabo hizo ilishinda tuzo mbili kwa mpigo. Je, ni ipi hiyo? Twende pamoja!
1. Hadi Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) zinasimama mwaka 2015, Chidi Beenz alikuwa ameshinda mara tano, ambapo mara ya kwanza alishinda mwaka 2006 kupitia wimbo wake, Naitwa Nani (2006) akimshirikisha K-Lynn.
2. K-Lynn ambaye ni Miss Tanzania mwaka 2000, alikuwa mwanamuziki wa kwanza wa kike maarufu kushirikishwa na Chidi Beenz, kisha wakafuata wengine akiwemo Ray C ambaye walirekodi ngoma mbili pamoja.
3. Baada ya Chidi Benz kutotokea katika video ya wimbo wake Lady Jaydee, Upo Juu (2009) ambao alishirikishwa, vesi yake iliondolewa katika toleo hilo la video. Kitu kama hicho kilimtokea Nay wa Mitego baada ya kushindwa kushuti video ya wimbo wa Harmonize, Bedroom Remix (2020) ambao ulikutanisha wasanii wengi akiwemo Darassa, Billnass, Rosa Ree, Young Lunya na kadhalika.
4. Watayarishaji muziki ambao wametengeneza nyimbo kali za Chidi Beenz ni pamoja na Dunga (41 Records), P-Funk Majani (Bongo Records), Pancho Latino (Dhahabu Records), Lamar (Fish Crab) na kadhalika.
5. Pancho ndiye aliyetengeneza wimbo wa Chidi Benz, Dar es Salaam Standup (2009) ambao ulishinda tuzo ya Muziki Tanzania (TMA) 2009 katika kipengele cha Wimbo Bora wa Rap. Wakati huo Pacho alikuwa akifanya kazi katika studio hiyo ya Dully Sykes kabla ya kuhamia B'Hits kwa Hermy B, ambaye ametengeneza wimbo wa Chidi Benz na Ray C, Beibi (2008).
6. Chidi Benz amesikika katika nyimbo nyingi za Hip Hop ambazo zimekutanisha wasanii wengi, alifanya hivyo katika wimbo wa Nako 2 Nako Soldiers, Mchizi Wangu Remix (2009). Mbali na Chidi Beenz, wasanii wengine waliosikika katika wimbo huo ni pamoja na Fid Q, Mansu Li, Mh Temba, Mwana FA, Geez Mabovu, Babuu wa Kitaa, Ibra Da Hustler, Jay Moe, Adam Mchumvu, Lord Eyes n.k.
7. Pia Chidi Benz alifanya hivyo katika wimbo wa JCB, Ukisikia Paah (2010) ambao Fid Q na Jay Moe walishikishwa. Wimbo huo ulishinda tuzo mbili za Muziki Tanzania TMA (TMA) 2011 ukishinda kipengele cha Wimbo Bora wa Hip Hop na Wimbo Bora wa Kushirikiana.
8. Kwa JCB, msanii wa kundi la Watengwa, pamoja na Jay Moe hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza kushinda tuzo ya TMA ila kwa Chidi Beenz na Fid Q tayari wao walikuwa wameshashinda tuzo hizo mara kadhaa huko nyuma.
9. Je, wajua kuwa Chidi Benz amefanya kolabo tatu na Diamond Platnumz lakini cha kuchangaza hakuna hata moja ambayo video yake ilifanyika?, ndiyo, wamerekodi nyimbo tatu ila hawajashuti video hata moja. Nyimbo hizo ni Nalia na Mengi (2012), Mpaka Kuche (2014) ambao AY pia alishirikishwa, na Tunaishi Nao (2023). Wimbo wa kwanza ni wake Diamond, na hizo mbili za mwisho zake Chidi Benz.
10. Hata hivyo, mshindani wa Diamond, Alikiba, naye ameshirikiana na Chidi Benz katika nyimbo tatu, Hasira za Nini (2008), Far Away (2010), na VIP (2026), huku nyimbo mbili za mwisho zikipata video.